loader
Picha

UFUTA: ‘Dhahabu’ ya kijani inayoipaisha Kilwa kimapato

ZAO la ufuta limekuwa nguzo muhimu katika mapato na uchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla.

Mbali na ufuta, mazao mengine yanayolimwa katika wilaya hii kwa wingi ni mpunga, korosho, mihogo, mahindi na mboga mboga. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Abdul Mjaka anasema, kwa miaka mitatu mfululizo ufuta umeongoza kwa kuingiza mapato katika halmashauri hiyo. Anasema katika mwaka wa fedha 2017/2018, kati ya Shilingi bilioni tatu zilizotokana na mazao mbalimbali, Shilingi bilioni 1.4 zimetokana na mapato ya mauzo ya ufuta pekee. Halmashauri ilifanikiwa kupata fedha nyingi kutoka katika zao la ufuta ikilinganishwa na mengine kama korosho.

“Ufuta unaongoza kwa mapato katika Halmashauri ya Kilwa kuliko mazao mengine, hivyo kilimo cha ufuta kikiongezeka tuna uhakika wa kukusanya nusu ya fedha ya halmashauri nzima kutoka katika ufuta peke yake,” anasema Mjaka wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya ofisini kwake. Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai anasema pamoja na wilaya yake kuongoza katika kilimo cha ufuta, ina eneo kubwa kabisa ambalo halijaguswa hivyo anawakaribisha wawekezaji katika kilimo hasa ufuta.

Anasema Wilaya ya Kilwa ina eneo lenye ukubwa wa hekta 886, 500 linalofaa kwa kilimo lakini eneo linalotumika kwa kilimo ni asilimia 10 kati ya eneo zima linalofaa kwa kilimo cha ufuta. Hii ina maana kuwa asilimia 90 ya eneo lote linalofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali kikiwemo cha ufuta halitumiki. Kwa maana hiyo ni fursa kubwa kwa wawekezaji wa zao la ufuta kuja kuwekeza katika kilimo cha zao hilo linalotoa mafuta mazuri. “Wilaya ya Kilwa ni ya pili kwa ukubwa katika mkoa wa Lindi. Tuna eneo kubwa ambalo ni rasilimali ya kilimo ambalo hata wananchi wa Kilwa pekee hawawezi kulimaliza.

Tunawakaribisha wawekezaji katika zao la ufuta waje Kilwa wapate faida,” Ngubiagai anatoa wito. Ujenzi wa viwanda vya kukamua mafuta ni fursa nyingine kwa wawekezaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Hii ni kutokna na uwepo wa viwanda vichache ambavyo vinatumia teknolojia duni katika uzalishajiwa mafuta ambayo yanatajwa kuwa ghali zaidi katika soko la dunia.

Anasema hekta chache zinazotumika katika kilimo cha ufuta zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha soko la bidhaa za ufuta kama vile mafuta. Kuna sababu kadhaa zinazosababisha ufuta wa Kilwa kupendwa zaidi duniani. Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, sababu ya kwanza ni kwamba ufuta wa Kilwa unatoa mafuta mengi wakati wa kuukamua tofauti na ufuta mwingine unaolimwa katika mikoa mingine nchini. Sababu hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kupata soko kubwa nchini na nje ya nchi kutokana na ubora wa bidhaa hiyo.

Sababu ya pili, kwa mujibu wa DC Ngubiagai, ni kwamba ufuta wa Kilwa ni mweupe hivyo mafuta yanayozalishwa yana rangi nzuri ambayo inavutia ikilinganishwa na ule unaolimwa maeneo mengine. Tatu, kilimo cha ufuta Kilwa hakitumii mbolea za kemikali kwani wakulima wa Kilwa siku zote wamekuwa mbali na matumizi ya mbolea zenye kemikali kutokana na ardhi yenyewe ina mbolea ya kutosha.

Sababu hizo na nyingine kadha wa kadha ndizo zilizomfanya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi katika mazungumzo na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ofisini kwake kusema: “Mkoa wa Lindi kupitia wilaya ya Kilwa, unazalisha mafuta bora na namba moja duniani yasiyokuwa na lehemu. Kuthibitisha umuhimu wa ufuta katika mapato ya Halmashauri ya Kilwa, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk Elikizemba Halfani anasema, mwaka huu wanakadiria kuingiza mapato yatokanayo na mazao kwa jumla ya Shilingi bilioni 3.9 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Dalili njema za kuvuka malengo ya makusanyo ya halmashauri zimeanza kuonekana kabla ya mwaka kumalizika kwani halmashauri hiyo kongwe imeweza kukusanya Shilingi bilioni 2.2, sawa na asilimia 64.5 ya makusanyo yote.

Kwa upande wake Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Kassim Kambwili anasema maeneo ambayo ni maarufu kwa kilimo cha ufuta katika Wilaya ya Kilwa ni Tarafa za Nanjilinji, Pande pamoja na baadhi ya maeneo ya Kipatimo na Tarafa ya Njinjo. Naye Afisa Umwagiliaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Maulidi Kilekikali anasema Kilwa kuna mabonde mbalimbali ambayo yana rutuba ya kutosha na yanafaa kwa kilimo cha ufuta.

Baadhi ya mabonde ambayo yanafaa kwa uwekezaji wa kilimo cha ufuta ni pamoja na bonde la Mto Mavuji ambalo ukubwa wake umeanzia Matipane hadi Mchakama. Takwimu za halmashauri zinaonesha kuwa eneo hilo lina ukubwa wa hekta 12,000 huku bonde la Mto Matandu likiwa na ukubwa wa hekta zaidi ya 20,000. Kutokana na ukubwa huo, Kilekikali anasema Halmashauri inahitaji wawekezaji katika zao la ufuta ili kuzalisha kwa kiwango kikubwa, jambo analotabiri kuwa litasababisha mapato ya halmashauri kuongezeka sambamba na kipato cha wakulima na wananchi kwa ujumla.

“Ikiwa tutapata mwekezaji ambaye anahitaji eneo kubwa kabisa kwa kilimo na kiwanda cha kukamua ufuta, anakaribishwa kwa kuwa maeneo ambayo hayajaguswa ni makubwa na yenye rutuba ya kutosha,” Ofisa huyo anatoa wito. Katika Mkoa wa Lindi, wilaya inayoongoza kwa kilimo cha ufuta ni Kilwa ikifuatiwa na Liwale, Nachingwea, Ruangwa na ya mwisho ni Lindi.

Kati ya mikoa inayohitaji uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo, Lindi inaongoza kwa uhitaji wa wawekezaji kutokana na kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba ambayo hadi hivi sasa haijaguswa.

Mawasiliano Tanzania Standard Newspapers Ltd, Daily News Building, Plot No. 11/4 Mandela Express Way. Po. Box 9033, Dar es Salaam. Simu: +255 286 4862; 0712 516 169; 0655 332 866. Baruapepe: info@tsn.go.tz advertising@dailynews.co.tz. Website: www.tsn.co.tz; Shamba la ufuta. www.dailynews.co.tz.

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro, Kilwa

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi