loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Wataalamu wa Kiswahili jisajilini katika kanzidata’

SERIKALI imehimiza wataalamu wa Kiswahili nchini kujisajili katika kanzidata wanufaike na fursa mbalimbali ikiwamo ukalimani na kufundisha lugha hiyo kwa wageni.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2019/20, bungeni jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema yapo maombi kutoka nchi nyingi ndani na nje ya Afrika zikihitaji walimu wa Kiswahili kwa ngazi mbalimbali za masomo. Dk Mwakyembe alikuwa akizungumzia taasisi za wizara yake ikiwamo Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) lenye majukumu ya kuratibu na kusimamia matumizi na maendeleo ya lugha hiyo nchini na kufuatilia maendeleo yake nje ya nchi.

Alisema hadi Machi, mwaka huu, wataalamu 624 wamejisajili katika kanzidata ambao wanawake ni 340 na wanaume 284. Aidha mafunzo ya kuimarisha stadi za kufundisha Kiswahili kwa wageni yametolewa kwa wataalamu hao katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza huku mipango ya kufikia mikoa mingine ikiendelea.

Waziri alisema sasa wanakamilisha mwongozo wa ufundishaji wa Kiswahili kwa ngazi mbalimbali na kazi hiyo ni shirikishi chini ya uratibu wa wizara yake na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Wengine ni vyuo vikuu na taasisi za maendeleo ya Kiswahili Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumzia mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20, Dk Mwakyembe alisema pamoja na kuendelea kusajili wataalamu hao na kuandaa mwongozo, Bakita itatambua na kusajili taasisi na vituo 20 vinavyofundisha Kiswahili. Alisema baraza litaandaa pia vipindi 600 vya redio na televisheni vya kuelimisha umma kuhusu matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili.

IKIWA fomu moja ya kuomba ridhaa ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi