loader
Picha

Wamudu kugeuza taka za plastiki kuwa matofali

UTUNZAJI wa mazingira ni jambo linalopigiwa chapuo sana, kwani lina uhusiano mkubwa na maendeleo ya watu. Mabadiliko ya tabianchi, kupungua kwa mvua na hata uzalishaji duni wa mazao unatajwa kuchangiwa na uharibifu wa mazingira.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mazingira ya mwaka 2017 (National Environment Statistics Report, 2017 - NESR), Jiji la Dar lilikuwa linazalisha taka ngumu tani takribani 4,600 kwa siku. Inakadiriwa kwamba kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kibinadamu, jiji hilo litakuwa linazalisha tani 12,000 kwa siku ifikapo mwaka 2025. Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi sana Afrika na kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, jiji hilo lilikuwa na watu wapatao milioni 4.3.

Moja ya taka zinazozalishwa kwa wingi katika jiji hilo ni zinazotokana na plastiki za aina mbalimbali ikiwemo mifuko na chupa. Baadhi ya athari za mazingira zinazosababishwa na taka za plastiki ni pamoja na kusababisha mitaro kuziba na hivyo kuleta mafuriko na kuharibu ubora na rutuba ya ardhi kwa kuwa mifuko mingi ya plastiki inapozikwa ardhini haiozi haraka.

Mifuko hiyo na chupa za plastiki vimekuwa pia na athari kwa viumbe wa majini pale vinapoingia kwenye bahari, mito au maziwa. Lakini matumizi ya vyombo vya plastiki kwa kufungia chakula cha moto yamekuwa pia yakielezwa kuwa na athari mbalimbali za kiafya kwa walaji kutokana na joto la chakuka kufanya plastiki (mifuko, mabakuli na hata vikombe) kutoa sumu inayoaminika kuwa chanzo cha matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo saratani.

Ni kutokana na madhara ya mifuko ya plastiki, wiki hii serikali imeweka wazi kwamba matumizi ya mifuko ya plastiki mwisho ni mwezi Juni mwaka huu. Je, serikali inafanya nini kuhusu chupa za plastiki? Wakati hali ikiwa hivyo, Abdallah Nyambi (26), mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Kampala, kampasi ya Dar es Salaam, anayesomea shahada ya Sayansi ya Kompyuta amekuwa miongoni mwa wale wanaogeuza taka kuwa pesa. Taka ambazo amekuwa akizilenga kwa kushirikiana na wenzake wanane ni za chupa za plastiki ambapo amefanikiwa kuzigeuza na kuweza kutumika kama matofali yanayofaa kutandikwa maeneo ya watu kupita (pavements).

Katika msimulizi yake, Abdallah anasema mwishoni mwa mwaka 2018, alikutana na Liberatha Kawamala (24) katika maonesho yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa, ambapo bidhaa mbalimbali zikiwepo za mapambo yatokanayo na chupa za plastiki zilikuwa zikioneshwa. Maonesho hayo ndiyo yaliwafanya wawili hawa kuungana na kuamua kufanya kazi pamoja ili kufikia lengo lao la kutengeneza ajira kwao na kwa vijana huku pia wakipambana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mabaki ya bidhaa za plastiki.

Muungano huo ulizaa Kampuni yao iitwayo Plastic Recycle and Youth Organization (PREYO), yenye wasichana wawili na wavulana saba ambapo pamoja na kugeuza taka kuwa pesa wanasema wamekuwa pia wakitoa elimu kwa vijana juu ya utunzaji wa mazingira. Siku nilipotembelea eneo wanalofanyia kazi, Gogo la Mboto, nilimkuta Abdallah akiwa amevalia kaptura ya rangi nyekundu na shati ya rangi ya chungwa huku akiwa ameweka kifuniko (mask) kwenye pua. Hakuwa peke yake bali alikuwa wenzake anaoshirikiana nao katika kazi hiyo.

Miongoni mwao walikuwa wakikusanya chupa za plastiki, wengine wakiandaa moto huku wengine wakikusanya mchanga. Nikaona wanamimina chupa za plastiki kwenye pipa, moto ukachochewa na chupa zikawa zinayeyuka taratibu. Hakika halikuwa zoezi dogo kwani nilishuhudia moshi mzito ukipanda angani. Kisha nikamwona Abdallah akichanganya mchanga na ujiuji wa chupa kwenye pipa, tayari kutengeneza matofali madogo. Baada ya muda nikayaona matofali yenyewe.

Anasema kwa siku wana uwezo wa kuzalisha matofali 25 na anasema ni matofali imara, yanayotumia mchanga kidogo, plastiki nyingi na yasiyopitisha maji, Changamoto kubwa ya uzalishaji wa tofali hizo ni ukosefu wa mitambo ya kisasa ya uzalishaji, ambayo itaweza kuyeyusha chupa bila kutoa moshi ambao anaamini si kitu kizuri pia kwa mazingira. Anasema moshi huo, pamoja na kuvaa mask wakati wa uzalishaji, unaweza ukawa unahatarisha afya zao pamoja na ajamii inayowazunguka.

Kuhusu matarajio ya kikundi, Abdallah anasema ni kupata mtambo wa aina hiyo na pia kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu taka za plastiki. Liberatha anasema utunzaji wa mazingira ni wito ulio moyoni mwake na ndio maana ameamua kuacha taaluma yake aliyosomea na kujikita katika mambo yanayookoa mazingira. “Nimesomea masuala ya itifaki na usafirishaji (Logistics and Transportation) lakini moyo ukanipeleka kwenye mazingira. Watu wengi huniuliza kwa nini unapenda na hata kufundisha masuala ya mazingira wakati umesomea mambo mengine. Huwa nawa-kitu fulani, ni vizuri ukifanye hicho,” anasema Liberatha.

Anatumia sehemu kubwa ya muda wake kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira ikiwemo kufungua zaidi ya klabu 300 za mazingira katika shule za msingi jijini Dar es Salaam ambapo anafundisha umuhimu wa utunzaji wa mazingira na namna ya kukabiliana na taka za plastiki. Anasema watu wengi katika jamii yetu hawana utamaduni ya kutupa taka sehemu maalumu na hivyo hutupa taka ovyo ovyo bila kuzingatia madhara mengi wanayosababisha.

Anasema ukosefu wa mifuko ya kutenganisha taka kulingana na aina zake mathalani, karatasi, chupa, na taka zinazooza hufanya hali kuwa tete zaidi hasa kwa watu wanaofanya kazi ya ukusanyaji wa taka mitaani. “Wale waliojiajiri kukusanya chupa za plastiki, hawapiti kila siku, hivyo ni changamoto kidogo, unafanya usafi lakini unakuta una lundo la chupa za plastiki na hujui pa kuzipeleka. Nilichukua changamoto yangu kama fursa,” anasema Liberatha. Abdallah anasema kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu halafu ukajihusisha katika ukusanyaji wa chupa za plastiki mitaani ni jambo lisilo la kawaida sana.

Anasema baadhi ya watu huwachukulia waokota chupa za plastiki kama watu duni na walioshindwa maisha au hata vichaa, lakini kwa Abdallah wenzake hilo kwao ni jambo la kawaida na hawajali macho ya watu. Yeye anaona sio kama jamii haijali kabisa kuhusu mazingira, bali imekosa elimu bora kuhusu utunzaji wa mazingira. “Watu wanakosa uelewa tu. Kama tukianza kuelimisha wananchi, nafikiri wote watakuwa wanatambua kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kwa kufanya mambo ambayo ni rafiki kwa mazingira,” anaongezea.

Kwa upande wake, Liberatha anatamani kuwe na kitu cha kuwaunganisha watu wanaotunza mazingira sambamba na wanaogeuza taka kuwa pesa. “Kuna watu wengi wanajihusisha na masuala ya mazingira lakini kinachokosekana ni kitu cha kutuunganisha pamoja. Unaweza kusikia mtu fulani kwenye chombo cha habari kwamba anatengeneza matofali ya plastiki, lakini hufahamu wapi anaishi, ofisi yake ipo wapi inakuwa shida. Yaani hakuna jukwaa la kutuunganisha pamoja,” anasema Liberatha.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Goodhope Amani

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi