loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Familia ya Kanumba, King Majuto zalipwa

KAMPUNI zilizoingia mikataba mibovu na baadhi ya wasanii, akiwamo Amri Athumani ‘King Majuto’ na Steven Kanumba (sasa marehemu) na kuathiri kipato chao, zimeanza kuwalipa viwango vinavyoridhisha na nyingine kuingia makubaliano baada ya kubanwa.

Aidha, Kamati ya Kupitia Mikataba haijafikia maridhiano na kampuni saba, hali ambayo serikali imetaka kampuni husika zifikie makubaliano mapema iwezekanavyo bila kulazimika kupelekwa mahakamani. Kanumba alifariki mwaka 2012 na Majuto mwaka jana na kwa muda mrefu familia zao zimekuwa zikilalamika wasanii hao pamoja na umaarufu wao na kazi nzuri walizofanya, wamekufa masikini ikidaiwa baadhi ya kampuni kuwadhulumu.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitoa taarifa hiyo jana, akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2019/20. Kulingana na hotuba yake, baada ya wizara kutaka kupitiwa upya kwa mikataba yote mibovu waliyoingia wasanii na kuathiri kipato chao, kamati ya wadau wa filamu iliundwa na kuchambua mikataba 11 iliyowasilishwa.

“Baadhi ya kampuni zimethibitisha kuwalipa wahusika viwango vya kuridhisha,” alisema na kutaja kampuni tofauti zilizomlipa Majuto jumla ya takribani Sh milioni 65. Kampuni hizo ni Pan-Africa Enterprises Ltd na Ivori Iringa ambazo zimeshaingiza kwenye akaunti maalumu Sh milioni 30 kwa kazi alizotekeleza kimkataba.

Aidha, Azam (SSB) imeandaa malipo ya ziada ya Sh milioni 20 na kampuni ya Tanfoam ya Arusha imeandaa Sh milioni 15, malipo ambayo yatawasilishwa kwa msimamizi wa mirathi wa marehemu. Baadhi ya kampuni ikiwamo ya Neelkanth Salt Ltd zilisema zimejiwekea utaratibu wa kuridhisha wa mawasiliano ya moja kwa moja na familia ya Majuto.

Kwa upande wa Kanumba, Mwakyembe alisema kampuni ya Steps Entertainment imeshakabidhi malipo ya ziada ya Sh milioni 15 kwa mama yake mzazi na imeahidi kushirikiana naye kuandaa filamu ya maisha ya mwanawe. Kampuni hiyo ya Steps Entertainment pia imemlipa msanii Sikujua Mbwewe Sh 6,750,000 kutokana na kusambazwa kwa filamu yake ijulikanayo ‘Utu Wangu’ bila ridhaa yake na filamu hiyo imerejeshwa.

Wakati huo huo, akizungumzia kampuni ambazo hazijafikia makubaliano, Mwakyembe alizitaja Tigo; Freedom Film Production; Afsar Furniture; Sterling Surfactants Ltd; Al-Riyamy Production na Al-Abdi’s Entertainment zinazohusika na kazi za Majuto. Kwa kazi za Kanumba ni kampuni ya Startimes na kwa upande wa Wastara Juma ni kampuni ya KZG Service Ltd. “Nawahimiza wadau wote wa sanaa kuhakikisha hawaingii mikataba yoyote bila ushauri wa kisheria,” alisema na kupongeza wajumbe wa kamati kwa kujitolea kwa uadilifu mkubwa.

WASANII sasa mambo yao safi baada ya serikali kuwarahisishia utendaji ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi