loader
Picha

TRA yahimiza ulipaji kodi kwa wakati

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo kote nchini kulipa kodi kwa wakati. Kodi hizo ni za Mapato awamu ya kwanza na Kodi ya Majengo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Akizungumza na walipakodi katika Ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema kodi ya ongezeko la thamani inatakiwa kulipwa ifikapo Machi 20 mwaka huu, kodi ya mapato inatakiwa kulipwa kabla ya Machi 30 2019 wakati mwisho wa kulipa kodi ya majengo ni Juni, 2019.

“Ninachukua fursa hii kuwahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo mliopo hapa na wale watakaosikia taarifa hii kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwahi kulipa kodi hizi kwa wakati, ili kuepuka usumbufu na hatimaye kujikuta mnatozwa faini na riba,” alisema. Amesema kuwa viwango vya kodi ya majengo ni Sh 10,000 kwa nyumba za kawaida, Sh 50,000 kwa kila sakafu ya ghorofa na Sh 20,000 kwa nyumba za ghorafa zilizoko vijijini. “Tunaona serikali imepunguza kiwango cha kodi ya majengo, hivyo hakuna sababu ya watu kuchelewesha na kusubiri dakika za mwisho, tulifanye suala la ulipaji kodi kuwa utamaduni wetu kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Kayombo amewatahadharisha walipakodi kuhusu uwepo wa watu wanaotumia jina la mamlaka hiyo kufanya utapeli kwa kujitambulisha kuwa ni maofisa wa TRA wakidai kwenda kukagua ulipaji wao wa kodi. “TRA ina utaratibu wake wa kuwasiliana na wafanyabiashara na kuwajulisha siku rasmi ambazo maofisa wetu watakwenda kufanya ukaguzi na unafanyika kwa uwazi bila vitisho na si kwa taratibu nyinginezo,” alisema.

Ameongeza kuwa, “kama mtu atapigiwa simu au kama kuna mtu una wasiwasi naye tafadhali toa taarifa kwa ofisi zetu zilizopo karibu nawe au toa taarifa Kituo cha Huduma kwa Wateja namba 0800 780 078 au 0800 750 075 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 1:00 usiku na utupe namba ya mhusika ili tuweze kufuatilia. “Pia kuna namba ya WhatsApp ambayo unaweza kutoa taarifa au kuuliza chochote kupitia namba 0744 233 333 ambayo ni maalumu kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi na kuwawezesha kulipa kodi kwa wakati,” alisema.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi