loader
Picha

Ndugai- CAG kajieleze kwa Magufuli

SAKATA kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali,(CAG), Profesa Mussa Assad limechukua sura mpya baada ya Spika kumtaka CAG ajipime kama anastahili kuendelea kushikilia wadhifa huo.

Hoja hiyo ya Ndugai imekuja, ikiwa ni siku kadhaa baada ya CAG kusisitiza msimamo wake kuwa ataendelea kutumia neno dhaifu kama kipimo chake cha kupima utendaji wa Bunge.

Neno hili ndilo CAG alilitumia dhidi ya Bunge wakati akihojiwa na mwandishi wa habari nchini Marekani na kusababisha tafrani kubwa baina yake na Bunge.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Bunge wa kufanyia kazi ripoti za hesabu ya CAG ya mwaka 2018-19 pamoja na msisitizo huo wa CAG wa kuwa ataendelea kulitumia neno dhaifu, Spika Ndugai alimtaka CAG kutambua kuwa kwa uamuzi wake wa kuendelea kutumia neno hilo ni sawa na kumtukana Rais John Magufuli pia na Baraza lake la Mawaziri.

Alisema, kwa kuwa Bunge hilo analolitukana linafanya kazi kwa ukaribu zaidi na Rais Magufuli aliyemteua yeye CAG kushika wadhifa huo, hiyo ni sawa na anamtukana Rais Magufuli pamoja na baraza lake la mawaziri ambalo linaundwa na wabunge ambao nao wamejumuishwa kwenye kauli hiyo ya CAG kuwa ni dhaifu.

Alisema,”yaani huyu anamtukana mtu anayempa kula, kwanza anaonekana ni Profesa ambaye anajua jumlisha na kutoa tu na sio kujua hata kuwa akitukana Bunge ni sawa na kuwa anamtukana mwajiri wake, sasa ninamshauri tu akajipime na kuona kama anastahili kuendelea kushika hiyo nafasi bado na kwanza anapaswa kwenda kujieleza kwa Rais Magufuli.”

Aliwataka wananchi kujua kuwa yeye hana ugomvi wala chuki na CAG ila anamtaka kuliheshimu Bunge na kutambua kuwa ni chombo kinachoundwa na wawakilishi wa wananchi na hivyo hapaswi kulizungumzia vibaya.

Alimkanya kuwa asiendelee kutumia neno dhaifu kwenye ufafanuzi wake wa shughuli za Bunge na kuwa kama akiendelea ataitwa tena bungeni na safari hii kitakachomtokea kinaweza kuwa kibaya zaidi.

Alisema kuwa licha ya CAG kuliudhi bunge, lakini bado bunge hilo litaendelea kufanya kazi na ofisi yake kwa maana ya wafanyakazi wa ofisi ya CAG huku akibainisha kuwa madudu yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo sio kwamba ni kweli kila kitu kimetokea.

Alisema baada ya Bunge kupokea ripoti hiyo kutokea kwa watendaji wa Rais Magufuli inakuwa ni jukumu la Kamati za Bunge hasa ya Hesabu za Serikali na ya Serikali ya Mitaa kukaa na kuwaita wale waliotajwa kufuja fedha ili kuwasikiliza.

Alisema kwa upande wake kamati hizo kutakuwa na wanasheria na wahasibu wa bunge ambao nao watasaidiana na kamati hizo kufuatilia kwa undani kuhusiana na majibu kutokea kwa taasisi za serikali zitakazokuwa zimetajwa kufuja fedha hizo kama ilivyoelekezwa kwenye ripoti ya CAG.

“Hii imekuwa ikifanyika hivyo sio tu kwa Tanzania ila ni kwa nchi zote za Jumuiya ya Madola, kuwa ikishakabidhiwa ripoti basi wahusika waliotuhumiwa wanaitwa kujieleza kwa undani zaidi ili kusikiliza upande wao, sasa kama watakuwa ni kweli wamehusika basi Bunge linaielekeza serikali nini cha kufanya,” alifafanua Spika Ndugai.

Aliongeza kuwa kama serikali ikishindwa kufanyia kazi basi inapaswa CAG kuilalamikia na si kukwepa na kupeleka lawama kwa Bunge, pia alisisitiza kuwa hatua za kutumbuliwa kwa baadhi ya watendaji wa serikali kutokana na ubadhirifu ni moja kati ya matokeo ya ushauri wa bunge hilo.

Alisema kuwa serikali hii ndio imeongoza kwa kufanyia vema kazi ushauri wa bunge kuliko serikali yoyote ile kwa kuwa kila wanachopendekeza kutokana na kile walichokichuja kwenye ripoti ya CAG kinafanyiwa kazi na hakuna udhaifu katika hilo.

“Ninasisitiza kuwa aache kutumia jina baya dhidi yetu wabunge kama anaona jina hilo zuri si ajiite yeye sisi hatulitaki na sio uungwana kuwatolea maneno mabaya watu wazima ambao wamesema hawataki,” amesema Spika Ndugai.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi