loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kamati za siasa kata zatakiwa kuweka ajenda ya maendeleo

KATIBU wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole amezitaka kamati zote za siasa za kata kuhakikisha wanaweka ajenda ya maendeleo na kuwahusisha wataalamu wa ngazi husika.

Pia, amewataka makatibu uenezi kutotumia lugha za matusi dhidi ya wapinzani bali wanapaswa kutumia nguvu ya hoja. Polepole aliyasema hayo jijini hapa wakati akifungua mafunzo ya siasa na uenezi kwa makatibu uenezi wa CCM, Dodoma mjini. Alisema chama kinatakiwa kuendelea kuwatumikia wananchi, hivyo ni vyema kila wakutanapo kuweka ajenda ya maendeleo kwa wananchi na kuwashirikisha wataalamu wa eneo husika.

“ Kabla ya kuanza vikao vyenu mnapaswa kuweka ajenda za maendeleo na ihusishe wataalamu na viongozi wote wa kata, kueleza nini serikali ifanye, inafanya na imefanywa, CCM ndio iko madarakani hivyo na ina wajibu na inatakiwa kuendelea kutumika wananchi,” alisema. Aidha, Polepole aliwataka makatibu uenezi kutotumia lugha za matusi dhidi ya wapinzani bali wanapaswa kutumia nguvu ya hoja. “Kiongozi wa CCM kutumia lugha ya matusi ni kwenda kinyume na maadili ya chama. Msiwaite wanachama wa vyama vingine nyumbu,” alisisitiza.

Alisema viongozi wa CCM wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia maadili na matendo mema katika kuwatumikia wananchi. Polepole pia alisema idadi kubwa ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) yamepoteza mwelekeo wa kuwahudumia wananchi, hivyo nafasi hiyo inapaswa kuchukuliwa na viongozi wa CCM katika kusemea na kutatua kero za wananchi.

“Kwa sasa asilimia kubwa ya NGOs zinapoteza mwelekeo kwa sababu baadhi baada ya kuwasemea wananchi wamekuwa wakipotosha ukweli. Nafasi hiyo inapaswa kuchukuliwa na wana CCM,” alibainisha. Polepole aliwataka viongozi wa chama wenye dhamana ndani ya serikali kuacha tabia ya kutopokea simu pindi wananchi wenye kero wanapowatafuta.

“Kiongozi wa CCM mwenye dhamana serikalini anatakiwa kusikiliza na kutatua kero za wananchi muda wowote. CCM ni sauti ya umma, kuna haja ya kupaza sauti kueleza mambo muhimu ya wananchi. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma Godwin Mkanwa, alisema katika uchaguzi mkuu uliopita, walipoteza kata sita ambapo tayari kata nne zimerejea CCM na kusisitiza kuwa wanauhakika katika uchaguzi mkuu ujao watashinda kwenye kata zote.

IKIWA fomu moja ya kuomba ridhaa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi