loader
Picha

MWAJUMA MASAIGANAH: Jasiri aliyeruka kiunzi kuozwa utotoni

JUMAPILI iliyopita, nyota wetu alikuwa Mwajuma Masaiganah; mama shujaa aliyesimulia alivyopambana na kundi la majambazi waliovamia nyumbani kwake akafanikiwa kuua mmoja wao. Simulizi ya alivyojibizana kwa risasi na wahalifu hao akiwa peke yake katika kijiji cha Mlingotini, wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani inasisimua. Kupitia simulizi, historia ya mapambano yake inanzia utotoni alipopambana na mila potofu na kujikuta baba yake mzazi akimkana na kumwambia ni bora angezaliwa mwanaume. Fuatilia kisa hiki:

Mwajuma aliyezaliwa na kukulia kijijini wilayani Serengeti mkoa wa Mara, mapambano dhidi ya ndoa za utotoni kama yangekuwa yameshika kasi katika miaka ya 1960 kama ilivyo sasa, basi angepewa tuzo ya mtoto jasiri aliyemgomea baba yake kumuoza akiwa darasa la nne kama anavyosimulia: Akiwa ni mtoto wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto watano yenye wasichana watatu anasema baba yake alikuwa mhudumu wa mtawala wa jadi (Mwanangwa).

Alipoanza darasa la kwanza, ukoloni ulikuwa unaishia. Akiwa darasa la nne, baba yake alishawishika kumuoza kwa mwanakijiji mmoja. Lakini dada yake aliendelea kusoma hadi shule ya wasichana Bwiru mkoani Mwanza. “Baba aliponipeleka kunioza mimi nilikataa, lakini kimya kimya alichukua mahari kwa mtu ambaye alikuwa mjomba wetu kiukoo.

Alichukua ng’ombe 24… haya ya watoto kuozwa yapo siku nyingi,” anasema. Wakati hayo yakiendelea, alifanya mtihani wa kujiunga na shule ya kati (middle school) akafaulu kujiunga na shule ya wasichana ya Murembe lakini baba yake akakataa kumlipia ada.

“Wakati huo ada ilikuwa shilingi 240. Nikasema nifanyeje?” Alikuwapo kaka yake (mtoto wa mama yake mkubwa) aliyekuwa akifanya kazi katika machimbo ya Buhemba mkoani Mara. Alimuandikia barua kumueleza juu ya uamuzi wa baba yake kukataa kumpeleka shule. Kaka yake alimwambia kwamba ni lazima aende shule, hivyo akamtumia fedha kwa siri akaenda kuendelea na masomo. Kwa mujibu wa Mwajuma, baba yake alikasirika akamwambia kuwa si mtoto wake.

 “Nikaendelea kusoma. Nikawa nakaa shule ya bweni… ,” anasema na kuongeza kwamba kwa kuwa baba yake hakumsomesha, hakuwa na njia. Alisoma mpaka akachaguliwa kwenda sekondari ya wasichana ya Rugambwa mkoani Kagera. Wakati huo kaka yake aliyekuwa akimfadhili, alikwenda kufanya kazi Kilembe, Uganda na alimuahidi kuwa akifaulu aongozane na mama yake waende huko aliko awape fedha.

“Tuliondoka na mama (Amina Nyakiboha) tukaenda kwa meli hadi Musoma kisha Kisumu (Kenya) na baadaye tukafika Jinja (Uganda). Tuliondoka hapo kwa treni hadi Kampala. Nikaenda kutafuta ada ya kusoma,” anasema na kwamba ilikuwa mwaka 1967.

“Kwa hiyo baba alinichukia sana mpaka akanikana. Nilikuwa hata nikienda nyumbani nikiomba fedha napewa Sh 100. Nakwenda kwa mama ananiambia usilie nitakupa; akiwa ameuza pamba, mahindi ananipa fedha. Kumbuka wakati huo nikisoma, nilikuwa mke wa mtu kwa maana kuwa nilikuwa nimelipiwa mahari lakini nilikataa kuolewa,” anasema.

 Hata alipokuwa anaendelea kusoma Rugambwa, baba yake alikuwa bado anayo mahari iliyotolewa. “Bahati mbaya yule bwana akawa amefariki. Nikawa nimeokoka na nimejiokoa mwenyewe kwa kumtumia kaka. ”

 Baada ya kuanza kazi, alipata mchumba na mahari ikapelekwa kwa baba yake akaipokea. Hata hivyo, licha ya kuolewa, baba yake aliendelea kumkana. Mwajuma anasema aliishi maisha ya uchungu wa kukataliwa na mzazi. Anakumbuka katika miaka ya 1980, akiwa Dar es Salaam, baba yake aliugua ndugu zake wakamleta kwake na alihakikisha baba yake anatibiwa kisha akarudi nyumbani (Serengeti).

 Hata hivyo anasema baba yake aliendelea na msimamo wa kumkana kuwa sio binti yake. Anasema baadaye ilimbidi aende nyumbani kwani baba yake alikuwa bado anaumwa. “Nilimfuata nyumbani tukazungumza, nikamwambia baba nimekusamehe kwa kuendelea kunikana kuwa mimi si mtoto wako.” Mwajuma anasema, “ni changamoto.

Nimepata shida kidogo, sikusomeshwa na baba, nilikataliwa, niliozwa lakini kwa uelewa kwangu nikajitoa kwenye makucha ya kuolewa na mtu ambaye sikumchagua. Kwa sababu ya kupambana kwangu, ndipo baba akawa anasema bora ungekuwa mwanaume.” Anastahili nishani Simulizi hizi za maisha yake hususani tukio la kuvamiwa na majambazi Desemba 6, 2012 na kufanikiwa kuua mmoja, zinashawishi baadhi ya watu kumuona mama huyu kama mtu aliyepaswa kutuzwa kwa ujasiri.

“Hakika huyu mama ni shujaa… anastahili tuzo ya ushujaa. Kisa chake kinagusa sana…Mungu ni mwaminifu,” hizi ni sehemu ya kauli zilizotolewa na baadhi ya wasomaji wa makala yaliyopita. Baadhi wakataka kufahamu endapo aliwahi kutambuliwa rasmi kwa ujasiri kama ilivyowahi kufanyika kwa baadhi ya watu.

Wakakumbushia tuzo iliyotolewa kwa mkaanga chipsi wa jijini Dar es Salaam, Kassim Said aliyejitoa mhanga kukabili jambazi mwenye silaha aliyevamia eneo lake la biashara Julai 7, mwaka 2013. Kassim alikuwa miongoni mwa watunukiwa 28 wa nishani mbalimbali zilizotolewa mwaka 2014 na aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 53 ya Uhuru.

 “Kitendo cha mwanamke huyu kupambana na majambazi wengi hivyo wenye bunduki, hakikuwa cha kawaida. Alistahili nishani,” anasema msomaji ambaye hakutaka jina lake liandikwe. Mwanahabari Mwandamizi, Leila Sheikh anasema anamfahamu mama huyu tangu mwaka 2006. Anamuelezea kuwa ni miongoni mwa watu ambao anavutiwa nao kwa ujasiri wake kuhusu harakati za haki, jinsia na ni mwanamama mcheshi na shupavu anayepaswa kutunukiwa.

 “Hilo tukio la kuwashikisha adabu majambazi waliovamia nyumba yake Bagamoyo lilinigusa mno ndiyo nikabandika ile kanda (kwenye kundi moja la whatsapp) anayoelezea jinsi alivyopambana peke yake,” anasema Sheikh. Sheikh anasema ni watu wachache; wake kwa waume wenye ujasiri wa kupambana na majambazi wenye silaha za moto.

“Mwajuma anastahili tuzo kutoka kwa wanaharakati, wanajamii, serikali…tatizo letu, jamii imejenga taswira ya mwanamke wa nguvu lazima awe tajiri, mjasiriamali, maarufu.

 

Tunasahau wapo wanawake jasiri kama Mwajuma.” “Tunawasahau kabisa wanawake waliopo pembezoni,” anasema Sheikh na kushauri yaanzishwe majukwaa yanayothamini michango kama ya Mwajuma. Kwa upande wake Mwajuma ambaye anatamani wahusika wote wa uhalifu huo wangekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, anasema anachomshukuru Mungu ni uhai. “…ni kweli hata pongezi sikupata lakini uhai nilipata kwa Mwenyezi Mungu.” Mama huyu anayejishughulisha zaidi na jamii, anamshukuru Mungu na kujivunia kuthubutu kuonesha nguvu ya mwanamke kwa kufanya vitu vingi ambavyo jamii inadhani vinapaswa kufanywa na wanaume. Anapendelea nini? Katika kudhihirisha anavyopenda kazi za kijamii, amewekeza kwenye shule. Anamiliki shule za msingi mbili; Twibhoki ya wilayani Serengeti na Mwasama iliyoko katika kitongoji cha Ukuni, Bagamoyo.

“Nilifungua Twibhoki kulipa fadhila za wazazi. Sisi tulisomea kwenye miti tukasema hebu tujenge shule tujinyanyue ,” anafafanua jina la shule hiyo ‘Twibhoki’ ni neno la Kikurya linalomaanisha ‘tuinuane’.

Vile vile hupenda watoto hali ambayo wakati mwingine hutumia muda wake kujumuika na wanafunzi (hasa wa shule ya Mwasama anaoishi nao karibu) katika shughuli mbalimbali ikiwamo utunzaji mazingira na ufugaji ikizingatiwa pia ni mpenzi wa mazingira. “Nikikaa mahali nataka pawe pa asili,” anasema jambo ambalo mapenzi yake kwa familia yanadhihirika nyumbani kwake ambako amezungukwa na miti mbalimbali, maua ya kila aina, mazao na ndege ambao wamewekewa mazingira mazuri ya kuishi.

Ipo miti ya mianzi na zinaonekana chupa maalumu za kulishia ndege zinazowekewa maji na chakula. Mazao mbalimbali yamepandwa na kumwagiliwa kwa njia ya matone. Anafuga kuku, bata na lipo bwawa la kufugia samaki. “Watoto (wanafunzi) huwa wanawawekea ndege maji na chakula kwenye chupa,” anasema na kusisitiza umuhimu wa kujengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri baada ya kuhitimu.

 “Watoto wanakuja kujifunza kulisha kuku, wanafuga bata, najaribu kuwaweka katika hali ya kutambua kwamba shule si kitabu tu bali na vitu vingine…Najaribu kuwafundisha kwamba, enzi za mwalimu Julius Nyerere tulifundishwa elimu ya kujitegemea; inamjenga mwanafunzi kwamba hata asipoajiriwa ataendelea kujiajiri,”anasema.

 Mwajuma mwenye watoto wanne na wajukuu sita, anasema anao watoto wengi anaowalea akiwamo mmoja (mjukuu) wa kuasili. Alimchukua mtoto huyo wilayani Rombo mwaka 2004 wakati akiwa kwenye kazi za kijamii baada ya kumkuta katika mazingira magumu hali iliyomuumiza moyo. Mtoto huyo sasa yuko chuo kikuu.

Anapendelea kujisomea kuongeza maarifa. “Hata nikikaa na simu, kazi yangu ni kusoma. Hata usiku nikiingia chumbani huwa naendelea na kusoma ama vitabu au kwenye laptop (kompyuta mpakato). Hata siku aliyovamiwa na majambazi, Desemba 6, 2012 alikutwa akiangalia kipindi cha televisheni ikiwa ni sehemu ya kujiongezea maarifa.

Huyu ndiye Mwajuma; anayemshukuru Mungu kwa kumleta duniani Mei 12, 1951 na kumwezesha kuwa miongoni mwa wanawake wapambanaji na jasiri walioruka viunzi mbalimbali maishani.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Stella Nyeminochi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi