loader
Picha

'Bodaboda kateni bima ya maisha'

MADEREVA wa pikipiki maarufu bodaboda, wameshauriwa kujiunga na bima ya maisha, itakayowasaidia watakapopata ulemavu wa kudumu au kifo.

Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Acclavia, Ancelim Mushi kwenye bonanza la bodaboda, lililofanyika mwishoni mwa wiki viwanja vya Msimbazi, Dar es Salaam.

Amesema, wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri, wamekuwa wakifuatilia zaidi bima za vyombo vyao huku wakiwasahau madereva wanaovitumia.

Amesema, kampuni hiyo imetoa elimu ya masuala ya bima kwa madereva bodaboda 500 kutoka vikundi 42 vya bodaboda jijini Dar es Salaam.

Mushi alisema utafiti walioufanya, umebaini kuwa watu wengi hawana uelewa kuhusu masuala ya bima na kwamba ni asilimia chache tu ya watu walioko kwenye sekta rasmi ndio wana uelewa.

‘’Bodaboda ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, hivyo tumeona tubuni bima yenye gharama nafuu itakayowasaidia waendesha bodaboda ili iweze kuwasaidia wanapokumbana na majanga mbalimbali, ikiwemo ulemavu wa kudumu au vifo,’’ amesema Mushi.

Aliongeza kuwa bima ya maisha ambayo ni kwa ajili ya bodaboda, inatambulika kama Boda Salama na gharama yake ni Sh 56,000 kwa mwaka, ambapo itampatia fidia ya bodaboda mbili na mkono wa pole wa Sh 500,000 endapo atapata ulemavu wa kudumu.

‘’Bima hii pia itaipatia familia bodaboda mbili na Sh milioni 1.5 endapo mwendesha bodaboda atafariki dunia. Lakini iwapo mwendesha bodaboda atafiwa na mkewe bima hii itampatia mkono wa pole wa Sh milioni moja na kwa mtoto itampatia Sh 500,000.

Alieleza kuwa fidia hiyo itatolewa kwa wakati muafaka na itasaidia familia kuendeleza biashara na kusomesha watoto walioachwa.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA), Faustine Oyuke amesema, wanaendelea kuhamasisha bodaboda kujiunga kutumia huduma za bima, ambazo zitawasaidia kupata matibabu na bima za maisha.

Oyuke amesema, kama mamlaka inasimamia kuhakikisha kwamba vyombo vya moto ikiwemo pikipiki kuwa na bima na kwa madereva wake pia.

Amesema bodaboda anaposababishiwa ajali, anapaswa kuhudumiwa na mtu aliyemsababishia ajali iwe ana bima au la.

Kwamba ikiwa bodaboda ndiye aliyesababisha ajali, basi chombo chake kinatakiwa kitoe huduma kwa aliyemsababishia ajali.

Alisisitiza kuwa watu wanaotumia bima, wanatakiwa pindi wanapopata shida kutoka kwa kampuni hizo, wafike kwenye mamlaka hiyo ili iwasaidie kupata fidia zao.

Alifafanua kuwa kama mtu ana nyaraka zote muhimu na madai yake ni halali kuhusu kupata fidia anatakiwa kujibiwa na kampuni kuwa wanashughulikia madai hayo ndani ya siku 30 na katika siku 45 anatakiwa kulipwa fidia hizo.

Ofisa Habari wa Bodaboda Ilala ambao ndio waandaaji wa bonanza hilo, Abdallah Bakari amesema, Wizara ya Mambo ya Ndani imetoa kibali kwa Chama cha Maendeleo ya Madereva wa Pikipiki Tanzania (MAPIMATA), kuzunguka mikoa 26 kuhamasisha bodaboda kujiunga na bima za afya na za maisha.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi