loader
Picha

Waziri Mkuu anayekumbukwa kwa mengi mazuri Tanzania

“NDUGU wananchi, leo majira ya saa 10 jioni, ndugu yetu, kijana wetu na mwenzetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, wakati akitoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake imepata ajali, amefariki dunia.”

Sauti ya Rais Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere inasikika ikitamka maneno hayo Jumatano, Aprili 12, 1984 majira ya saa 11:30 jioni. Kipindi cha salamu cha ‘Jioni Njema’ cha Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo sasa ni TBCTaifa, kilikuwa hewani. Ghafla matangazo yake yanakatishwa na wimbo wa Taifa ukapigwa. Nyerere akatoa taarifa hiyo ya majonzi kwa taifa.

Waziri Mkuu Edward Sokoine, “amekwenda, amekufa.” Leo Aprili 12, Watanzania wanaadhimisha Kumbukizi ya miaka 35 tangu kufariki kwa Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Nyerere, Aprili 12, 1984 kwa ajali ya gari. Ni kwa msingi huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anasema: “Serikali na Watanzania wote kwa jumla, wataendelea kumuenzi shujaa huyo, Edward Sokoine.”

Anayasema hayo katika hotuba yake ya uzinduzi wa marathon kwa ajili ya Kumbukizi ya Miaka 35 tangu kufariki dunia kwa Sokoine. Uzinduzi wa mbio hizo ulifanyika Aprili 6, 2019 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Anasema katika kipindi cha uhai na utumishi wake, Sokoine alijitoa kwa dhati kuchapa kazi na kulitumikia taifa kwa bidii, uaminifu na uadilifu mkubwa. Kutokana na hali hiyo anasema, Taifa na Watanzania kwa jumla, wataendelea kufuata nyayo za Sokoine katika mema mengi aliyoitendea Tanzania na siku zote watandelea kumuombea kwa Mungu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, miongoni mwa mambo ambayo taifa limefanya ili kuendelea kumwenzi Sokoine, ni pamoja kuamua kwa makusudi kukiita Chuo Kikuu cha Kilimo cha Morogoro kwa jina la Sokoine, yaani Sokoine University of Agriculture (Sua). Anasema, kufanyika kwa mbio hizo ni ushahidi kwamba Sokoine bado anaendelea kukumbukwa, kuenziwa na kuheshimiwa na Watanzania kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa taifa.

“Katika uhai wake, Sokoine alikuwa mfano bora wa kiongozi wa juu wa nchi aliyedhamiria kwa dhati kupambana na vitendo vya rushwa, uonevu, ubadhirifu na ufisadi,” anasema Waziri Mkuu Majaliwa. Anaongeza: “Leo hii tunaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 35 ya Kifo cha Sokoine sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, John Magufuli inayoendeleza kwa vitendo utendaji, uadilifu na mtazamo aliokuwa nao Sokoine.”

Kumbukumbu zilizopo zinaonesha kuwa, kabla ya kifo chake, Waziri Mkuu Sokoine alikuwa akiongozi vita dhidi ya walanguzi na wahujumu uchumi nchini, hali iliyompa umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Profesa Raphael Chibunda anasema, Sokoine ana historia kubwa katika chuo kikuu hicho. Anasema ni kutokana na ushawishi alioufanya bungeni akiwa waziri mkuu, Sokoine alifanikiwa kuwashawishi wabunge kupitisha Muswada wa Uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro.

Hata hivyo, Profesa Chibunda anasema, baada ya kupitishwa na Bunge na kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hiki, Sokoine alifariki dunia kwa ajali wakati akirejea Dar es Salaam kutoka Dodoma. Chuo kikuu hicho kilianzishwa Julai Mosi, 1984 na kuzinduliwa Septemba 25, 1984 na Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa Kwanza wa Tanzania. Chibunda anasema, kwa kutambua mchango wa Sokoine kwa chuo hicho, mamlaka zilifikia uamuzi wa kukibadili kutoka jina la awali la Chuo Kikuu cha Kilimo cha Morogoro, na kuitwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua).

“Sokoine alikuwa mpigania haki na maendeleo ya watu wake wakiwamo wanyonge ili wapate haki na baada ya kifo chake mwaka 1991, Seneti ya chuo hiki ilipitisha kuwa na mhadhara wa kuenzi juhudi hizi akiwa ni chimbuko la chuo hiki,” anasema. Anasema baada ya seneti kupitisha azimio la kuwa na mhadhara huo ili kuenzi juhudi zake, kila mwaka kumekuwa na Wiki ya Kumbukizi ya Sokoine inayoanza Aprili 9 hadi 12. Chibunda anamtaja Sokoine pia kama kiongozi aliyekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa aliishi kama alikuwa ‘akihubiri’ na pia, mtu aliyepanda usawa kwa kila mtu.

Anasema Sokoine aliamini kila mmoja anaweza kuwa na maendeleo endapo atajituma katika kilimo na mahali alipo pamoja na pia, mtu anaweza kujitegemea akiwa ni mpenda mabadiliko katika nchi na mwaminifu. Profesa Chibunda anafahamisha kuwa, kumbukizi ya mwaka 2019 inabeba ujumbe isemayo: “Uzalishaji wa Kilimo na Viwanda kwa Maendeleo ya Tanzania: Mambo ya Kujifunza kwa Sokoine na Matarajio ya Siku zijazo.” Anasema maadhimisho haya yanayofikia kelele chake leo Aprili 12, yanajumuisha shughuli mbalimbali yakiwamo maonesho ya teknolojia za kilimo, mifugo na misitu.

Pia, kuna mawasilisho ya mada za kilimo na mifuko zinazotolewa na wanataaluma na wadau wa sekta binafsi za kilimo na viwanda. “Katika wiki hii shauku kubwa ya watu ni kuona chuo kikuu hiki kinakuwa na onesho la teknolojia zake mbalimbali pamoja na utafiti,” anasema Chibunda. Anasema SUA kinaonesha namna kinavyoshiriki kutoa elimu na utaalamu wake kwa wakulima ambao ni wadau wakubwa katika uzalishaji wa mazao mengi na bora ili kukidhi mahitaji ya malighafi itakayotumika katika sekta ya viwanda.

Kutokana na kuridhishwa na namna Taifa linavyomwenzi Sokoine, mtoto wa Sokoine; Namelok Sokoine anasema kwa niaba ya familia ya marehemu Sokoine kuwa, wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuwaenzi kwa vitendo waasisi wa Taifa la Tanzania. “Tunafarijika kuona kwamba yale yote aliyoyaamini na kuyasimamia Sokoine hivi sasa yanatekelezwa kwa kasi zaidi na ufanisi wa hali ya juu na Serikali inayoongozwa Rais Dk John Magufuli,” anasema Namelok Anasema familia ya marehemu Sokoine inaunga mkono kwa dhati juhudi zinazofanywa na serikali iliyopo madarakani na inaamini kuwa, Tanzania yenye neema inakuja. Sokoine alizaliwa Agosti 1, 1938 katika Wilaya ya Maasai Land inayofahamika kama Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Alifariki dunia katika eneo la Kijiji cha Wami Ruhindo (Wami- Dakawa), Barabara Kuu ya Dodoma – Morogoro takriban kilometa 40 kabla ya kufika mjini Morogoro kutokea Dodoma baada ya kufunga kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati huo, eneo la Kijiji cha Wami Ruhindo lilikuwa sehemu ya Wilaya ya Morogoro kabla ya kuanzishwa wilaya mpya ya Mvomero mwaka 2002. Wananchi mbalimbali wakiwamo wa Morogoro wanasema Sokoine hatasaulika kutokana na utendaji wake wa kazi uliotukuka wa kulinda maslahi ya taifa na kupingania haki za wanyonge.

Wamemweleza alikuwa ni mtetezi wa haki za wanyonge na waliowengi alipambana na wahujumu uchumi wakati walipotaka kulichezea Taifa kwa kuficha bidhaa muhimu na adimu ili waje wazilangue kwa kuuza kwa bei kubwa. Sokoine alianzisha mara moja mapambano ya nyumba kwa nyumba kwenda kuwafichua na kukamata bidhaa walizozificha, wahujumu uchumi.

Pia katika uongozi wake, anakumbukwa kwa kuanzisha mapambano dhidi ya majangili na wavamizi wa misitu walioshughulikiwa kutokana na wao kushiriki kuunguza miti na misitu kitendo kilichohatarisha taifa kuingia kwenye jangwa. Sokoine alichukizwa na watu waliotaka kuchezea, rasilimali, utajiri na hadhi ya Watanzania na akasimamia zinatungwa sheria zinazowabana husika wakiwamo wanaoharibu mazingira. Sokoine alikuwa kiongozi wa mfano aliyekataa kujilimbikizia mali bali alikubali kupunguza mali zake ili aweze kuwatumikia vyema Watanzania.

Ataendelea kukumbukwa na Watanzania kutokana na uzalendo, ushujaa na nia yake ya dhati ya ujenzi wa Taifa hili, na alikuwa kiongozi wa mfano aliyesimamia imara kutetea haki za wanyonge. Miongoni mwa mambo wanayorejea kumkumbuka wanasema ni pamoja na kujitoa kwake kutetea wanyonge wakiwamo maskini kwa kuanzisha huduma za usafiri wa magari ya abiria ya watu binafsi aliyojulikana kwa jina la ‘chai maharage’ yaliyowakomboa wengi wakiwamo wanafunzi na wafanyakazi baada ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) kulemewa.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi