loader
Picha

Tanzania ichangamkie soko la gesi EAC

SERIKALI za Tanzania na Uganda zina mpango wa kujenga bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Kijiji cha Chongoleani mkoani Tanga, likiwa na urefu wa kilometa 1,445 huku sehemu kubwa likiwa katika ardhi ya Tanzania.

Lakini, wakati kukiwa na mpango huo, Serikali ya Uganda imeomba kupelekewa gesi ili iweze kusaidia uzalishaji viwandani.

Hivyo, tunahimiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuchangamkia soko la nishati ya gesi lililopo Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki (EAC) za Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Tunaomba uongozi wa TPDC kujenga bomba la gesi asilia, ambalo litaisaidia Tanzania kufanya biashara ya gesi siyo na Uganda pekee, bali na nchi nyingine za EAC.

Tunaomba mipango ya kujenga bomba hilo la kusafirisha gesi asilia kutoka Uganda iharakishwe, ikiwemo kukamilisha upembuzi utakaotoa taswira halisi ya jinsi mradi huo utakavyotekelezwa.

Jambo la kukumbuka ni kuwa gesi ilivumbuliwa Tanzania mwaka 1974 huko Songosongo mkoani Lindi. Kwa sasa Tanzania ina hazina kubwa ya gesi, yenye ujazo wa futi trilioni 57.2 iliyothibitishwa.

Hicho ni kiasi kikubwa kinachoweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa na kwa kasi uchumi wa nchi. Gesi ina faida nyingi ambazo kwanza ni biashara nzuri na pili inasaidia kuleta umeme wa uhakika na wa bei nafuu, hivyo kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya viwanda.

Faida nyingine kutokana na gesi ni kusaidia utunzaji wa mazingira na kuchochea matumizi ya gesi asilia nyumbani, hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira wa utumiaji wa mkaa na kuni.

Pia, gesi inapanua wigo wa ajira na kuinua sekta ya kilimo, inayochangia kwa kiasi kikubwa malighafi za viwandani.

Aidha, kwa sasa vyanzo kadhaa vya asili, kama makaa ya mawe na mafuta, vimekuwa vikipungua kila siku, hivyo ni vema kuwekeza katika gesi asilia.

Hali kadhalika, kutokana na maendeleo ya teknolojia duniani, hivi sasa gesi imekuwa chanzo cha uhakika cha nishati, hata kwa nchi ambazo hazina visima vya gesi asilia.

Hivyo, Tanzania lazima ichangamkie suala hilo kwa kusambaza utajiri wa gesi asilia uliopo nchini kwa nchi nyingine za EAC.

Ni wazi kuwa Tanzania ikianza kupeleka gesi nchini Uganda, itafanya biashara nzuri na kwa muda mrefu, hivyo kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa nchi.

KITUO cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinajitahidi sana kuboresha shughuli za ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi