loader
Picha

Vivutio vya kihistoria Tabora haviakisi maendeleo yaliyopo

NIMEISHI na kusoma mkoani Tabora, hasa katika wilaya za Nzega, Igunga na Tabora Mjini, hivyo natambua kuwa Tabora ni mkoa uliobeba historia kubwa sana ya nchi hii. Unapozungumzia historia ya uhuru wa Tanganyika huwezi kuacha kuutaja mkoa wa Tabora, hasa unapokitaja chama kilicholeta uhuru wa nchi hii (TANU).

Tabora ni miongoni mwa mikoa mikubwa zaidi na yenye vivutio vingi sana vya kihistoria, kama makumbusho ya Kwihala, makumbusho ya Mtemi Mirambo, Ngome ya Wajerumani, Ikulu ya Mtemi Isike, vyumba vilivyotumika kwa ajili ya watumwa na minyororo ya kufungia watumwa shingoni. Kuna maandishi yaliyoandikwa na mmisionari na mvumbuzi, Dk David Livingstone, viatu vyake na kiti alichokalia, na kuna kaburi lake pembeni.

Ikumbukwe kuwa Dk Livingstone alizikwa mara mbili, sehemu ya mwili ilizikwa hapo na nyingine Kigoma. Pia kuna misitu mikubwa ya asili, milima na mabonde yenye kuvutia, mito mbalimbali na bila kusahau ukiwa wilayani Sikonge kuna kaburi la mchungaji wa kwanza wa Kinyamwezi wa Kanisa la Moravian.

Na pia utapata kuona Kanisa la pili la Moravian lililojengwa miaka ya 1897 na linatumika mpaka leo. Lingine linalopatikana Tabora ni uwepo wa uwanja wa Isike, eneo ambalo Warugaruga (askari wa Kinyamwezi) walipambana na Wajerumani wakiwa chini ya utawala wa Mtemi Isike, wakitumia upinde na mshale dhidi ya bunduki. Ukiwa mkoani Tabora unaweza kufika kwenye wilaya zenye historia na vivutio vya utalii kama Sikonge, Uyui, Urambo, Nzega, Kaliua, Igunga na hata Manispaa ya Tabora.

Pia utalii wa kiutamaduni unapatikana sana mkoani Tabora, hasa kwa makabila ya Wanyamwezi na Wasukuma, na hivyo kuufanya mkoa wa Tabora kuwa wenye urithi mwingi wa Tanzania kwani maandiko haya ni sehemu tu ya historia ya Tabora. Ukiacha makabila ya Wanyamwezi na Wasukuma yanayopatikana mkoani Tabora pia yapo makabila mengine kama Waha, Wamanyema, Watutsi na watu wa makabila mengine waliohamia au kwenda Tabora kikazi.

Tabora ina neema nyingi sana kama asali, na wakazi wa mkoa huu wanalima sana tumbaku, karanga na mazao mengi ya chakula na biashara. Tatizo kubwa la wakulima wa Tabora imekuwa ni soko kwani wengi wa wakulima hujikuta wanadhulumiwa na wafanyabiashara wajanja ambao hununua mazao yao kwa bei ya kutupa kutokana na ufahamu mdogo na soko kuwa gumu.

Pia kuna wafugaji ambao hufuga kama sehemu ya biashara na utamaduni. Wakazi wa Tabora hupendelea sana vyakula kama viazi, wali na ugali huku wakitumia sana karanga kama sehemu ya kiungo muhimu cha mboga. Hali ya hewa katika mkoa huu ni nzuri, kuna joto kiasi kipindi cha kiangazi na hali ya ubaridi kipindi cha masika. Historia ya mkoa huu inaonesha kuwa wakati Waarabu wanafika katika mji wa Tabora miaka ya 1830 walikuta mji huo umeendelea, hasa katika maeneo ya Kwihala na Itetemya.

Na hii ni kwa sababu maeneo hayo yalikuwa yana idadi kubwa ya watu. Kwihala ilikuwa ndiyo eneo maalumu la kufanya manunuzi (shopping center). Uwepo wa nyumba za tope zilizoezekwa kwa makuti ulikuwa utamaduni asilia na hizo nyumba za tembe au misonge ndiyo ilikuwa mji wa kwanza, kama ilivyo kwa Mji wa Kilwa. Inasemwa kuwa Waarabu hawakuwa na mpango wa kukaa hapo, ila kwa kuwa walilazimishwa kutoa kodi, ndipo walipoanzisha vita na mwisho kuchukua baadbhi ya maeneo ambayo walijenga nyumba ya tembe ambayo ipo Tabora mpaka leo.

Na mara baada ya Waarabu kukaa Tabora, kuliibuka baadhi ya Waarabu ambao waliokuwa maarufu sana kama Kazeh, ambaye alimwakilisha Sultani wa Zanzibar na alitokea kuheshimiwa sana na wakazi wa Tabora. Kazeh alikuwa anaishi katika eneo la mwinuko kiasi cha kwamba ukitokea njia yoyote kama ndiyo unaanza kuingia Tabora Mjini ilikuwa lazima upaone hata ukiwa mbali.

Eneo hilo likajulikana kama Kazeh Hill, na hilo lilikuja kwa sababu hapo ndipo kuna tangi la maji ambalo lilitengenezwa kwa ajili ya Tabora School ambayo sasa inajulikana kama Sekondari ya Wavulana ya Tabora (Tabora Boys), ambayo enzi hizo ilikuwa sehemu ya kuandalia wanajeshi wa Tanganyika. Hivyo, mji wa Tabora ukafahamika kama Kazeh kulingana na ujio wa wageni hao.

Lakini kwa kuwa utamaduni wa wenyeji kwa wakati ule na hata sasa, ulitegemea sana kilimo cha viazi vitamu, ambavyo baada ya kuvunwa huanikwa juani ili vinyauke kidogo na kuchemshwa kisha kukatwa vipande na kukaushwa juani. Zao litakalopatikana baada ya mchakato huo linajulikana kwa Kinyamwezi kama matoborwa. Hivyo, muingiliano wa Wanyamwezi, Waarabu na wageni wengine ndiyo ulioleta ugeuzi wa matamshi hayo kutoka “matoborwa” na kuwa matabora, neno lililozaa jina la Tabora.

Pia maeneo hayo ndipo ilipo ikulu ya Chifu Fundikila, eneo ambalo sasa hivi limekuwa pembeni kidogo ya mji kwa sababu ya zile nadharia za ongezeko la watu na maendeleo. Pia kuna gereza la watumwa ambalo ndiyo kubwa kwa Tabora na huenda kwa Kanda ya Magharibi, ambalo kwa sasa ni ofisi za Jeshi la Wananchni (JWTZ), Brigedi ya Faru.

Hata hivyo, ukizungumzia historia ya Tabora na maendeleo yaliyopo ni vitu viwili tofauti. Pamoja na uwepo wa historia nzuri, mkoa huu umeshindwa kuwa na makumbusho maalumu ya mambo ya kale (kama ilivyo makumbusho ya Bujora jijini Mwanza) ambayo ingeweza kuwa chachu ya maendeleo, kwa vile makumbusho yana mchango mkubwa katika maisha ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Makumbusho ni maeneo maalumu ambapo historia ya kale huhifadhiwa. Lakini je, watu wanatambua umuhimu wa makumbusho? Je, wanayathamini makumbusho kwa kiwango gani? Wageni wafikao Tabora wangependa kuona makumbusho ya Mtemi Mirambo, iliyosheheni utajiri mkubwa wa vitu vyake ambavyo vimepotelea kwingine.

Mtemi Mirambo alikuwa miongoni mwa viongozi walioheshimika sana na waliokuwa na majina makubwa ndani na nje ya nchi na mtemi huyo alifariki mwaka 1884. Kwa kutumia umaarufu wake na kumuenzi kwa kujenga makumbusho yake ingeweza kuwa kivutio kikubwa na watu wengi kupenda kwenda kuona alipokuwa anaishi, na hivyo kuongeza chanzo cha mapato.

Eneo la makumbusho ya mtemi huyo lipo katika eneo la Kijiji cha Usigala, barabara ya 44 katika Jimbo la Ulyankulu. Makumbusho mengine ya mtemi huyo yaliyopo katika eneo la Ikonongo hayana sifa, yanatakiwa kuboreshwa ili yalingane na hadhi ya Mtemi Mirambo tofauti na ilivyo sasa. Nadhani ni hali hii ndiyo iliyoufanya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, mapema mwaka jana, kufikiria kuboresha makazi yaliyokuwa ya Mtemi Mirambo kwa ajili kuvutia wageni kutembelea eneo hilo, ili kutalii na kufanya tafiti mbalimbali, na hivyo kuwa chanzo kingine mapato yake na wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dk John Pima alibainisha wakati akijibu hoja mbalimbali za madiwani waliotaka kujua mpango wa kuboresha eneo hilo kwenye mkutano maalumu wa kupitisha mpango wa bajeti ya 2018/19. Awali Diwani wa Kata ya Ilege, Masanja Lufungija alisema kuwa halmashauri hiyo imekuwa ikikosa mapato kutokana na kutoboreshwa kwa makazi wa Mtemi Mirambo na kuthamini umuhimu wa eneo hilo.

Alisema kuwa kila wiki wageni kutoka maeneo mbalimbali wakiwemo wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi wamekuwa wakitembelea eneo hilo lakini hakuna kitu ambacho halmashauri inaingiza kutokana na uwepo wa wageni hao. Naye Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, eneo asili la makazi ya Mtemi Mirambo, John Kadutu alisema kuwa eneo hilo ni vema likaboreshwa kwa kujenga hata nyumba kwa ajili ya wageni kupata huduma mbalimbali wakati wanatembelea eneo hilo ili kusaidia kuongeza mapato katika Halmashauri ya Kaliua.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi