loader
Picha

Umasikini, watoto kujilea chanzo mimba utotoni

WASICHANA wengi wanaopata mimba huishia kuishi maisha ya tabu huku wengine wakitelekeza watoto wao vijijini na kwenda mjini kutafuta kazi za ndani. Eliza (16), mkazi wa kijiji cha Chalinze Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Chibulunje alifukuzwa shule kutokana na ujauzito.

Eliza ambaye sasa ni mama wa mtoto mwenye umri wa mwezi moja, katika mahojiano anasema alikuwa akisoma darasa la sita akati alipogundulika kuwa ni mjamzito. Anasema ujauzito huo alianza kuugundua yeye mwenyewe baada ya kukosa siku zake kwa miezi mitatu.

"Baba wa mtoto hayupo, alishakimbia baada ya mimi kugundulika kuwa ni mjamzito,” anasema Eliza na kutaja aneo analotoka kijana huyo kuwa ni Manchali.

Eliza ambaye kwa sasa anaishi na mama yake mzazi na baba yake yuko mkoani Tanga ambapo hujishughulisha na vibarua kwenye mashamba, anasema alijiingiza katika mapenzi kutokana na ugumu wa maisha.

Anasema pamoja na nia hiyo, hali yake ya sasa ni mbaya zaidi kwani hawezi kujitunza mwenyewe wala mtoto wake na kwamba mama yake ndiye anayewatunza. “Huyo mwanaume sijamuona tena," anasema.

Kwa maneno yake binti huyo anasema maisha magumu yamekuwa yakisababisha wasichana kama yeye kujiingiza kwenye mapenzi wakiwa na umri mdogo na kwa kutojitambua wanabeba mimba na kuzaa watoto wenzao.

Msichana mwingine, Sophia Simon (21) ambaye pia ni mkazi wa Chalinze anasema yeye ni mama wa familia ya watoto wawili wasio na msaada wa baba zao na hiyo inatokana na hadithi ndefu.

Binti huyo ni miongoni mwa maelfu ya wasichana nchini Tanzania walioathirika na mimba za utotoni. Nilimfahamu binti huyo kupitia kwa Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai, baada ya kumueleza azma yangu ya kufanya mazungumzo na wasichana waliokatisha masomo kutokana na ujauzito ili watoe shuhuda jamii ijifunze kitu kutoka kwao.

Takribani mwendo wa robo saa kutoka barabara kuu hadi kufika kijijini hapo kwa kutumia pikipiki, nilifika katika makazi ya binti huyo na kumkuta akiwa na mama yake na ndugu zake wengine. Wanaishi kwenye nyumba kubwa iliyojengwa kwa matofali ya kuchoma.

Nilijitambulisha, na kwa kuwa tayari nilishafanya mazungumzo naye kwa njia ya simu na kukubali kuzungumza, nilipomkumbusha alitabasamu kisha akacheka huku akifunika uso wake kwa mkono kama mtu aliyekuwa akiona aibu.

WAZAZI KUTENGANA

Alinieleza kuwa, alipozaliwa alikuwa akilelewa na baba na mama, lakini alipofikisha miaka mitatu, anaambiwa wazazi wake walitengana na ndipo akaanza kulelewa na bibi mzaa mama na hivyo sehemu kubwa ilikuwa mithili ya kujilea.

“Nilipoanza darasa la kwanza ndilipo nilipochukuliwa na bibi mzaa baba,” ana na kuongeza kwamba hata huko maisha yalikuwa ya kuungaunga kutokana na hali ya umaskini iliyokuwa kwenye familia.

Anasema kupata milo mitatu kwa siku ilikuwa ikitokea mara chache na kwamba familia hiyo kumudu hata milo miwili kwa siku ilikuwa ‘mbinde’ pia.

MAISHA SEKONDARI MAGUMU

Anasema pamoja na umaskini wao, alipofika darasa la saba alifaulu na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Manchali na hivyo kulazimika kwenda kuishi kwa baba yake mzazi.

Anasema wakati ule baba yake alikuwa ameoa mke mwingine na mama yake akiwa ameolewa na mume mwingine ambako alikuwa na watoto wengine.

Anaeleza kuwa maisha hayakuwa rahisi hata kidogo kwani alikuwa hapewi fedha yoyote kwa ajili ya kujikimu kwenye mahitaji yake akiwa kama mtoto wa kike. Sophia anasema ugumu wa mazingira aliyokuwa akiishi ndiyo ulimsababishia kujiingiza kwenye mapenzi mapema.

"Ikafika wakati nikawa napata msaada kwenye Shirila lisilo la Kiserikali la Watoto Seremala. Wakawa wakinipa msaada wa sare, vifaa vya shule na fedha kidogo kwa ajili ya kujikimu.

"Maisha yaliendelea hivyo hivyo, navumilia kuishi na mama wa kambo, mara ninyimwe chakula na ugumu huo wa maisha ukapelekea kuingia kwenye mapenzi na kijana wa kijijini ambaye alikuwa akiitwa Gerson," anasema na kuongeza kwamba si baba wale mama aliyekuwa akijali malezi na makuzi yake.

Anasema kijana huyo alikuwa akiishi Singida na alikuwa akija kijijini hapo kwa mjomba wake.

KUPIMWA UJAUZITO

Hata hivyo, alipofika kidato cha nne kulikuwa na mwanafunzi wa kike waliyekuwa wakimshuku kuwa ni mjamzito ndipo walimu wakasema wasichana wote wa kidato cha nne waende kupimwa ujauzito zahanati ya Manchali.

Anasema majibu hayakuwa mazuri kwake kwani aligundulika kuwa na ujauzito wa miezi mitatu. Akasimamishwa masomo na kuambiwa mpaka bodi itakapokaa watapewa majibu kama watarudishwa kufanya mitihani au la.

“Lakini hatukupewa majibu na hivyo nikapoteza fursa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne,” anasema.

Sophia anasema alirudi nyumbani na kukaa mpaka alipojifungua mtoto wa kike ambaye kwa sasa ana miaka miwili.

Kijana aliyempa ujauzito huo hakuwahi kumuona tena kwani mara tu aliposikia kuwa ni mjamzito hakuonekana tena hapo kijijini na hawana mawasiliano kwani hata namba ya simu alibadili.

“Wakati nalea mtoto huyo kuna wakati tulitafutwa wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na kupata mimba, tukaundiwa kikundi, tukafundishwa ujasiriamali wa kutengeneza sabuni za usafi na hata batiki,” anasema.

Wakati akiwa katika kuendelea na maisha yake ya ujasiriamali akiwa na lengo la kuongeza kipato ili aweze kujitegemea na kulea mtoto wake, ndipo akakutana na kijana mwingine ambaye alikuwa ni mtoto wa mchungaji katika kanisa la Anglikana.

Kijana huyo anamtaja kwa jina la Geoffrey. Kijana huyo alimpa matumaini kuwa watayajenga maisha pamoja na hivyo kumfanya ‘kujiachia’ kwake akimwamini.

Sophia anasema alipata tena ujauzito lakini wakati akiwa mjamzito mchungaji huyo alihama kijijini hapo na familia yake na hajui walipohamia ila amekuwa akiwasiliana na kijana huyo akimwahidi kwamba atakuja kumsalimia mtoto.

"Sijui kama atakuja mtoto ana wiki tatu sasa,” anasema binti huyo.

Anasema maisha yake yamekuwa kama mtihani mgumu, kwani ni kweli awali alifanya kosa na akili yake ilikuwa haijakomaa wakati akilaghaiwa, lakini kwa mimba ya pili alimwamini mtu ambaye alidhani kuwa ataweza kuja kumsaidia. “Lakini mambo yamekuwa tofauti na nilivyokuwa nikifikiri,” anasema Sophia akionesha kujuta.

Sophia anaamini kwamba sababu nyingi za mimba za utotoni kama iliyotokea kwake ni ugumu wa maisha na malezi yasiyothabiti kutoka kwa wazazi. "Msichana anapokosa mahitaji muhimu ya maisha hujikuta katumbukia huko. Naomba wazazi wasikwepe kutimiza majukumu ya familia ili watoto wafikie ndoto zao, mimi nilikuwa nasoma kwa bidii ili nije nikomboe familia yangu, lakini ndoto yangu sasa imepotea," anasema.

Anasema kuparaganyika kwa ndoa kama ilivyotokea kwa wazazi wake nako kunatoa nafasi kwa mtoto kuharibikiwa na hivyo anahimiza wazazi walio katika ndoa kujitahidi kuwa pamoja kwa faida ya watoto.

Anasema mtoto anapopewa jukumu la kujilea mwenyewe madhara yake huwa ni makubwa kwani wengi hufikiria watoto wanaopata mimba mapema ni malaya, lakini hilo si kweli kwani unaweza kufanya mapenzi siku moja tu na ukapata ujauzito.

“Tunakuwa tunapitia wakati mgumu kwenye familia, hakuna anayejali mahitaji yako unapoamua kujitafutia chochote unaishia kuharibikiwa. Yaani mimi sikuwahi kufikiria maisha yangu yatafikia hapa nilipo na kwenye umri huu.

"Utakuta usiku hujala, asubuhi unakwenda shule na njaa, mwalimu anafundisha wala huelewi. Unaona maluweluwe tu, unapiga miayo wala huelewi kinachofundishwa, vitu kama hivyo vinamfanya msichana kuanguka katika vishawishi," anasema.

MAMA MZAZI AFUNGUKA

Mama mzazi wa Sophia, Happy Chaurembo ambaye ni mkulima, anasema aliumia sana binti yake alipopata ujauzito.

Anakiri kwamba yeye kama mzazi anaona ana hatia ya kutotimiza ipasavyo wajibu wake wa kulea mtoto huyo baada ya kuachana na mzazi mwenzake.

Anasema alitengana na baba yake Sophia wakati Sophia akiwa na miaka mitatu na hivyo mwanae akalazimika kulelewa na bibi yake.

"Baada ya Sophia kupata ujauzito kama mzazi nilichukua jukumu la kumrudisha nyumbani na sasa tunaishi wote hapa nikimhudumia yeye na watoto wake," anasema. Anasema Sophia ana matamanio makubwa ya kuwa mjasiriamali, ila mtaji ndio umekuwa ukimkwamisha.

Anasema maisha yao ni ya kawaida na amekuwa akijitahidi ili wajukuu wake wapate huduma inavyotakiwa.

Anasema kutengana kwa wazazi mara nyingi kumekuwa na athari kwa maisha ya watoto kwani hapo baba anakwenda tena kuoa na mama anakwenda kuolewa na wote wanakuwa na miji mipya na maisha mapya huku watoto wakiachwa kulelewa na bibi zao, na ndivyo ilivyokuwa hata kwake.

UMBALI KWENDA SHULE

Diwani wa kata ya Manchali, Mary Mazengo, anasema: "Mwaka jana katika kata ya Manchali wanafunzi saba walipata ujauzito; wawili ni wa shule ya msingi na watano wa sekondari."

Anasema umbali wa kutoka shuleni hadi yalipo makazi ya watu kuwa moja ya sababu za mimba za utotoni kwani mara nyingi watoto hupata vishawishi wakiwa njiani. Anasema tatizo lingine ni watoto kushindwa kutoa ushirikiano juu ya wahusika wa mimba zao.

"Mtoto hata umbane vipi hawezi kumtaja aliyempa ujauzito, tatizo lingine ni malezi ya wazazi, hawawafuatilii watoto wao. Kwa mfano, eneo la Chalinze Nyama ambapo kuna stendi ya malori watoto wanazurura hadi saa tano za usiku. Kama mzazi unatakiwa ujue muda ambao mtoto anatakiwa kwenda kulala," anasema.

Aidha anasema kundi lingine la watoto linaloathirika na mimba za utotoni ni wafanyakazi wa kazi za ndani.

Diwani huyo anasema miaka sita iliyopita kuna binti wa miaka 14 alikwenda kufanya kazi za ndani Dar es Salaam, bosi wake alikuwa akimbaka akapata ujauzito.

"Badae akarudi akawa anaishi kwangu, kumbe wakati anarudi alikuwa mjamzito, hata hivyo mimba ilikuwa haionekani alikuwa na umri mdogo ambao huwezi kudhani kuwa ni mjamzito," anasema.

Anasema binti huyo alijifungulia hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa njia ya operesheni na baada ya miezi sita nikamruhusu arudi kwa wazazi wake waliokuwa wakiishi kijiji cha Majereko na kwamba baada ya miaka miwili binti yule alifariki dunia baada ya kuugua.

Anasema mimba za utotoni zina athari kubwa kwa maisha ya wasichana wadogo kwani wakati mwingine zimekuwa zikigharimu uhai wao.

IMANI POTOFU

Aidha anasema imani potofu zimekuwa zikitumika na watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji ili wapewe kinga wasikamatwe.

Kwa upande wake anaona hilo ni tatizo kubwa katika maeneo ya vijijini na elimu zaidi inahitajika ili imani hiyo isitumike katika kuharibu maisha ya wasichana wadogo ambao wana ndoto za kujiendeleza kielimu.

Anasema viongozi kuanzia ngazi za vitongoji wana wajibu wa kuhakikisha wanawafuatilia watuhumiwa ili wafikishwe kwenye mikono ya sheria na si kutishika na imani za kishirikina.

KUSAIDI WASICHANA WAZAZI

Joanita Kahangwa, mkazi wa Kijiji Cha Chalinze Nyama, kata ya Manchali anasema mwaka jana waliamua kukusanya wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni ambao sasa hivi wana watoto.

Anasema walifanikiwa kupata wasichana 24 ambao waliwapatia elimu ya ujasiriamali hususani kutengeneza sabuni za usafi na kutengeneza batiki.

"Tulipopata wazo hilo tukaanza kupita nyumba hadi nyumba kutafuta wasichana hao, lakini jambo la kushangaza baadhi ya watu walikuwa wakisema tunataka kuwatumia wasichana hao kama chambo cha kupata fedha za wafadhili. Ukweli ni kwamba tulikuwa tunataka kuwasaidia ili wapate ujuzi utakaowasaidia kuongeza kipato ili waweza kujimudu katika maisha,” anasema

Anasema kupitia kikundi chao cha ujasiriamali cha Ujirani Mwema walipata mabinti hao 24 na kuanza kuwapa mafunzo na miongoni mwa mabinti hao ni Sophia ambaye alikuwa na moyo sana wa kujifunza na mpaka sasa anaweza kutengeneza batiki na sabuni za maji.

“Huwa tunamtumia kama binti wa mfano, natumaini akipata mtaji anaweza kuwa mjasiriamali mzuri kwani hatua za maisha alizopitia zimempa zaidi ujasiri wa kujitambua yeye ni nani," anasema.

WATUHUMIWA KUTOADHIBIWA

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Vumilia Nyamoga anasema kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kuwapa mimba wanafunzi kunaendelea kushamiri kutokana na wanaosababisha vitendo hivyo kutopata adhabu stahiki huku vitendo hivyo vikionekana kama vya kawaida katika jamii.

Kulingana na mkuu huyo wa wilaya, sera ya mtoto ya mwaka 2007 pamoja na sheria yake ya mwaka 2009 zinaweka bayana haki za watoto, wajibu wa watoto, wajibu wa wazazi, walezi, wajibu wa taasisi za serikali, wanasiasa, viongozi wa dini, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na wananchi.

Anabainisha kuwa, kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na UNICEF, WHO, na hata tafiti zilizotumika kuandika Mwongozo wa Kisera wa Sekta ya Afya wa Kuzuia na Kupambana na Ukatili wa Kijinsia uliotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mwaka 2013 na asasi nyingine zisizo za kiserikali na kuchapishwa katika mitandao zinaonesha wastani wa asilimia 60 ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike kutokea shuleni.

Aidha anasema wasichana watatu kati ya 10 wamefanyiwa unyanyasaji wa kingono, na mtoto moja wa kiume kati ya watoto saba wamefanyiwa ukatili kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Anasema unyanyasaji wa kimwili unaonesha asilimia 72 ya watoto wa kike na asilimia 71 ya watoto wa kiume wamefanyiwa ukatili kabla hawajafikishwa umri wa miaka 18, mtoto moja kati ya wanne wamefanyiwa unyanyasaji wa kijinsia kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Aidha anasema taarifa za kesi kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana kutoka dawati la polisi la kijinsia wilayani humo zinaonesha kwamba kulikuwa na kesi mbili za ubakaji watoto chini ya miaka 10, kufanya mapenzi na wanafunzi kesi nane, kulawiti kesi moja, kuzini na maharimu (ndugu) kesi mbili, mimba kwa wanafunzi kesi 10 na kutelekeza familia kesi nne.

“Nina taarifa za kesi mbili za ubakaji wa watoto zinazoendelea mahakama ya wilaya, ninataka kujua pia hatua za kesi nyingine hadi sasa,” anasema mkuu huyo wa wilaya.

Pia anasema kuna watoto wilayani humo wanafanyiwa ukatili wa kijinsia nyumbani kwa kushawishiwa wasifanye vizuri katika mitihani yao ya kumaliza darasa la saba, ili waolewe au wakafanye kazi za ndani kuongeza kipato kwa familia.

WAZAZI KUOZA WATOTO

“Lakini pia kuna watoto wanashawishiwa waache shule huku wazazi wakiwaficha watoto wenye ulemavu, watoto wengine wakipata vipigo kutoka kwa wazazi, walezi wao, wanapokwenda kuanya kazi za ndani wanafanyiwa ukatili ikiwemo vipigo, kusimangwa kwa matusi na ubakaji huku familia yake inapokea mshahara wa mtoto bila kujali anateswa au la,” anasema.

Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai anasema wananchi wana wajibu wa kutoa taarifa juu ya matukio ya ukatili ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua.

Anasema ni vyema mashahidi wakatoa ushirikiano wa kutosha wakati wa kuendelea kwa kesi hizo mahakamai ili haki iweze kutendeka.

NDUGU KUSIHIRIKI NGONO

Pamoja na hayo anasema kuwa katika wilaya hiyo kuna tabia ya ndugu kushiriki mapenzi. "Utakuta mtu na mjomba wake ni wapenzi na watoto wengi wanaopata mimba wahusika ni ndugu wa karibu, hali ambayo husababisha wahusika kutotajwa ili kulinda undugu na kama kesi iko mahakamani hawako tayari kwenda mahakamani kutoa ushahidi,” anasema Swai.

Pia anasema kuna baadhi ya mila ambazo zinataka mtoto anapovunja ungo asikae nyumba moja na wazazi wake. “Baadhi ya maeneo ukifika nyumba wanazolala watoto huwa mpaka uvuke barabarani, kwa mazingira hayo watoto wanakosa ulinzi hasa nyakati za usiku na kujikuta wakiingia kwenye mahusiano ya kingono,” anasema.

Anasema kuna mwanafunzi alipata ujauzito kumbe alikuwa na mahusiano na binamu yake ambaye mara nyingi alikuwa na mazoea ya kufika nyumbani kwa wazazi wa binti, anasema kijana huyo alikuwa akirudi usiku kulala na binti huyo na alikuwa akipitia dirishani.

Swai anasema baada ya binti kupata ujauzito na kumtaja wazazi waliamua kumaliza suala hilo kimya kimya na binti akafukuzwa shule kutokana na ujauzito. Mkazi wa Buigiri wilaya ya Chamwino, Newton Chamagenzi (65), anasema utamaduni wa kuoana ndugu kwa ndugu katika wilaya ya Chamwino upo.

“Sasa hivi wazazi wamejisahau sana katika suala la malezi, sasa watoto wanakaa kwao na wazazi kwao na hawazingatii suala la kulinda watoto jambo ambalo limekuwa likisababisha watoto kupata ujauzito wakiwa shuleni,” anasema Chamagenzi.

Mtendaji wa kijiji cha Wilunze kata ya Machali, Georgina Richard, anasema kumekuwa na tatizo kubwa kwa watoto kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo.

Anasema hata linapokuja suala la msichana kapata mimba, wazazi hawako tayari kutoa ushirikiano ili suala hilo lifike mahakamani ushahidi utolewe, lakini badala yake wazazi wa pande zote wanaelewana na kumaliza suala hilo.

WAZAZI KUKWEPA POLISI

Aliyekuwa Mratibu wa dawati la Jinsia Wilaya ya Chamwino, Krista Kayombo ambaye kwa sasa amehamishiwa Dodoma Mjini, anasema wazazi wengi wamekuwa hawafikishi polisi kesi za watoto wanapopata ujauzito.

“Mtoto analetwa kituoni baada ya kushindwa kumalizana kifamilia. Kinachotakiwa ni kuwa na ushirikiano. Kinachofunga mtu ni ushahidi,” anasema Kayombo na kuongeza kwamba kwa sasa kesi zinazopelekwa polisi kuhusiana na mimba za utotoni zinashughulikiwa haraka tofauti na miaka ya nyuma.

Anasema wakati mwingine kesi ya kumpa mimba mwanafunzi inafikishwa polisi tayari mtoto anakuwa tayari ana miaka miwili.

“Kesi kama hii inakuwa vigumu kuishughulikia kwani kwanza unajiuliza siku zote alikuwa wapi. Lakini ukichunguza utaona kulikuwa na makubaliano ambayo sasa yamekiukwa,” anasema.

Anasema sasa katika wilaya ya Chamwino makosa yanayoongoza ni ubakaji, ulawiti na mimba za utotoni.

Anasema wakati mwingine kuna kutoelewa kwa sheria kwa wananchi kwani mzazi anadhani akimshtaki aliyempa mimba mtoto wake kesi hiyo haina dhamana, lakini mshtakiwa akipewa dhamana na kuwa nje wanasema polisi wamepewa rushwa na kumwachia mtuhumiwa.

“Wakati mwingine wananchi waelimishwe kama kuna kesi zenye dhamana na zisizo na dhamana,” anasema.

Anasema tatizo la watoto kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo limekuwa kubwa na hivyo jamii inawajibika kuzingatia maadili ya watoto kwa ajili ya ustawi wa maisha yao ya baadae. Kayombo anasisitiza kuwa tatizo la kupotosha ukweli limekuwa likirudisha nyuma juhudi za kupambana na mimba za utotoni.

“Utakuta mtu kapewa mimba na Juma, lakini akifika kituoni kujohiwa anasema amepewa mimba na Hamisi au alibakwa kisimani au na dereva wa gari kubwa akiwa na lengo la kumficha mhusika asifungwe, akihofia kuzaa mtoto atakayekuwa na baba anayeishi gerezani,” anasema.

KESI NYINGI KUFUTWA

Pia anasema changamoto nyingine ni waliopata madhara katika matukio hayo kutofika kutoa ushahidi na kusababisha kesi kufutwa.

“Kuna changamoto za rushwa, upelelezi chini ya kiwango usio na ufanisi na wa kizembe na umbali waliopo walalamikahi kuwawezesha kufika, mahakamani kutoa ushahidi kila wanapohitajika,” anasema.

Pia anasema kesi nyingi zimekuwa hazifiki ukongoni kutokana na kuharibiwa kwa ushahidi. “Kesi inafunguliwa ya kumpa mimba mwanafunzi, anajifungua na baadaye anaamua kuishi na mtuhumiwa. Wakati kesi inaendelea wanakuja mahakamani wakiwa wameongozana, hapo kuna ushahidi wa kumfunga mtuhumiwa kweli?” anahoji.

MIMBA ZA UTOTONI CHAMWINO

Takwimu zilizotolewa na Mkuu wa wilaya ya Chamwino zinaonesha kuwa, tatizo la mimba za utotoni nchini limeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2016/17. Sababu kubwa ikitajwa ni ukosefu wa huduma pamoja na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 19.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Venerose Mtenga, anasema jamii ina wajibu wa kulisemea hilo ili kupunguza idadi ya watoto wanaopata ujauzito wakiwa na umri mdogo.

Hata hivyo, Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto (Unicef) linasema Tanzania ni ya tatu kwa ndoa za utotoni Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Unicef imesema kuna mafanikio makubwa ya kupungua kwa ndoa za utotoni duniani ambapo inakadiriwa kuwa ndoa za utotoni zipatazo milioni 25 zimeweza kuzuiliwa katika muongo iliyopita. Kwa mujibu wa takwimu za Unicef za kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.

Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40.

Tanzania ni asilimia 31. Kenya ni watoto asilimia 23 wanaoozwa kabla ya kutimiza miaka 18. Mwisho Kaption 1. Binti aliyekatisha masomo kutokana na ujauzito, Sophia Simon akiwa nyumbani kwa mama yake mzazi 2.

Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai akitoa elimu kwa wazazi na wanafunzi wa shule ya Msingi Mlowa barabarani Wilayani humo.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi