loader
Picha

Hongera Tanzania, Kenya, Burundi, Uganda kufuzu fainali Afcon

WATANZANIA juzi walikesha wakishangilia baada ya timu yao ya soka ya taifa, Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zitakazofanyika Misri.

Ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya jirani zao, Uganda, The Cranes, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umeifanya Taifa Stars iweke historia ya kutinga fainali baada ya miaka 39 tangu iliposhiriki fainali hizo Nigeria, 1980.

Ni kutokana na ushindi huo unaoifanya Taifa Stars na timu za Taifa za Burundi, Uganda na Kenya, wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), tuungane na Rais John Magufuli na wananchi wote kuipongeza.

Tunaipongeza Taifa Stars kwa sababu imeweka historia mpya Afcon baada ya ile mwaka 1980, wakati ikiongozwa na nahodha Leodgar Tenga na kuwatoa kimasomaso wananchi na Rais JPM.

Tunaungana na Rais Magufuli kutaka wachezaji hao kuongeza bidii na maarifa kwa maslahi ya Taifa wafanye vizuri zaidi katika michuano ya fainali kwa kufika robo fainali, nusu au fainali.

Kama alivyosema Rais Magufuli, tumefurahi pia na tunaungana na wananchi wote kupongeza wachezaji wote wa Taifa Stars na viongozi wao na Serikali kuwapa zawadi ya viwanja Dodoma.

Ni matumaini yetu zawadi hiyo itakuwa chachu ya Taifa Stars kufanya vizuri Misri kuhamasisha ndugu zao, timu ya vijana kufanya vizuri fainali za soka vijana Afrika 2019 jijini Dar es Salaam Aprili, ikibidi ifuzu Kombe la Dunia Vijana.

Zaidi tumefurahishwa na ushindi huo wa Taifa Stars ulivyowaunganisha Watanzania wa dini, makabila, klabu tofauti kuwa kitu kimoja kwa mwavuli wa umoja wa kitaifa na pia uzalendo.

Ni matumaini yetu, wananchi wataendeleza umoja huu kwa maeneo mengine ya maendeleo kama alivyoomba Rais Magufuli kama nyenzo ya kupambana na hila za mabeberu kutoka nje.

Rai yetu nchi nyingine za Afrika Mashariki, Kenya, Burundi na Uganda zilizofuzu fainali za Afcon Misri pia ziige mshikamano uliooneshwa na Watanzania kushangilia timu kwa uzalendo.

Tunaamini, Kenya, Uganda na Burundi nazo zitakuwa zimefurahia kupata nafasi hiyo ndio maana tunaungana na Watanzania kuzipongeza na kuzitaka ziwakilishe vyema EAC huko Misri.

Kwetu ushindi wa timu za mataifa hayo manne tunauchukulia kama chachu ya kuendeleza zaidi umoja wao katika jumuiya na kuimarisha sauti zao katika mtangamano wa kikanda na kidunia.

Ni matarajio yetu zitaiwakilisha vyema EAC katika fainali Misri na kuimarisha uhusiano, udugu na ujirani wao kwa maslahi ya jumuiya hiyo 2019. Kila la heri Taifa Stars, The Cranes, Intamba Murugamba, Harambee Stars.

HIVI karibuni wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni, Waziri ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi