loader
Picha

AG atoa msimamo sakata la CAG, Spika

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi amesema hawezi kufungua shauri lolote mahakamani la kuomba ufafanuzi wa kikatiba kuhusu mgogoro uliopo kati ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad uliodumu kwa takribani miezi minne sasa.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili hivi karibuni, walisema kuwa miongoni mwa watu ambao wanaweza kusaidia kupata ufumbuzi wa mgogoro huo kati ya Bunge na CAG ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Chama cha Mawakili. Miongoni mwa watu waliotoa ushauri huo ni Wakili wa Kujitegemea, Onesmo Mpinzile aliyesema kuwa kama busara ikishindikana katika kuumaliza mgogoro huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye Mlinzi Mkuu wa Katiba, anaweza kufungua shauri la kikatiba ili kuomba ufafanuzi wa kikatiba kuhusu mamlaka hizi mbili na kuiomba mahakama kutoa uamuzi.

Baada ya kuulizwa jana kama yuko tayari kuufanyia kazi ushauri huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kilangi alisema hawezi kufanya hivyo kwa kuwa katika mgogoro huo hakuna jambo lenye mashaka litakalomfanya ahitaji tafsiri ya kisheria au jambo analolalamikia ili Mahakama itoe uamuzi. Kwa mujibu wa Profesa Kilangi, watu wanakwenda mahakamani kama kuna jambo ambalo tafsiri yake haieleweki vizuri ili Mahakama isaidie kutoa tafsiri au kuiomba mahakama ifanye kitu fulani juu ya jambo husika, na siyo kuomba namna nzuri ya kutatua mgogoro.

Alisema kama kuna jambo linampa mtu mashaka au jambo analolalamikia ikiwemo jinai kama vile kupigwa, kuibiwa au madai kama vile kudhulumiwa, kuporwa kiwanja, hivyo mhusika anaweza kwenda kufungua shauri mahakamani kwa ajili ama ya kupata tafsiri ya kisheria au Mahakama itoa uamuzi wa jambo husika. “Katika mambo haya mawili, sijaona jambo la kunifanya niende mahakamani, kwa sababu ninapokwenda mahakamani kufungua shauri, naenda kulalamika au kudai kuhusu nini,” kama tafsiri, Katiba ipo na sheria zipo, naenda kuomba tafsiri ya kitu gani,” alieleza Profesa Kilangi.

Alipoulizwa nini nafasi yake kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kupata suluhu ya mgogoro kati ya Bunge na CAG, Profesa Kilangi alisema yeye ana wajibu wa kuushauri mhimili wa utendaji na Bunge lina mwanasheria wake ambaye ana wajibu wa kulishauri Bunge, Spika au Katibu wa Bunge. Profesa Kilangi alisema pale anapotakiwa kutoa ushauri, huutoa ushauri huo kimya kimya kule alikoombwa kama ni kwa Rais, Waziri Mkuu, Waziri au mamlaka nyingine yoyote iliyoomba ushauri kwa kuwa mmiliki wa ushauri ni yule aliyeomba si aliyetoa ushauri.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshala, alisema kwa sasa TLS haijachukua uamuzi wowote kuhusu sakati hilo kati ya Bunge na CAG ikiwemo kufungua shauri mahakamani. Dk Nshala alisema TLS haiwezi kufungua shauri mahakamani mpaka Baraza la Utawala likae na kuamua kama kuna haja ya kufanya hivyo.

Alisema hata kama kutakuwa na haja ya kuingilia kati mgogoro huo kwa ajili ya kupata ufumbuzi, si lazima wafungue shauri mahakamani, bali wanaweza kwenda kuonana na kila upande na kuwashauri ili hatimaye suala hilo liishe. Alisema ni vyema inapotokea tofauti kama hizo kwa viongozi wakazimaliza kimya kimya badala ya kuziweka hadharani. Mgogoro huo umeifanya jamii kugawanyika kimtazamo, kwa kuwa wapo wanaounga mkono uamuzi wa Bunge na wengine wanaunga mkono msimamo wa CAG.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi