loader
Picha

Sababu za wasichana kuacha shule zabainishwa

UTUMIKISHWAJI wa watoto wa kike ili kusaidia familia, umaskini, mazingira magumu kwenye shule, mimba za utotoni ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wasichana kuacha shule katika wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa mahojiano jana, Mratibu wa Programu wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Marafiki wa Elimu Dodoma (MED), Luhaga Makunja alisema kuna idadi kubwa ya wasichana wanaoacha shule kutokana na sababu mbalimbali. Alisema shirika hilo lilikuwa likitekeleza mradi wa kutatua changamoto za unyanyasaji wa kijinsia katika elimu ya msichana ambapo eneo la mradi lilikuwa kata nne za Chibelela, Mapanga, Mtitaa, Mwitikila na Chipanga. Alisema mradi huo ulilenga watoto wetu umri kuanzia tisa hadi 19 ambao wako shuleni.

“Ukatili mkubwa tuliouona ulikuwa ni kuachishwa masomo kutokana na mimba za utotoni,” alisema. Alisema kulingana na takwimu walizopata kutoka Idara ya Elimu wasichana 3,179 walioanza shule 2013 miongoni mwao 1,238 hawakumaliza kidato cha nne mwaka 2017 ambapo ni asilimia 39 sababu kubwa ikiwa ni mimba za utotoni. Makunja alisema tulikuwa na wasichana kutumikishwa kazi za majumbani ambapo wasichana wamekuwa wakiachishwa shule na kwenda mijini kufanya kazi za ndani kusaidia familia.

“Bado kuna mila na desturi ambazo hazioni thamani ya mwanamke kwenye elimu hata inapofikia umri wa mtoto kuandikishwa shule suala la kusoma linaokana sio muhimu,” alisema. Makunja alisema umasikini, utumikishwaji wa watoto kusaidia familia, mazingira magumu shuleni kutokana na umbali kutoka makazi Hadi shuleni inaonekana ni kikwazo cha elimu kwa mtoto wa kike.

“Kuna wanafunzi wanalazimika kwenda kupanga vijijini ili wawe karibu na shule, wanakosa ulinzi wa wazazi na kujikuta wakiingia kwenye ngono na hivyo wengi hujikuta wakikatisha masomo kutokana na ujauzito,” alisema. Pia alisema mazingira magumu ya nyumbani hupelekea watoto kufika shule wakiwa hawajala huku akitembea umbali mrefu kufika shuleni.

“Anatoka nyumbani hajala anakaa muda mrefu na njaa, hata masomo haelewi vizuri anajua atafeli tu alishakata tamaa anaona amalize tu shule,” alisema. Makunja alisema ukosefu wa mabweni na chakula unasababisha watoto kutoshawishika kwenda shuleni.

Alisema kumekuwa na mtazamo hasi wa wazazi na walimu juu ya elimu kwa wasichana. “Jitihada kubwa zinahitajika kuhakikisha elimu inatolewa ili kupunguza unyanyasaji wa kijinsia unaosababisha wasichana kukosa elimu,” alisema. Pia alisema wasichana wengi walikuwa hawashiriki katika maamuzi hata kwenye mipango ya shule na vijiji.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi