loader
Picha

Mwendokasi 300 kutumia gesi

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea na majadiliano na wateja wa gesi, ikiwamo DART ili magari zaidi 300 ya mwendokasi yatumie gesi asilia.

Mpaka sasa kuna kituo kimoja cha kujazia gesi kwenye magari na zaidi ya magari 200 yanatumia nishati hiyo.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Kapuulya Musomba alipokuwa akizungumzia mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mradi wa gesi iliyoshindiliwa (CNG) mkoani Dar es Salaam.

Musomba alikuwa akiwasilisha mada ya kuhusu shughuli za uendelezaji wa mafuta na gesi asilia chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwenye semina ya siku mbili ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Alisema katika kutekeleza mradi wa CNG Dar es Salaam ambao unatarajia kugharimu Sh bilioni 5.7, kwa sasa TPDC inafanya mazungumzo na DART na Kairuki ili kuweza kuwaunganisha na gesi asilia.

"Mazungumzo yetu na DART yanaendelea vizuri, tunataka mabasi zaidi ya 300 ya mwendokasi ambayo yanatarajiwa kuingizwa nchini yatumie gesi asilia, na hii imeonekana kuwa itawasaidia kupunguza gharama za mafuta kwa wastani wa asilimia 40," alisema.

Kuhusu mradi wa kuunganisha gesi asilia majumbani, Musomba alisema kwa mkoa wa Dar es Salaam tayari nyumba 96 zinatuma gesi asilia na kwa sasa ujenzi unaendelea kwa eneo la Mlalakuwa na Chuo Kikuu ambapo jumla ya kilomita 1.8 za bomba zimefukiwa.

"Lengo ni kufikia jumla ya nyumba 212 kwa Mkoa wa Dar es Salaam ifikapo Juni mwaka huu, na kwa upande wa Mkoa wa Mtwara vibali vyote vya wilaya, mkoa na serikali za mitaa na vijiji zimepatikana na lengo letu kuunganisha nyumba 125 na taasisi nne.

Awali, akiwasilisha mada ya udhibiti wa shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asili chini ya Mamlaka ya Uthibiti wa Mkondo wa juu wa Petroli (PURA), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Sangweni alisema mpaka sasa eneo kubwa lenye mafuta au gesi asilia bado haijafanyiwa utafiti.

"Hadi sasa maeneo ambayo yamefanyiwa tafiti ni kiasi cha kilomita za mraba 534,000.

Alisema pia mchango wa sekta ya mafuta na gesi katika Pato Ghafi la Taifa (DGP) limendelea kuongezeka kutoka asilimia 1.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 1.9 mwaka 2017 na pia kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa gesi asili kutoka futi za ujazo bilioni 50,851 kwa mwaka 2017 hadi kufikia futi za ujazo 59,096 kwa mwaka 2018.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi