loader
Picha

Serikali ipongezwe kusaidia nchi tatu

JUZI serikali ya Tanzania imetoa msaada wa dawa, vifaa tiba na chakula kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika na mafuriko katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.

Mafuriko hayo yaliyosababishwa na kimbunga, yalitokea hivi karibuni na kusababisha vifo na maafa makubwa katika nchi hizo.

Kwa upande wa Msumbiji, Rais Filipe Nyusi alitembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo, ambako alielezwa kuwa watu waliokufa ni zaidi 200 na walioathiriwa ni 600,000.

Kwamba mjini Beira watu 100,000 wanahitaji msaada wa dharura, ambapo nyumba nyingi zimeharibiwa na hakuna umeme wala mawasiliano ya simu. Baadhi ya watu wameangukiwa na miti na majengo.

Wengine walikwea kwenye miti ili kujiokoa. Kwa Zimbabwe, watu 98 wamekufa na wengine 217 wamepotea na hawajulikani waliko, kutokana na mafuriko hayo. Wanafunzi wawili wa shule moja ya bweni, wamekufa baada ya bweni lao kuangukiwa na mawe makubwa kutoka milimani.

Kutokana na janga hilo, Rais Emmerson Mnangagwa amekatisha ziara yake katika Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) na kurejea nyumbani. Kwa upande wa Malawi, kimbunga hicho kimesababisha vifo vya watu 122.

Hivyo, tunapongeza mno hatua iliyochukuliwa na serikali ya Tanzania juzi, kutoa msaada wa dawa, vifaa tiba na chakula kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika na mafuriko katika nchi hizo za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi. Msaada huo umekabidhiwa kwa mabalozi wa nchi hizo kwenye Uwanja wa Jeshi la Anga (Air Wing) jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, Tanzania imeguswa na maafa yaliyotokea katika nchi hizo jirani.

Kwamba kwa taarifa alizo nazo, mafuriko hayo yamesababisha vifo 221 nchini Msumbiji, ambapo vifo 88 vimetokea katika mji wa Beira.

Anasema Tanzania ina wajibu mkubwa wa kuzisaidia nchi hizo, kwa kuwa tupo nao katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), lakini pia tunapaswa kujua kwamba kifo cha jirani ni kifo chetu, shida ya jirani ni shida yetu na maafa ya jirani ni maafa yetu. Kwamba malori saba yameshaanza kupakia dawa na malori mawili kupakia chakula kupeleka Malawi.

Msaada kwa Zimbabwe na Msumbiji utapelekwa kwa ndege ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kwamba msaada huo pia unajumuisha tani 24 za dawa, ambapo kila nchi itapata tani nane.

Dawa hizo zinajumuisha aina tano ya dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria, dawa za kutibu magonjwa ya matumbo ikiwemo kuhara, dawa za kuzuia maumivu, dripu na vifaa tiba kama vile mashuka, mablanketi na vyandarua.

Pia, Serikali ya Tanzania imetoa msaada wa chakula tani 14 za mchele kwa waathirika wa mafuriko katika nchi za Msumbiji na Zimbabwe, ambapo kila nchi itapata tani saba, wakati tani 200 za mahindi zitapelekwa Malawi kwa malori kutokea mkoani Mbeya.

Kwa ujumla, tunaipongeza sana serikali kwa kutoa msaada huo mkubwa kwa nchi hizo tatu.

KITUO cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinajitahidi sana kuboresha shughuli za ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi