loader
Picha

Mawaziri 7 kufa au kupona

AHADI saba za mawaziri waliokuwa katika ziara ya Rais John Magufuli mkoani Njombe, zinaanza kutekelezwa leo kadri ya muda uliowekwa kwa kila ahadi kwa mradi husika.

Miongoni mwa mawaziri waliokuwamo kwenye ziara hiyo ambao walimpa Rais Magufuli ahadi ya kukamilika kwa miradi yao au utoaji wa vibali vya miradi ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa Barabara ya Njombe-Makete yenye urefu wa kilomita 107 kwa gharama ya Sh bilioni 224, Waziri Kamwelwe alimweleza Rais kuwa kibali cha mazingira kwa ajili ya kununua makaa ya mawe kilichoombwa na serikali ya India na China, kitatoka leo.

Kamwelwe alisema India na China zimeahidi kila moja kununua tani laki sita za makaa ya mawe kutoka mkoani Ruvuma, lakini kilichokuwa kinachelewesha ni kibali kutoka kwa watu wa mazingira. Ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na biashara hiyo, alisema kibali hicho kitatoka Jumatatu yaani leo.

“Mauzo ya bidhaa nje kwa nchi yetu ni madogo, hivyo kwa kutoa kibali hicho tutaongeza kiasi cha bidhaa zetu kuuzwa nje kwa kuwa sisi ni wazalishaji wazuri,” alieleza Kamwelwe.

Katika kuhakikisha uwekezaji wa viwanda unashika kasi, Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda, alisema kuwa mwekezaji wa kiwanda cha kutengeneza mafuta ya parachichi, atapewa kibali kwa ajili ya uwekezaji huo mwezi ujao.

Alisema Njombe ni moja ya mikoa inayozalisha parachichi kwa wingi na parachichi zao zina ubora wa hali juu, hivyo kuja kwa kiwanda hicho kutatoa fursa kwa wakulima wa zao hilo kuuza parachichi zao kiwandani hapo.

Mbali na mawaziri hao, waziri mwingine aliyetoa ahadi ya mradi anaousimamia kwa Rais Magufuli, ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Kwa kuzingatia umuhimu wa afya kwa wananchi wa Njombe, Waziri Ummy alisema kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 96, itaanza rasmi kutoa huduma ifikapo Julai mosi, mwaka huu.

Aidha, katika kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa, alisema wizara yake itahakikisha vifaa na vifaa tiba vinawekwa, kukamilisha usajili wa hospitali pamoja na kufunga mifumo ya kutolea taarifa, jambo jingine ni ujenzi wa nyumba 10 za watumishi wa hospitali hiyo.

“Awamu ya kwanza inajumuisha ujenzi wa jengo la huduma la wagonjwa wa nje (OPD) lililobeba huduma zote muhimu zinazohitajika ikiwemo uchunguzi, maabara, mionzi ya x-ray, ultrasound, upasuaji wa kibingwa, pua, masikio, macho, meno, kinywa na magonjwa ya wanawake na watoto,” alieleza Waziri Ummy.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, amesema kupitia ufadhili wa serikali ya India wa Sh bilioni 32.2, utasaidia kutatua tatizo la maji katika mji wa Njombe kwa asilimia 100 na mkandarasi atakuwa eneo la ujenzi ifikapo Septemba, 2019.

Profesa Mbarawa alisema upatikanaji wa maji katika mji huo kwa sasa ni asilimia 67.2, lakini pia kuna miradi mitano ya maji inayotekelezwa kwenye mji huo kwa gharama ya Sh bilioni 12.8.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, aliahidi kuwa ifikapo Juni, 2021, wananchi wote wa Njombe watakuwa wamepata umeme. Alisema kwa sasa mitaa na vijiji 32 mkoani humo vinapelekewa umeme na usambazaji unaendelea.

Baada ya ahadi hizo za mawaziri, Rais Magufuli alijibu kwa kifupi kuwa ahadi ni deni.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi