loader
Picha

'Msiatamie fursa, zitumieni mtajirike'

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka wawekezaji, wafanyabiashara, taasisi za fedha na wajasiriamali kuwa na uthubutu na kuchangamkia fursa, zinazoibuliwa Lindi ili kuujenga mkoa huo, ambao ni kati ya mikoa yenye utajiri uliojifi cha.

Pia, amewataka Watanzania na wawekezaji, kuchangamkia fursa zinazoibuliwa katika mikoa mbalimbali nchini na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ili kuijenga Tanzania ya viwanda.

Makamu wa Rais amesema hayo mjini Lindi jana katika Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji, lililoandaliwa na TSN kwa kushirikiana na Mkoa wa Lindi.

Hotuba ya Makamu wa Rais ilisomwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Amesema kampuni hiyo ya magazeti kwa muda mrefu, imekuwa ikitembelea mikoa na kuweka kambi kupitia timu yake ya waandishi wa habari, ambayo huingia hadi vijijini na kuibua fursa zilizopo katika mkoa huo na kuzitangaza kupitia vyombo vyake vya habari.

TSN ni wachapishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo, SpotiLeo, Daily News na HabariLeo Digitali.

“Jukwaa hili ni njia ya busara iliyochaguliwa na TSN kushawishi majitu ya miraba minne hapa Tanzania ambayo bado yameatamia fursa kubwa. Huyaamsha na kuyaonesha kuwa yameatamia utajiri mkubwa na kuuonesha utajiri huo kupitia vyombo vyake vya habari kwa lengo la kuvutia wawekezaji,” ameeleza.

Alisema pamoja na kuamshwa kwa mikoa hiyo, lakini pia majukwaa hayo huvutia taasisi mbalimbali za serikali ambazo hutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, wawekezaji na hata wajasiriamali katika maeneo mbalimbali nchini.

“Kule Arusha kwenye moja ya majukwaa haya, wafanyabiashara wengi waliogopa kujitokeza kuzungumza kwa kuhofia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini baada ya mwakilishi wa mamlaka hiyo kuzungumza, hali ilibadilika na wengi walifurahi kupata elimu ambayo awali walikuwa hawana na walikuwa wakihofia bure tu,” alisema.

Alisema wazo la kuendesha majukwaa hayo ni ubunifu tu wa TSN ili kuleta ari mpya ya kuibua fursa za kiuchumi kwenye mikoa na kuhamasisha umma, kampuni, taasisi za kibiashara kuchangamkia fursa zinazoibuliwa.

Akizungumzia Jukwaa la Lindi, alisema Lindi si tu ni jitu la miraba minne lililolala, bali pia limeatamia utajiri mkubwa na hakuna anayethubutu kuliamsha kwa hofu ya kudhurika au likanuna na kusifanyike kitu chochote.

“Lakini TSN imekuja na njia ya staha imeishawishi Lindi na kuelezea faida za kuibuliwa kwa fursa zake, na sasa inaamka polepole,” alisisitiza.

Alisema mpaka sasa mkoa huo utajiri wake umeshaibuliwa na kutangazwa na kilichobaki ni wawekezaji, taasisi za fedha, wafanyabiashara na wajasiriamali, kugeuza macho yao Lindi ambako ni sawa na mgodi ‘uliotema’.

“Nimethibitisha kuwa Lindi ni hazina ya Taifa kwa kuwa na fursa nyingi, kuna kilimo cha korosho, ufuta, madini grafaiti, gypsum, utalii wenye fukwe zenye viwango vya kimataifa, utalii wa mambo ya kale, utalii wa urithi wa harakati za ukombozi wa Afrika, wanyama na uwindaji, misitu na mazao yake,” alisema.

Alisema uwekezaji wowote ili ufanikiwe, lazima uwe na uthubutu na alitoa mfano namna alivyofanikisha ujenzi wa uwanja wa taifa kupitia mfadhili mpya na kumuondoa mfadhili wa awali, ambaye alikuwa hachangii chochote.

Pamoja na hayo, aliwataka wawekezaji na wenye viwanda, kuhakikisha wanatumia malighafi zinazozalishwa nchini, jambo litakalowapatia faida, lakini pia kuinua wazalishaji wa ndani.

“Lindi mmeshaonesha njia, lakini kama leo hii mmeweza kushinda mikoa sugu kama Dar es Salaam ambako wengi wanakimbilia huko, lakini mkawa wa kwanza katika kuanzisha viwanda vidogo, ni wazi kuwa mtapiga hatua kubwa,” amesema.

Dk Mwakyembe alisema Makamu wa Rais alipenda sana kuhudhuria jukwaa hilo, lakini imeshindikana kutokana na kuibuka kwa shughuli nyingine za kitaifa zilizohitaji uwepo wake.

“Ametutakia mjadala mzuri na ametaka apewe mrejesho wa mwitikio wa wana-Lindi katika jukwaa hili,” alisema.

Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN, Tuma Abdallah alielezea lengo kuu la TSN kuanzisha majukwaa hayo kuwa ni kuhakikisha inaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika kuifikia serikali ya viwanda kwa kuibua fursa zilizopo kwenye mikoa hiyo na kuzitangaza.

“Tuliamua kwenda mikoani baada ya kuona kuna fursa nyingi ambayo hata wananchi wa mikoa husika wenyewe hawazifahamu. Mpaka sasa tumeshafanya majukwaa haya kwenye mikoa nane na huu wa Lindi ni wa tisa,” alisisitiza Tuma.

Mikoa iliyokwishafanya majukwaa hayo ya kuibua fursa za biashara kupitia TSN ni Simiyu, Geita, Shinyanga, Mwanza, Zanzibar, Arusha, Tanga na Tabora. Alisema mkoani Lindi, kampuni hiyo ilituma waandishi wake wiki tatu zilizopita, ambao waliziibua fursa za Lindi na wiki hizo mfululizo wamekuwa wakizitangaza.

“Leo (jana) hii gazeti letu la HabariLeo lina kurasa 48, kati hizo kurasa 35 zina habari za Mkoa wa Lindi pekee,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Mkwizu aliwataka washiriki wote wa jukwaa hilo, kuhakikisha wanaondoka na funzo ambalo watalitumia kuwasaidia katika biashara zao ili majukwaa hayo yawe na tija.

Aliwashukuru wadhamini wa jukwaa hilo na uongozi mzima wa mkoa wa Lindi kwa kufanikisha jukwaa hilo kufanyika, ambalo pia linamalizika rasmi leo.

WAKUU wa Mikoa ya Tabora na Geita, wamesema Jukwaa la ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Lindi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi