loader
Picha

Faida za kuzuru vivutio vya ndani

JE, mara yako ya mwisho kusafi ri sehemu ngeni ilikuwa lini? Uliposafi ri, huenda ulihisi kwamba ulihitaji kupumzika na kusahau taabu za kila siku? Je, umewahi kwenda likizo katika maeneo yoyote ya vivutio? Fikiria karne moja hivi iliyopita, watu wengi duniani hawakuwa wakipata nafasi ya kusafiri au kwenda mapumziko kama ilivyo sasa.

walikaa karibu na kwao maisha yao yote bila kutembelea maeneo ya mbali. Kusafiri nchi za mbali kwa namna yoyote ile ikiwemo kupumzisha akili au kujielimisha lilikuwa jambo gumu na ni watu wachache tu, hasa matajiri au wafanyabiashara waliopenda kusafiri ndio waliweza kufanya hivyo. Lakini siku hizi mambo yamerahisishwa zaidi, mamia kwa maelfu ya watu wanasafiri kokote wanakotaka katika nchi yao au hata nchi nyingine, hasa kwa safari za kitalii.

Ripoti moja ya Shirika la Utalii Ulimwenguni inasema hivi: ‘Utalii wa huingiza fedha nyingi za kigeni ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi nyingi.” Inasema: “Mwaka 1996, utalii wa kimataifa ulichuma fedha za kigeni zenye thamani ya Dola bilioni 423 za Marekani. Mapato hayo yalikuwa zaidi ya yale yaliyochumwa kwa kuuza mafuta, magari, vyombo vya mawasiliano, nguo, na kadhalika, katika nchi nyingine.”

Ripoti inaenda mbali na kusema:: “Utalii ndiyo biashara inayostawi zaidi ulimwenguni,” na ilitokeza ‘asilimia 10 ya jumla ya pato la nchi zote ulimwenguni.’ Nadhani kila mmoja atakubaliana nami kuwa kutembelea maeneo ya vivutio kuna faida kubwa, japokuwa suala la kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio halijazoeleka sana kwa Watanzania na Waafrika kama ilivyo kwa Wazungu.

Kusafiri siyo lazima kwenda nchi nyingine, bali hata safari za ndani ya nchi au ndani ya eneo lako unaloishi zina maana kubwa, hasa kama zitafanywa kwa lengo la kujifunza. Unapofunga safari ya kutembelea vivutio na maajabu ni njia nzuri ya kuona fursa zilizoko kwenye eneo fulani unazoweza kuzifanyia kazi na ukajipatia kipato au ukaongeza kipato chako. Utalii una faida kubwa na hufaidisha pande zote. Wewe kama mtalii, unapotembelea vivutio au maajabu nchini kwako au hata katika nchi ya kigeni, utaburudika sana na kuelimika.

Tanzania tunayo maeneo muhimu kwa utalii kama: hifadhi za taifa, mapori ya akiba, fukwe za bahari, maeneo ya kihistoria, milima, maziwa n.k. Unaposafiri unajifunza mambo mbalimbali ambayo isingekuwa rahisi kujifunza ukiwa nyumbani. Utajifunza jiografia, utamaduni au hata mtindo wa maisha wa watu wa eneo unalotembelea.

Si ushamba kutembelea maeneo ya vivutio katika nchi yako na kujifunza huko, kwani inasemwa kuwa kutembea umbali wa maili moja ni bora kuliko kukaa sehemu moja bila jambo muhimu hivyo, kutembla maeneo mbalimbali ni shule nzuri ya kuongeza maarifa. Ifahamike wazi zaidi kuwa, nchi zinazowahudumia watalii hujipatia fedha nyingi za kigeni, kwa kuwa nchi yoyote huhitaji fedha za kigeni ili kulipia huduma na bidhaa zinazotoka katika nchi nyingine. Kwa hiyo, unaposafiri unaweza kuboresha maisha ya watu wengine wa eneo ulilotembelea kwa njia moja au nyingine.

Fikiria vyombo vya usafiri unavyotumia safarini, hoteli utakazolala, viingilio utakavyolipa na kadhalika. Hivi vyote vinawapa kipato watu wengine na kuboresha maisha yao, hivyo, safari yako haikunufaishi wewe peke yako, bali hata watu wengine wanaohusika au kuhusishwa kwenye safari yako. Unaposafiri pia unapata marafiki mbalimbali watanaotokana na watu uliokutana nao safarini. Wapo baadhi ya watu waliowahi kupata wenza wa maisha kutokana na kusafiri; hivyo faida hii ya kusafiri haiwezi kuachwa nyuma.

Karibu kundi kubwa la watu, pengine nawe ni mmoja wao, wamewahi kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa malengo tofauti tofauti likiwamo la kuburudika, hata hivyo, moja ya safari nzuri katika safari hizo ni yenye kusudi la utalii. Utalii ni jambo linalopaswa kupendwa na kila mtu anayethamini uumbaji wa Mungu, kwa kuwa ni Mungu aliyewawekea wanadamu mazingira ya kuvutia na kustaajabisha ili tuweze kujifunza kupitia uumbaji wake.

Tanzania ni moja ya nchi zilizobarikiwa kuwa na maeneo ya kipekee katika nchi nyingi zenye utajiri wa maeneo ya vivutio, wanyamapori, milima, maziwa na hata historia katika makumbusho. Vivutio hivi ni utajiri mkubwa wa kujivunia na kila Mtanzania anapaswa kuiona thamani ya kuujali kwa kutembelea maeneo haya kujifunza na pia kuburudika.

Haipendezi kuona watu kutoka nchi za ughaibuni wakija kutalii maeneo haya ambayo sisi tumekuwa tukiyatazama tu pasipo kupata muda wa kwenda kujifunza huko. Yapo maneno ya asili na yenye kuvutia sana ambayo kama hujawahi kutembelea ni vyema ukajitahidi kutafuta nafasi ili kutembelea japo eneo moja au mawili, kwani utajifunza mengi s ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa kufikiri. Maeneo hayo ni pamoja na Msitu wa Nyumbanitu wenye kuku wa ajabu mkoani Njombe, Bwawa la Mto Nyange lenye viboko wanaocheka na mapango ya Kipatimo wilayani Kilwa, Hifadhi ya Gombe yenye sokwe wanaoishi kama binadamu mkoani Kigoma, eneo la Snake Park huko Monduli- Arusha, na Bonde la Ngorongoro ambalo ndiyo kitovu cha binadamu.

Maeneo mengine ni Maporomoko ya Maji ya Mto Ruaha, Mapango ya Amboni mkoani Tanga, eneo la Kondoa Irangi mkoani Dodoma, shimo la ajabu lijulikanalo kama Shimo la Mungu wilayani Newala, mchanga unaohama bila upepo huko Ngorongoro. Pia tunayo milima kama Kilimanjaro, Milima ya Usambara, Uluguru, Udzungwa, Oldonyo Lengai n.k. mbuga za wanyama kama Mikumi, Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Selous, Katavi, na maeneo yenye historia kama Kilwa Kisiwani, Bagamoyo, Zanzibar na kadhalika.

Utajiri huu wa uwepo wa vivutio hivi na vingine vingi licha ya kuiingizia nchi mapato makubwa, pia ni maeneo yenye fursa kubwa na yanayofaa kutunzwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vinavyokuja. Haya yanapaswa kutunzwa na kutumiwa ipasavyo kwa kutembelewa ili neema iliyo ndani ya urithi huu, iwanufaishe watanzania hasa kwa kupanua uelewa wao wa mambo na kuburudika. Haya, yanapaswa kutunzwa kwa kutunza na kutoharibu mazingira na ma;liasili zake. Hivyo, kusafiri na kwenda kujionea vivutio mbalimbali ndani ya nchi ni burudani ya aina yake, hasa kama unasafiri kwenda kwenye eneo sahihi.

Unaposafiri hutaacha kujifunza, kupata burudani bora na ya kipekee na faida nyingine lukuki. Uwapo safarini unaweza kuona vitu vya kuvutia kama vile mazingira ya asili (mito, milima, mabonde, n.k.), wanyama pamoja na sanaa za eneo husika kama vile ngoma, maigizo, mavazi ya kitamaduni na kadhalika. Ni ukweli usiopingika kuwa, Wazungu wanafahamu vyema umuhimu wa safari za kitalii, ndiyo maana wako tayari kulipa gharama kubwa ili watimize lengo hilo. Kimsingi, kutembelea vivutio humfanya mtu kuburudika na kufurahi, na tunapofurahi tutakuwa tumejiongezea siku za kuishi huku tukichochea utunzaji na ukuaji wa uchumi wa nchi. 0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi