loader
Picha

Bakhresa kuwasaidia NSSF viwanda vya sukari

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Said Salim Bakhresa ameahidi kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa ajili ya kupeana maarifa hasa kwenye maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya sukari.

Bakhresa alisema hayo jana ofisini kwake Dar es Salaam, alipokutana na uongozi wa NSSF chini ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, William Erio.

Alisema yupo tayari muda wowote kukutana na kuzungumza na uongozi wa NSSF kuhusu uwekezaji wa viwanda vya sukari ili kubadilishana uzoefu na kuangalia namna bora ya uzalishaji wenye tija kwa jamii na taifa.

Erio kwa kushirikiana na timu yake, walifanya ziara katika shamba la Bagamoyo Sugar lililopo Makurunge Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kwa ajili ya kujifunza.

Shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 10,000 sawa na ekari 25,000, linamilikiwa na Kampuni za S.S Bakhresa, ambalo litajengwa kiwanda cha sukari.

Mwaka 2016 Rais John Magufuli alimpa mfanyabiashara huyo shamba hilo kwa ajili ya kujenga kiwanda kikubwa cha sukari ili kupunguza uhaba wa sukari nchini.

Bakhresa alimshukuru Erio na timu yake kwa kutembelea shamba hilo kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu wa uendeshaji na kisha kwenda ofisini kwake na kuzungumza naye.

“Nakushukuru wewe na timu yako kwa kuja, maana tumepeana uzoefu wa kutosha na tumepeana maarifa mengi na kuzungumza mengi,” amesema Bakhresa.

Aliahidi kuendelea kukutana na uongozi wa shirika hilo kwa ajili ya kuzungumza mambo mbalimbali, ambapo alisisitiza kwamba yupo tayari muda wowote kukutana nao.

Erio amemshukuru Bakhresa kwa namna walivyopatiwa maelezo mazuri walipotembelea shamba hilo kwa ajili ya kujifunza.

“Tunakushukuru kwa nasaha zako, uzalendo wako na kukubali kutusikiliza na kubadilishana mawazo katika maeneo ambayo yatafanikisha uwekezaji ambao utafanikiwa na kuleta tija kwa Taifa,” alisema Erio.

Erio alimshukuru mfanyabiashara huyo kwa uwekezaji wake mkubwa katika viwanda vyake kwenye maeneo 17 tofauti, ambapo NSSF wanapata faida kwani wafanyakazi wa kampuni hizo ni wanachama wa shirika hilo.

Alifafanua kwamba lengo la ziara hiyo ni kujifunza uzalishaji wa miwa na namna ya uendeshaji wa kiwanda cha sukari, ambako NSSF kupitia kampuni yake ya Mkulazi Holding kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wameanzisha shamba la miwa katika Gereza la Mbigiri mkoani Morogoro.

Erio amesema wamepata fursa ya kutembelea baadhi ya viwanda vya sukari kwa ajili ya kujifunza, lakini tofauti ni kwamba Bagamoyo Sugar wanaanza moja kama wao. Alisema viwanda vingine vilikuta miundombinu ilishajengwa na serikali, lakini baada ya ubinafsishaji walivinunua na kuviimarisha zaidi.

“Sasa tulidhani uzoefu wa Bagamoyo Sugar na wa kwetu unafanana hii ni sehemu sahihi ya kujifunza na kuona wenzetu wanafanyaje na sisi tufanyaje, tumejifunza mengi ikiwemo tafiti zao walizaofanya,” amesema Erio.

WAKUU wa Mikoa ya Tabora na Geita, wamesema Jukwaa la ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi