loader
Picha

Suba wanavyopania kunusuru wanafunzi Rorya

“HAYA ni matokeo chanya ya Sera ya elimu bila malipo kwa kuwa watoto hawa, ndio ‘intake’ ya kwanza kuingia kidato cha kwanza maana wakati sera hii inaanza kazi, hawa vijana walikuwa darasa la tano… kabla ya hapo, watoto wetu wengi walikuwa wanaishia njiani kabla ya kumaliza shule, lakini sasa karibu wote wanamaliza ndiyo maana kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya madarasa.”

Anasema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Charles Chacha katika uzinduzi wa harambee kuchangia ujenzi wa madarasa katika Tarafa ya Suba, wilayani Rorya, mkoani Mara iliyoandaliwa na Umoja wa Maendeleo wa Wananchi kutoka Tarafa ya Suba.

Chacha anaongeza: “Waliokuwa wanaishia njiani, sasa wanaendelea, na walifanya vizuri wakafaulu. Hii ni baraka hivyo, tusiruhusu umaskini utupoteze, bali tujitokeze popote tulipo tuchangie shughuli za maendeleo katika Tarafa ya Suba, Jimbo la Rorya, wilaya na hata mkoa wetu.”

Anawahimiza Wanarorya kuendelea kutimiza azima yao kuchangia na kutumia nguvu zao kujiletea maendeleo jambo linalostahili kuigwa na kuendelezwa hususan elimu na afya.

“Nawapongeza kwamba sasa Suba kuna mwamko wa jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo ndiyo maana kwa mfano, katika Kijiji cha Kwibhuse wananchi wanajenga shule mbili za sekondari,” anasema na kuzitaja shule hizo kuwa ni Kukona na Kwibhuse.

Mkurugenzi huyo anashauri Wanasuba na Wanarorya kuwa jumla, kuungana kuhakikisha wanawanusuru watoto wanaofaulu kujiunga kidato cha kwanza, lakini wakashindwa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa ili wale wa kike wasiishie kuolewa na wa kiume wasizamie katika uvuvi.

Chacha anasisitiza kuwa, wananchi wa Suba pia waongeze nguvu ili wawezeshe ujenzi wa mabweni ili kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike kusoma, kuhitimu na hata kufaulu katika masomo ya sekondari.

Anasema: “Ili kuchochea ari ya masomo, ni vema hata zile shule za sekondari za Waningo na Kyang’ombe tuzijengee hosteli kuwezeshesha watoto wengi wa kike kusoma na hasahasa, kwa kuanzia, wale watakaofaulu mtihani wa kidato cha pili ili wawe hosteli.”

Uchunguzi wa makala haya katika vyanzo mbalimbali unabaini kuwa, miongoni mwa sababu zinazokwamisha wanafunzi wa kike katika shule za sekondari kukamilisha masomo na kufaulu ni pamoja na ukosefu wa mabweni au hosteli.

Ukosefu huu huwafanya wengine kutumia muda mwingi kutembea kwenda na kutoka shuleni huku wakikutana na vishawishi mbalimbali njiani na wengine kuishi geto huku wakikumbana na ugumu wa maisha unaowafanya wengine kupata ‘wachumba.’

Utafiti mmoja wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kupitia mradi wa GEWE miaka kadhaa iliyopita, ulibaini kuwapo baadhi ya wanafunzi waliokuwa wamepanga katika nyumba za watu binafsi, hatimaye wakaolewa na wenye nyumba. Kimsingi, Suba ni miongoni mwa tarafa nne za Wilaya ya Rorya katika Mkoa wa Mara.

Tarafa nyingine ni Girango, Luo-Imbo na Nyancha. Hii ni wilaya mpya iliyoanzishwa mwaka 2007 kutoka katika Wilaya ya Tarime. Upande wa Mashariki inapakana na Tarime, Kusini inapakana na Wilaya ya Butiama, Magharibi inapakana na Ziwa Victoria huku Kaskazini ikipakana na Nchi ya Kenya.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Wilaya ya Rorya ina wakazi 265,241 wanawake 138,994 na wanaume 126,247 huku kukiwa na vijana wengi wenye umri wa kuwa shuleni Katika uzinduzi huo wa harambee inayolenga kutafuta Sh milioni 360, Katibu wa Kamati ya Harambee, Pilly Marwa, anasema hadi mwisho wa uzinduzi huo uliofanywa na Mbunge wa Rorya aliyekuwa mgeni rasmi, Lameck Airo, Sh 70m/= zilikuwa zimepatikana huku watu wengine wakiendelea kuchangia kwa njia mbalimbali.

Kama alivyosema Pilly, wadau wa maendeleeo ya elimu wakiwamo marafiki wa Tarafa ya Suba na Jimbo la Rorya walio ndani na nje ya Suba, Jimbo la Rorya, ndani na nje ya nchi, waendelee kuchangia ufanisi wa juhudi hizo kwa namna mbalimbali ikiwamo ya fedha na vifaa mbalimbali vya ujenzi.

“Tunaomba hata walioshindwa kufika hapa, waendelee kuchangia fedha kupitia benki ya CRDB katika akaunti namba 0150431073801 iitwayo Maendeleo-Suba Education Fund na kutoa taarifa kwa viongozi wa Umoja na Kamati,” anasema Pilly.

Anasema Sh milioni 70 zilizopatikana siku hiyo, zinahusisha ahadi, fedha taslimu na vifaa vya ujenzi na lengo ni kupata Sh milini 360 ili kujenga madarasa 18 katika Shule za Sekondari za Kyang’ombe, Nyamunga, Nyihara, Kisumwa, Waningo na Suba. Katika uwasilishaji wa ripoti kabla ya kuanza uchangiaji, Pilly anasema:

“Hizi Sh milioni 360 ni wastani wa Sh milioni 20 kwa kila darasa kati ya madarasa 18 yanayohitajika katika shule hizo sita za sekondari.”

Mwenyekiti wa Umoja huo, Lucas Msimbete, anasema lengo la harambee hiyo ni kupata fedha na vifaa mbalimbali vitakavyowezesha kuboresha miundombinu ya shule za sekondari na madarasa katika tarafa hiyo ili kuwezesha watoto hao kupata haki yao ya elimu bora na kwa wakati.

“Tumelenga kuwasaidia vijana wetu walioshindwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza (sekondari) mwaka 2019 kutokana na upungufu wa madarasa,” anasema.

Anaongeza: “Tukio hili ni uzinduzi wa mpango endelevu wa kushirikiana kutatua changamoto za elimu katika Tarafa ya Suba na Jimbo la Rorya. Hivyo, harambee hii ya ya Karimjee ni uzinduzi rasmi wa kuangaza kwa mapana suala la maendeleo katika Tarafa ya Suba katika nyanja za elimu, afya, maji, umeme, teknolojia na hifadhi ya mazingira.”

Kwa mujibu wa Msimbete, harambee itakayofuata itajikita kutanua wigo wa mahitaji ya elimu kwa shule za tarafa hiyo.

“Hapo sasa tutaangaza katika kuboresha shule zilozopo, nyumba za waalimu, maabara, vyoo vya shule na vifaa vya kufundishia,” anasema na kuongeza: “Ndiyo maana hata sasa kamati inaendelea kutafiti mahitaji kwa kupitia wataalamu ili kupata mahitaji halisi ya shule zilizopo katika Tarafa ya Suba.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Harambee hiyo, Chacha Nshoya, naye anasisitiza kuwa, uchangiaji katika harambee hiyo umelenga kuwanusuru watoto 846.

Vijana waliofaulu ni 1246 kati yao wasichana ni 546 na wavulana 700. walioshindwa kuendelea na masomo wakiwamo wa kike ili wasitumbuukie katika janga la ndoa na mimba za utotoni huku wa kiume wakiishia katika uvuvi wa samaki katika Ziwa Victoria. Kamati ya Harambee ilichiangia Sh milioni 15 huku Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ikichanguia Sh milioni tano.

Katika uzinduzi huo, Mbunge Airo anawapongeza Wanasuba kwa kujitoa kuunga mkono juhudi za serikali kujiletea maendeleo hasa katika suala la elimu ambayo ni urithi wa kudumu kwa watoto na silaha dhidi ya maradhi na umaskini.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Albert Machiwa anasema kwa kujitoa huko, Wanasuba na Rorya wanakuwa mfano bora wa chachu katika kubadili na kuondoa mitazamo hasi ya baadhi ya wanajamii wanaodhani maendeleo lazima yaletwe na serikali na hivyo, watu hao kusita kushiriki.

Anasema: “Kwa mfano, katika elimu, watu wetu ni wazito hasa katika kutoa michango huku wangine wakisingizia na kuchanganya siasa katika mambo ya maendeleo. Hiki mnachokifanya nyie, ni njia na mwanga bora wa kuiga na kuendeleza.”

Anawahimiza wanavijiji wa Suba kuchangia ujenzi huo japo kwa malipo ya mafundi baada ya vifaa kupatikana ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa madarasa na kukidhi mahitaji sambamba na ongezeko la watoto lisiloendena na ongezeko la madarasa. “Unajua hata uzazi wetu una kasi ya kutisha kuliko uwezo wa madarasa hasa katika shule za msingi…” anasema Machiwa.

Katika hotuba ya uzinduzi, Mbunge wa Rorya, Lameck Airo anakiri kuwapo changamoto ya baadhi ya watu kushindwa kutofautisha mambo ya maendeleo yasiyobagua na badala yake, wanayachanganya na siasa. “Hata baadhi ya wasomi mara nyingine wanajisahau kwa kutumia majukwaa ya siasa kuwadanganya wananchi, badala ya kutumia kalamu zao kuleta maendeleo katika jamii yao.”

Anasema Wanasuba ni mfano wa kuigwa kwa kuwa wanatumia nafasi zao walipo kuchangia maendeleo ya Suba na Rorya kwa juma, hususani katika elimu.

Mjumbe wa Kamati ya Harambee, Francis Kibhisa anasema baada ya uzinduzi huo, sasa inafuatia harambee nyingine kubwa itakayoshirikisha mashirika ya umma, serikali, taasisi za umoja wa mataifa na taasisi binafsi.

“Huu ni moto wa maendeleo utakaosambazwa Rorya nzima,” anasema Kibhisa na kuongeza: “Maendeleo ya watu yakiwamo ya elimu, yanahitaji umoja na kujitoa na kwa kuunganisha nguvu namna hii, tutaiunga mkono Serikali yetu katika kuelekea uchumi wa viwanda…. Huu ni moto wa maendeleo tulioamua kuusambaza Rorya nzima.”

Wadau hao wa maendeleo licha ya kuchangia ujenzi wa madarasa katika shule hizo, wanasema lazima juhudi ziwekwe kuhakikisha wanaosoma na kuhitimu, wanatoka wakiwa wameiva kwa elimu bora.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi