loader
Picha

Kampuni yasitisha matumizi ya Boeing 737 Max 8

KAMPUNI ya Boeing imesitisha matumizi ya ndege zote aina ya Boeing 737 Max 8 baada ya wachunguzi kubaini ushahidi mpya katika eneo ambalo ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia ilianguka.

Aidha, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza juzi amri ya dharura ya kusitisha usafiri wa ndege zote muundo wa Boeing 737 Max 8 na Max 9 kwenye anga ya Marekani. Hatua hiyo ya kusitisha usafiri wa ndege zote 371 zinazohudumu, imekuja wakati nchi mbalimbali zikiwa zimetangaza kusimamisha huduma ya ndege hizo baada ya ajali ya hivi karibuni iliyoua watu 157 baada ya kuanguka ikitoka Addis Ababa, Ethiopia kwenda Nairobi, Kenya.

Katika taarifa yake kupitia tovuti ya kampuni, Rais wa Boeing, Dennis Muilenburg alisema wanaunga mkono hatua ya hadhari iliyochukuliwa na nchi mbalimbali. Alisema wanafanya kila wawezalo kwa kushirikiana na wachunguzi kubaini sababu ya ajali hizo mbili ili wahakikishe usalama ajali zisitokee tena. Ajali hiyo imetokea miezi mitano baada ya nyingine iliyotokea Indonesia mwaka jana na kusababisha vifo vya watu 189.

Awali, shirika linalosimamia Usafiri wa Anga (FAA) la Marekani lilisisitiza kuwa ndege ya Boeing 737 Max 8 ni salama. Lakini juzi lilikaririwa likisema ushahidi mpya pamoja na data mpya za satelaiti zimechangia uamuzi huo wa kupiga marufuku kwa muda usafiri wa ndege hizo. Kaimu Msimamizi wa FAA, Dan Elwell alisema juzi kwamba walichoshuhudia katika ajali ya Ethiopia kinashabihiana na ya Indonesia.

“Ushahidi tuliopata katika eneo umefanya tuone kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba hata njia ya ndege ilikaribiana na ile ya Lion Air (Indonesia),” alisema. Kwa upande wa Rais Trump, amesitisha usafiri wa ndege hizo za Boeing 737 Max 8 na Max 9 kwenye anga ya Marekani hadi hapo uchunguzi utakapokamilika na kubaini iwapo hitilafu ya kimitambo ilisababisha ajali mbili (Indonesia na Ethiopia).

Kwa mujibu wa shirika la habari la Voice of America (VOA), muda mfupi baada ya Trump kutangaza hatua hiyo, maofisa wakuu wa kampuni ya Boeing walitoa taarifa kupitia mtandao wa Twitter na kusema kampuni inaunga mkono kauli ya rais. Ujumbe ulisema, “Ni heri kuwa salama kuliko kujuta baadaye.”

Uamuzi huu wa Marekani umefanya nchi hii iwe sehemu ya takribani nchi 30 zilizokwishatangaza kusitisha safari za ndege husika. Uchunguzi unaendelea kufanyika kwenye mfumo wa kompyuta wa ndege hizo kwa kuwa unashukiwa kusabisha ajali hizo. Hadi wiki iliyopita (Machi 10 ambayo ndege ya Ethiopia ilianguka), Boeing ilikuwa imeuza ndege 400 ulimwenguni kote.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: WASHINGTON, Marekani

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi