loader
Picha

Nchi zingine ziige Tanzania, Rwanda

Nchi zingine ziige Tanzania, Rwanda HIVI karibuni iliripotiwa kuwa uhalifu katika mpaka wa nchi za Tanzania na Rwanda, umepungua kwa asilimia 26.3 ukilinganisha na mwaka jana.

Pia, iliripotiwa kuwa ng’ombe 26 waliokuwa wameibwa Tanzania, wamekamatwa nchini Rwanda na kurejeshwa Tanzania kwa wamiliki halali.

Mambo yote hayo yalibainika katika mkutano wa pamoja kati ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Rwanda (IGP), Dan Munyuza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro. Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni katika mpaka wa Rusumo upande wa Tanzania wilayani Ngara mkoani Kagera.

Tunapongeza mkutano huo wa Sirro na Munyuza na mafanikio hayo yaliyopatikana, kwa sababu uhalifu ni kero kubwa inayosumbua watu wa mpakani katika mataifa mbalimbali, ikiwemo nchi hizo.

Uhalifu huo umekuwa ukisababisha wakazi wa maeneo ya mpakani kuishi kwa hofu na pia umekuwa ukizorotesha shughuli za uzalishaji mali.

Tumevutiwa na kauli iliyotolewa na IGP Sirro kuwa polisi ndiyo uso wa nchi, hivyo wanatakiwa kuhakikisha wananchi wanaishi kwa furaha.

Anasema pia wananchi hawataki maneno maneno, bali vitendo. Kwa mujibu wa Sirro, uhalifu katika maeneo ya mipakani, hauwezi kukomeshwa na nchi moja tu, bali lazima polisi wa nchi kadhaa, kushirikiana kufanya operesheni za pamoja.

Kwamba mipakani kuna matukio mengi ya kiusalama na uhalifu wa aina nyingi, mfano wizi wa kutumia silaha, usafirishaji wa dawa za kulevya, ugaidi, usalama barabarani na usafirishaji binadamu. Kwamba ushirikiano wa polisi, utawezesha wahalifu wengi kukamatwa.

Tunampongeza IGP Munyuza aliyesema uhusiano wa Rwanda na Tanzania, hautokani na jiografia pekee, bali unatokana na watu wake, ambao wamekuwa wakishirikiana kwa miaka mingi na wanafanana katika masuala mengi.

Munyuza anataja faida za mkutano wake na Sirro kuwa ni kujadili kwa pamoja changamoto za kisasa za usalama, kubadilishana uzoefu wa kufanya kazi, kuendesha mafunzo, kuendesha operesheni za pamoja, kubadilishana wafungwa na kubadilishana taarifa za wahalifu na wataalam.

Faida nyingine ya mkutano huo ni kuongeza ushirikiano wa Rwanda na Tanzania katika masuala ya usalama katika kukabiliana na uhalifu mpakani kwa manufaa ya wananchi.

Ni wazi kuwa ushirikiano wa polisi, umewezesha kutatua kero siyo za miaka nyingi tu, bali hata zile za haraka kwa nchi hizi jirani.

Kwa mfano, hivi karibuni Jeshi la Polisi la Rwanda lilichukua hatua za haraka na kufanikiwa kuzima moto, uliozuka eneo la Rusumo upande wa Tanzania, wakati magari makubwa ya mafuta yalipogongana.

Hivyo, tunasisitiza kuwa mikutano kama hiyo ya wakuu wa polisi, ifanyike mara kwa mara ili kudumisha usalama na kuleta maendeleo endelevu.

MKUTANO wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi