loader
Picha

Maambukizi Ukimwi yapungua

MAAMBUKIZI ya ugonjwa wa Ukimwi nchini yameshuka au kupungua kutoka asilimia 5.1 ya mwaka 2012 hadi asilimia 4.7 katika mwaka 2016/17. Matokeo ya mwaka 2016/17 yanaonesha maambukizi ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 4.7, wanawake ni asilimia 4.7 na wanaume ni asilimia 3.1.

Kwa upande wa Zanzibar, maambukizi ni chini ya asilimia moja. Takwimu hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Uratibu, Bunge, Sera, Ajira, Kazi, Vijana na watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, kwenye uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi wa mwaka 2016/17.

Mhagama alisema kwa mujibu wa takwimu hizo, maambukizi mapya ya VVU yamepungua kutoka watu 80,000 mwaka 2012 hadi kufikia watu 72,000 mwaka 2017.

“Takwimu zinaonesha kupungua kwa viwango vya vifo vinavyotokana na Ukimwi kutoka watu 70,000 kwa mwaka katika mwaka 2010, hadi kufikia vifo 32,000 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2017,” alisema Mhagama.

Mhagama alisema maambukizi kwa vijana wenye umri wa miaka 15 – 24 ni asilimia 1.4 (wasichana ni asilimia 2.1 na wavulana ni asilimia 0.6).

“Utafiti huu unaonesha kuwa, maambukizi kwa vijana wa kike yako juu zaidi kuliko vijana wa kiume hasa kwenye umri wa miaka 15–34.”

“Natoa mwito kwa Taasisi ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) na wadau wote wa mapambano dhidi ya Ukimwi kuendelea kuweka mikakati na kusimamia utekelezaji wa afua za Ukimwi kwa vijana kwa msisitizo mkubwa zaidi,” alisema.

Aidha, matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa asilimia 53 ya wakazi wa maeneo ya mijini hawafahamu hali zao (kupima) na wale wa maeneo ya vijijini ni asilimia 55.8.

Kati ya wakazi wa mijini waliofahamu hali zao, waliokuwa wakitumia dawa ni chini ya asilimia 50 na vijijini ni asilimia 37.

Mhagama alisema mikoa inayoongoza kwa maambukizi ni Njombe asilimia 11.6, Iringa (11.2), Mbeya (9.2) na Kagera (6.8). Aidha, mikoa minne yenye maambukizi kidogo ni Lindi asilimia 0.3, Manyara (1.8), Arusha – (1.9) na Mtwara (2.1).

Alisema bila shaka viongozi wa mikoa husika yenye maambukizi makubwa na taasisi zinazojihusisha na kudhibiti Ukimwi bado wanayo mambo mengi ya kujifunza, kutafiti na kuibua afua mpya zitakazosaidia kupunguza maambukizi mapya.

Awali, akizungumza Mkurugenzi Mtendaji Tacaids, Dk Leonard Maboko alisema matokeo ya utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi (THIS) wa mwaka 2016/17 yanatokana na utafiti uliofanyika katika ngazi ya kaya kuanzia Oktoba, mwaka 2016 hadi Agosti, 2017 lengo likiwa ni kufahamu hali ya mwitikio wa Ukimwi nchini.

“Utafiti ulihoji kaya 14, 811 zilizojumuisha watu zaidi ya 31,000 wenye umri wa miaka 15 na zaidi na watoto zaidi ya 9,000 wenye umri wa miaka 0-14,” alisema.

Dk Maboko alisema utafiti umeonesha kiwango ni asilimia 60.9 tu ya watu wanaoishi na VVU ndio wanafahamu hali zao.

Kati ya wanaofahamu hali zao asilimia 93.6 ndio wanaopatiwa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV) ambapo miongoni mwao ni asilimia 87.0 virusi vyao vimefubaa.

Awali, akizungumza Kaimu Mtakwimu Mkuu kutoka NBS, Andrew Ulindula alisema utafiti unafanyika kila baada ya miaka minne na huu wa mwaka 2016/17 ni wanne, wa kwanza ulifanyika mwaka 2003/04, mwingine 2007/08 na mwingine 2011/12.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi