loader
Picha

TPA yapongezwa ongezeko la shehena

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imepongezwa kwa kuongeza shehena kutoka tani milioni 14 kwa mwaka hadi kufikia tani milioni 15 sambamba na kuwa shirika linaloongoza kwa kutoa gawio kwa serikali.

Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Francis Michael, wakati anafungua Mkutano wa Baraza Kuu la wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Alisema anaamini TPA ambayo yeye aliwahi kuwa mmoja wa wajumbe wa bodi yake miaka ya nyuma, itaendelea kufanya vizuri katika kuhakikisha inapata wateja wengi zaidi na hivyo kuongeza shehena.

Aliipongeza pia TPA kwa kufanikisha Mkutano wa huo wa Baraza ambao alisema ni chombo muhimu cha ushauri na kutatua matatizo ya wafanyakazi pamoja na kupanga bajeti ya mamlaka.

Akizungumzia kipengele cha mishahara, Naibu Katibu Mkuu alikiri kwamba mishahara ya watumishi wengi wakiwemo wa bandari bado midogo lakini akasema mchakato unaendelea wa kuboresha mishahara ya taasisi za umma.

Alisema hatua hiyo ikimalizika na vyombo vyote husika kupitisha mapendekezo yaliyofanywa na timu maalumu ya wataalamu, mishahara katika sekta ya umma itaongezwa.

Alisema kuna changamoto ya tofauti kubwa ya mishahara ya wakurugenzi kutoka shirika au taasisi moja ya umma kwenda nyingine na baina ya wakurugenzi na wafanyakazi wengine.

“Kima cha chini hakina tatizo isipokuwa hapo katikati ndipo kwenye tatizo,” alisema na kuongeza kwamba lengo ni kuona mishahara inakuwa na uwiano mzuri kuliko ilivyo sasa.

Mapema, Mkurugenzi wa shirika hilo, Deusdedit Kakoko, alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita shehena imeongezeka kwa asilimia 4.4.

Alisema baadhi ya mambo waliojipangia kama vile mapato na matumizi, mafunzo, ununuzi wa vifaa, miradi ya maendeleo na ulinzi na usalama wamefanikiwa kati ya asilimia 48 hadi 93 katika kipindi cha miezi sita.

“Tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini bado kuna udhaifu na changamoto kadhaa,” alisema na kuongeza kwamba changamoto mojawapo ni ya barabara kutofika mahala shehena zinapopelekwa.

Aliiomba serika kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu, kuona uwezekano wa kuharakisha ongezeko la mishahara ya watumishi wa bandari, huku ikizingatia kwamba wamekuwa wakiongoza kwa kutoa gawio.

Mjumbe wa Baraza hilo, Abraham Lukumay, alisoma mapendekezo 12 ya kamati ya Utendaji ya Baraza ambayo wanataka kufanyiwa kazi na menejimenti ya TPA.

Baadhi ya mambo hayo ni kuboresha maslahi ya wafanyakazi, kuziangalia kwa jicho la umakini zaidi bandari zinazofanya vizuri, hususani Bandari ya Dar es Salaam na menejimenti kuhakikisha mitambo na vifaa vinavyonunuliwa vinakuwa imara na vinavyotumia teknolojia ya kisasa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema yeyote atakayewekeza mkoani Pwani hatajuta.

Amesema ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari, Bagamoyo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi