loader
Picha

‘Kuna faida lukuki kuvuna mkaa kwa njia endelevu’

Machi 7 mwaka huu, kulifanyika Maonesho ya Wazi ya shughuli zinazofanywa na wanakijiji cha Mlilingwa kilichoko Ngerengere, Morogoro vijijini kama sehemu ya mafanikio ya mradi wa kuleta mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS).

Mradi huu unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi maarufu kama ‘Mkaa Endelevu’, unaendeshwa na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa kushirikiana na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (TaTEDO).

Mkurugenzi wa MJUMITA, RAHIMA NJAIDI alifanya mahoajini na waandshi wa habari na kufafanua mengi kuhusu mradi na maana ya maonesho hayo kama makala haya yaliyoandikwa na HAMISI KIBARI yanavyofafanua. SWALI: Tueleze lengo kuu la kufanya maonesho haya ya mkaa endelevu. Jibu: Leo tuko hapa Mlilingwa, Kata ya Tunanguo, Tarafa ya Ngerengere, Wilaya ya Morogoro kwa ajili ya kufanya hili tamasha la Mkaa Endelevu.

Lengo ni kwamba, tunataka kuonesha jamii na umma kwa ujumla kuhusu shughuli zetu za mradi wa Mkaa Endelevu. Tunataka Watanzania wafahamu shughuli zinafanyikaje na pia kuwaonesha wadau wa mradi ambao ni wananchi wanaojihusisha katika mradi huu namna wanavyonufaika. Lengo lingine ni kupaza sauti kwa serikali, kwa wilaya na mikoa mingine kuona mbinu ambazo tunafanya huku Mlilingwa pamoja na vijiji vingine 30 vinavyotekeleza mradi huu wa TTTCS, ili kuona namna wanavyoweza kuutekeleza katika maeneo yao.

Swali: Tueleze kwa kifupi mradi unavyofanyika. Jibu: Kama mlivyosikia kwa wazungumzaji mbalimbali, mradi ulianzishwa kwa kuzingatia kwamba Watanzania wataendelea kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa miongo kadhaa lakini kwa sasa mkaa unavunwa kwa njia holela na hivyo kuharibu mazingira. Mradi unalenga kuwawezesha wananchi wazalishe mkaa kwa njia ambayo ni endelevu na kuwafanya waone faida ya misitu yao na hivyo kugeuka kuwa walinzi madhubuti wa raslimali za misitu. Haya yote yamefanikiwa.

Mradi huu unaanza kwa kijiji kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi na kisha kutenga wastani wa asilimia 10 ya eneo la msitu wa kijiji kwa ajili ya uvunaji wa mkaa. Ndani ya asilimia hiyo 10 ya msitu hutengwa tena vitalu vyenye urefu wa mita 50 kwa 50 kupitia picha za satelaiti na kupimwa kwa teknolojia ya GPS. Katika kitalu, siyo kila mti unavunwa. Miti ya mbao, miti iliyoko katika vyanzo vya maji au ambayo ni mapango ya wanyama huachwa. Miti kadhaa kwenye kitalu pia kuachwa ili kulinda ikolojia ya eneo hilo.

Vitalu huvunwa kwa njia ya kuruka kitalu kimoja kwenda kingine kwa usimamizi wa Kamati ya Maliasili ya kijiji. Lengo ni vitalu vinavyovunwa leo kurudiwa baada ya miaka takribani 20 ambapo miti iliyochipua itakuwa tayari kwa ajili ya kuvunwa tena. Kwa hiyo kwa kupindi chote eneo la asilimia kati ya 10 au 15 ndilo linavunwa huku asilimia zaidi ya 80 ya msitu ikiwa haiguswi na shughuli za mkaa. Kwa mfano, Kijiji cha Mlilingwa kina msitu wenye ukubwa wa hekta 2,532 lakini eneo lililotengwa kwa ajili ya uvunaji wa mkaa ni hekta 477 tu.

Mkaa pia unachomwa kupitia tanuri la kichuguu udongo lililoboreshwa. Katika tanuri hili mkaa huokwa na hivyo miti ambayo inatoa wastani wa gunia 60 za kilo 50, kwa kutumia matanuri ya kawaida mtu anapata gunia kati ya 20 na 30 pekee. Kupitia mradi huu, kijiji hupata fedha na kama mlivyosikia kwenye risala ya kijiji kwamba kupitia leseni za uvunaji wa mkaa na mbao kwa njia endelevu, kijiji kimeingiza Sh 135,111,000 tangu uzalishaji uanze mwishoni mwa mwaka juzi.

Mmesikia pia kwamba pesa hizo ambazo ilikuwa ni ndoto kuzipata miaka ya nyuma, zimetumika kulipia wanakijiji bima ya afya, kusafirisha wahudumu wa afya na zitatumika katika ujenzi wa madarasa na shughuli zingine za maendeleo.

Halikadhalika, katika kuwaongezea wanakijiji kipato ili wasijielekeze kwenye kuvuna msitu, mradi huwasaidia kufanya kilimo hifadhi ambacho huwawezesha kuzalisha kwa wingi zaidi, mradi huwasaidia kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kama kile cha Bosi Kuku kinachojihusisha na ufugaji wa kuku hapa Mlilingwa pamoja na mpango wa kuweka na kukopa kupitia vikundi vya hisa. Mradi pia husaidia kijiji kuwa na utawala bora na kuunda sheria ndogo za kijiji kwa ajili ya ulinzi wa raslimali za misitu.

Swali: Ni jinsi gani mradi unashirikisha serikali na taasisi zingine? Jibu: Mradi huu umekuwepo kwa zaidi ya miaka 15 katika wilaya za Kilosa, Morogoro (vijijini) na Mvomero. Jumla ya vijiji 30 vinashiriki katika mradi huu wa mfano ambao kwa sasa uko awamu ya pili. Kwa kipindi chote tumekuwa tunashirikiana na serikali vizuri. Tunashirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kama mlivyosikia mwakilishi wao akisema, halmashauri za wilaya husika, ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Lengo letu siyo kuchukua majukumu ya serikali bali tunajaribu kuisaidi pale tunapoweza na kuwaonyesha mafanikio ya mradi kama tunavyofanya leo.

Swali: Ni changamoto zipi ambazo mnakutana nazo? Jibu: Changamoto zipo lakini kubwa ni baadhi ya wadau kutouelewa mradi. Tatizo ni kwamba ukizungumza mkaa endelevu juu juu bila kuangalia hasa kilichomo ndani kama nilivyofafanua kwa ufupi hapo juu, utadhani kwamba ni mradi wa uharibifu. Lakini ukija kama hapa Mlilingwa, ukapata nafasi ya kutembelea kijiji, ukaona jinsi wananchi wanavyofanya kazi, ukatembelea maeneo wanayovuna mkaa na kuona manufaa ambayo kijiji kinapata utaelewa kwamba huu ni mradi ambao, siyo tu kwamba unasaidia kuboresha maisha ya wananchi bali pia kuhifadi misitu na kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Swali: Tumeona kwamba mradi huu unasaidia kunusuru misitu mbali ya kusaidia kipato kwa wananchi na kijiji kwa ujumla. Lakini tumesikia mradi unaelekea mwisho. Mnajupangaje ili kuona mradi huu unasambaa zaidi katika mikoa mingine?

Jibu: Ni kweli, mradi huu ambao uko katika awamu ya pili unaelekea mwishoni. Hata hivyo, tuna lengo la kuona tunaendelea kuwepo kwa maana ya kuwa na awamu ya tatu ya mradi. Hivyo tunawaambia wananchi wasiwe na hofu. Hata hivyo, zile mbinu na elimu ambayo tumewapa wakizitekeleza ipasavyo wataendelea kunufaika na raslimali za misitu kama kawaida hata kama hatupo. Tunafanya maonesho kama haya ya leo ili kuisaidia serikali kuona kwamba sisi tukiondoka wanaweza kutumia hii moduli kuisambaza katika maeneo mengine.

Katika semina mbalimbali tulishaeleza kila kitu hata gharama za kuanzisha mradi huu kwenye kijiji kuwa ni kati ya Sh milioni 12 hadi 15 lakini manufaa yake ni makubwa. Sisi tunatamani kwenda maeneo mengine ambayo yana changamoto kubwa ya uzalishaji mkaa kwa njia holela inayoharibu misitu. Swali: Kama mtaanza awamu ya tatu, mmeshajua mahala mtakapoelekea (baada ya Morogoro)? Jibu: Hatua ya kuamua ni wapi tunaweza kwenda baada ya hapa ni zoezi zito kidogo. Huwa kuna vigezo ambavyo tunaangalia kama vile changamoto ya misitu ilivyo katika kijiji husika, uwepo wa miti ya miombo ambayo ndio inafaa kwa mradi kama huu kwa vile huchipua tena na kadhalika.

Swali: Serikali yetu inajitahidi kutafuta mapato kila yalipo kama tulivyoona kwa wachimbaji wadogo wa madini. Inaonekana kwenye mkaa pia kuna pesa ambazo bado zinapotea. Mnafanyaje ili serikali ione hilo?

Jibu: Ni kweli, kwenye mkaa kuna mapato makubwa sana lakini kwa kukosekana mipango kama tulioanzisha kwenye mradi huu wa mkaa endelevu, mapato yanapotea. Hata taarifa moja ya Benki ya Dunia inaonesha kwamba mkaa unaweza kuchangia sehemu kubwa ya pato la serikali. Lakini kumbuka mkaa unaozungumzwa hapa na Benki ya Dunia ni ule ambao umepita katika njia sahihi lakini kwa bahati mbaya mkaa mwingi haupiti njia zinatambulika.

Sisi tunaiambia serikali kwamba wahalalishe uvunaji wa mkaa kwa sababu mahitaji hayo bado yapo nchini, lakini uvunaji ufanyike kwa njia endelevu. Wanaweza kutumia huu mradi wetu wa mfano ambapo wanakijiji watanufaika, kijiji chenyewe, halmashauri hadi serikali kuu. Kwa ngazi ya kijiji, kwa mfano, tumeshuhudia mkaa ukiviwezesha vijiji kujenga zahanati, kununua madawati, ujenzi wa ofisi na kuchimba visima vya maji. Hii inaisaidia pia serikali kupeleka fedha mbazo zingetumika kwa ajili hiyo kufanya kazi zingine. Kwa hiyo ni muhimu mkaa uvunwe kihalali kama tunavyofanya sisi na vibali vitolewe kihalali. Hapo serikali itapata mapato mengi kwenye mkaa ambayo kwa sasa yanapotea.

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi