loader
Picha

Athari za kuchimba visima kiholela

NI ukweli usiopingika kwa kila mtu kwamba maji ni uhai na bila maji hakuna maisha kwa sababu shughuli za binadamu zinahusisha maji maana usipoyanywa, utayaoga, usipoyaoga utayapikia, usipopikia utayafulia.

Kwa msingi na umuhimu huu wa maji, ipo haja ya kipeke kila mtu na mamlaka zote kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa.

Licha ya umuhimu huo wa kipekee wa maji duniani na hata hapa nchini, bado baadhi ya watu wanafanya uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji nchini na hivyo, kusababisha uhaba wa maji. Hali hii ipo katika maeneo mbalimbali nchini likiwamo Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.

Uhaba huu wa maji katika maeneo mbalimbali umesababisha kushamiri kwa uchimbaji holela wa visima unaofanywa na watu binafsi, kampuni na taasisi mbalimbali usiozingatia na kukidhi matakawa ya kisheria.

Uchimbaji huo umesababisha madhara mengi ikiwa ni pamoja na kuchukua maji mengi zaidi ya uwezo wa miamba iliyopo na hivyo, kusababisha kushuka kwa kina cha maji baridi chini ya ardhi.

Hali hiyo inaweza kusababisha maji ya chumvi kutoka baharini kubadilisha mwelekeo na kuingia nchi kavu kisha kuleta mwingiliano wa maji baridi na chumvi. Kwa mujibu wa wataalamu, maji ya chumvi si rafiki kwa matumizi ya nyumbani kama vile kunywa, kupikia, kufulia na kuoga.

Wataalamu wanasema maji haya huchangia kuharibu miundombinu kwani husababisha kutu kwenye miundombinu.

Aidha, husababisha pia kuchukuliwa maji mengi na kuacha miamba inayohifadhi maji (aquifers) bila maji, jambo linalosababisha ardhi kutitia na kuleta madhara kwenye miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo marefu. Inaelezwa kuwa, wakati mwingine hali hii husababisha hata baadhi ya majengo kuanguka na kuleta hasara ya vifo na mali.

Uchimbaji holela wa visima unasababisha pia watu kuvuta majitaka kutoka kwenye vyoo vya mashimo, mifereji ya maji machafu na hivyo, kuathiri ubora wa maji chini ya ardhi ambao ni vigumu kuurudisha katika hali yake ya kawaida. Wataalamu mbalimbali wanasema hali hiyo husababisha milipuko ya magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Kadhalika, husababisha kukauka kwa visima vya maji hasa vile vifupi baada ya kina cha maji kushuka. Hali kama hii imekwishajitokeza katika baadhi ya maeneo na kusababisha wananchi kupata hasara sambamba na kuendelea kuwa na uhaba wa maji kwa kuwa kuchimba kisima kirefu hugharimu fedha nyingi.

Kwa kuzingati hilo, Bodi ya Maji Bonde la Wami/ Ruvu inafanya utambuzi wa wamiliki wa visima na kutoa elimu ya Usimamizi wa Rasilimali ya Maji na kuwataka wananchi wasajili visima vyao kwa mujibu wa sheria itakayosaidia usalama wa maji. Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Namba 11 ya Mwaka 2009, inatoa haki kwa kila mtu kutumia maji.

Hata hivyo, sheria hiyo inafafanua pia kuwa, katika visima mtu anaruhusiwa kutumia maji bila kuomba kibali kama hana miundombinu katika kisima chake na pia kisima kilichochimbwa hakizidi mita15. Mintarafu suala hilo, Mwanasheria kutoka Bonde la Maji la Wami/Ruvu Monica Shio anasema:

“Kama kisima hicho kina urefu wa mita 8, lakini kina miundombinu, maana yake umeweka pampu ina maana uhitaji wako ni mkubwa utahitaji kibali.”

Anasema vibali vinavyotamkwa katika sheria hiyo ni kwa ajili ya kutumia maji, kuchimba kisima, kuchepusha maji na kutiririsha maji machafu ili kuhakikisha maji yanakuwa endelevu, safi na yasichafuliwe na kemikali.

Anasema sheria ya rasilimali hizo za maji inamtaka kila mkazi akaaye Tanzania Bara awe mdau, yaani awajibike kutunza na kulinda vyanzo vya na rasilimali za maji na awajibike kutoa taarifa ya tukio lolote kwa mamlaka husika endapo litaathiri ubora na wingi wa rasilimali za maji.

“Mtu ambaye chanzo cha maji kiko kwenye eneo lake anaweza kuyatumia kwa matumizi ya nyumbani tu, ili mradi kwa masharti ya sheria hii, hairuhusiwi kujenga miundombinu kwenye chanzo hicho,” anasema.

Kwa mujibu wa sheria, endapo katika ardhi anayoishi mtu kihalali yatapatikana maji chini ya ardhi, ataruhusiwa kujenga kisima cha mkono kwa ajili ya kutumia maji kwa matumizi ya nyumbani hata bila kuwa na kibali. Inasisitiza kuwa, yeyote anayetaka kuchepusha, kukinga, kuhifadhi, kuchukua na kutumia maji kutoka kwenye chanzo cha maji juu ya ardhi au chini ya ardhi au kujenga miundombinu yoyote lazima aombe kibali cha kutumia maji.

Hata hivyo, kibali kilichotolewa kwa mujibu wa sheria nyingine hakitahusisha matumizi ya maji au kuwa na uhalali wowote kwenye chanzo cha maji bila idhini ya maandishi kutoka Bodi ya Maji ya Bonde.

Utaratibu wa kupata kibali cha kutumia maji ya chini ya ardhi, kutiririsha maji machafu, kuandikisha haki ya kimila ya maji, kuandikisha matumizi ambayo yalikuwa hayana haki ya kutumia maji ni lazima mtu kupeleka maombi kwenye Bodi ya Maji ya Bonde na maombi yataangaliwa kanuni ambazo zitaeleza utaratibu wa kuomba vibali.

Aidha, kwa mujibu wa sheria hiyo, kibali cha kutumia maji hakimaanishi kuwa ubora na wingi wa maji ulioelezwa kwenye kibali utakuwepo.

Mtu yeyote anayetarajia kujenga, kuchimba, kuongeza ukubwa au kina cha kisima katika eneo lililotangazwa kuwa la hifadhi ya maji chini ya ardhi, anapaswa kuomba kibali cha maji chini ya ardhi, Bodi ya Maji ya Bonde ina mamlaka ya kufanya ukaguzi.

Shio amasema mtu yeyote anayejihusisha na uchimbaji au utafutaji anatakiwa kutunza na kuwasilisha kwenye Bodi ya Maji ya Bonde taarifa/takwimu za maji waliyokuta chini ya ardhi.

“Mtu mwenye lesenimaalumu ya madini au leseni ya kutafuta madini iliyotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123 au leseni ya kutafuta petroli endapo atakuta maji chini ya ardhi anapaswa (a) kuijulisha Bodi ya Maji ya Bonde mara moja kuhusu maji aliyokuta chini ya ardhi (b) kuwasilisha takwimu husika kwenye Bodi ya Maji ya Bonde, (c) kuchukua hatua stahili ili kuzuia uchafuzi wa maji chini ya ardhi, (d) kuzingatia maelekezo ya Bodi ya Maji ya Bonde kuhusu ulinzi au uondoaji wa maji. Mwanasheria huyu anafafanua kuwa, lengo serikali kuweka utaratiba wa vibali kwa wachimbaji wa maji ni bodi kujua visima vilivyopo.

Hii inalenga kuwezesha kuwapo takwimu sahihi zitakazomwezesha waziri kudhibiti uchimbaji holela wa visima na pia, kuhakikisha visima hivyo vinachimbwa sehemu sahihi.

Hata hivyo, yapo mambo yatakayochukuliwa kuwa ni mhusika kukiuka masharti ikiwa ni pamoja na mhusika kushindwa kutimiza masharti aliyopewa kwenye kibali, au amechukua au kutumia maji mengi zaidi ya kiasi kilichoruhusiwa.

Mwingine ni kama amejenga kisima au kukiongeza kinyume na masharti au vigezo vya kiufundi vilivyoelezwa kwenye kibali cha haki ya kutumia maji chini ya ardhi.

Kimsingi, endapo ukiukwaji unaweza kurekebishika, Bodi ya Maji ya Bonde itampa kwanza mwenye kibali taarifa ya maandishi inayoeleza ukiukwaji na kumtaka mwenye kibali kurekebisha mapungufu hayo ndani ya muda utakaoelezwa kwenye taarifa.

Endapo Bodi hiyo inaamini kuwa ndani ya miaka mitatu mfululizo mwenye kibali hajafaidika na kibali hicho, Bodi inaweza kumpa taarifa ya maandishi kumtaka aeleze ni kwanini kibali hicho kisifutwe au kurekebishwa.

“Endapo hakutakuwa na majibu ndani ya miezi mitatu tangu mwenye kibali alipopewa taarifa Bodi ya Maji Bonde inaweza kufuta au kurekebisha kibali husika, mwenye kibali anaweza kuwasilisha hoja kwa maandishi kueleza sababu ni kwa nini kibali kisifutwe au kurekebishwa au kuomba apewe fursa ya kusikilizwa,” inaelezwa.

Adhabu ya kutoa taarifa za uongo kwa bodi ni faini ya kuanzia Sh 500,000 hadi milioni tano au kifungo kisichopungua mwaka mmoja au kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi