loader
Picha

Polisi acheni kubambikizia watu kesi

BAADHI ya mambo ambayo Rais John Magufuli amekuwa akihimiza kila siku ni kutenda haki, utawala wa sheria, kudumisha demokrasia na kupiga vita rushwa.

Katika utendaji wa haki, Rais amekuwa akihimiza vyombo vya dola kama vile Jeshi la Polisi, kutenda haki kwa wananchi.

Lakini, jambo la kushangaza ni kuwa bado wapo baadhi ya polisi nchini, ambao hawajaacha tabia hiyo ya kubambikizia watu kesi.

Hali hiyo imethibitishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alipozungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa DPP, mkazi mmoja wa Tabora, Musa Adam Sadiki alibambikiziwa kesi ya mauaji namba 8 ya mwaka 2018 katika Mahakama ya Tabora Mjini.

Kwamba baada ya kumkamata, polisi walimnyang’anya Sh 788,000, simu ya mkononi na mali zake zingine. Aliwekwa kwenye Kituo cha Polisi Tabora Mjini ambako alibambikiziwa kesi ya kuvunja na kuiba.

Alikaa kituoni hapo kwa wiki moja kisha alipelekwa mahakamani ambako alisomewa mashtaka ya mauaji, akidaiwa kuwa Mei 6, mwaka jana akiwa katika Barabara ya Kazima mjini Tabora, alimuua Jackson Thomas.

DPP anasema alifuatilia na kubaini ukweli wa tukio hilo na Machi 8, mwaka huu, aliwafutia mashtaka Sadiki na mtu mwingine, Edward Matiku na Mahakama ya Tabora Mjini ikawaachia huru. Matiku alikuwa ameunganishwa kwenye kesi hiyo ya mauaji.

Anasema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imebaini kuwa malalamiko ya Sadiki ni ya kweli na chanzo chake ni Rais John Magufuli, alisoma Barua ya Wasomaji katika gazeti la Majira la Machi 6, mwaka huu.

Barua hiyo ilikuwa ya wazi kwa Rais, ikiwalalamikia Polisi hao wa Tabora. Baada ya kusoma barua hiyo, Rais aliagiza Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, ifuatilie kwa haraka malalamiko ya Sadiki ili kujua ukweli na baada ya kufuatilia, wamebaini kuwa malalamiko hayo ni ya kweli.

Kwanza, tunampongeza Sadiki kwa ujasiri mkubwa, aliouonesha wa kuweka wazi malalamiko hayo kwenye vyombo vya habari, hatua iliyowezesha Rais na Watanzania kufahamu maovu yanayoendelea kufanywa na baadhi ya polisi wa Tabora.

Tunahimiza Watanzania wengine kuiga ujasiri wa Sadiki kwa kufichua maovu kwenye maeneo yao. Tunatambua kuwa tukio hilo la Tabora, ni sehemu ndogo tu ya tatizo kubwa lililopo la watu kubambikiziwa kesi na kufungwa kimakosa.

Hivyo, tunaomba polisi wote waliohusika na tukio hilo la Tabora, na wengine wanaokiuka maadili ya Polisi, wachukuliwe hatua kali ili kukomesha tabia hiyo, inayoichafua serikali kwa wananchi wake na dunia nzima.

Tunasisitiza kuwa Polisi acheni mchezo wa kubambikizia watu kesi.

KITUO cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinajitahidi sana kuboresha shughuli za ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi