loader
Picha

'Dereva alinipa mimba akataka niitoe, tusijuane'

“NILIPOMALIZA kujifunzia kwa mtu ushonaji mwaka 2016, nilienda kijijini Winza katika Wilaya ya Mpwapwa kusalimia wazazi. Yaliyonikuta huko, yakabadili mwelekeo wa maisha yangu.”

Anasema Katarina Gogo (siyo jina lake halisi) aliyehitimu elimu ya msingi mwaka 2014 akiwa na umri wa miaka 15, lakini hakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari.

Katarina ambaye sasa anaelekea kutimiza umri wa miaka 20, ni miongoni mwa waathirika wa mimba za utotoni, akautumia mwaka 2015 kujifunza ushonaji kazi aliyokuwa akiifanya baba yake na alipohitimu mafunzo, alikuwa anajua kushona na kubuni mitindo mbalimbali.

Akiwa nyumbani kwa wazazi wake, Katarina alianza ushonaji wa nguo za wateja. Anasema katika kazi hiyo, alikumbana na changamoto za bidhaa zinazotumika hasa kufanyia marekebisho ya nguo kama zipu, vitambaa, nyuzi na majora.

Anasema kutokana na changamoto ya mazingira ya kijijini pale na hasa kukosekana kwa malighafi za kushonea, aliamua kuagiza vitu hivyo kwa kumtumia dereva wa gari la abiria linalofanya safari kati ya Winza na Mpwapwa.

Kwa mujibu wa Katarina, walianza vyema kwani alikuwa akiandika mahitaji kwenye karatasi na kumpa dereva huyo pamoja na fedha za kununulia vitu hivyo na kwamba, kuhusu mzigo na pesa, hapakuwa na tatizo.

“Huyo dereva alikuwa ni baba mtu mzima tu, lakini akaanza kunishawishi na kunitaka kimapenzi,” anasema na kuongeza:

“Sasa ndo natambua kuwa utoto ndio ulinifanya nikakubali kuwa na uhusiano naye kimapenzi tukawa tunakutana nyumbani kwake kijijini Winza.”

Anasema alipokuwa akifika nyumbani kwa dereva huyo mzee, hakuona mtu wala dalili yoyote ya kuwapo mwanamke katika nyumba ile.

Anasema: “Nikamwamini maneno yake, nikajitoa kwake.”

Anaulaumu umri wake kuwa mdogo wakati huo akisema kama isingekuwa hivyo, asingerubuniwa na pia, angekuwa na elimu sahihi ya kutosha kuhusu afya ya uzazi anayosema, isingemruhusu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu wa makamo yale kiasi cha kufanya ngono zembe na kuambulia ujauzito.

“Nilipomwambia kuwa nina ujauzito wake, akakataa katakata na kunitaka niitoe na ‘tusijuane.’

Kwa kweli nilichanganyikiwa sana,” anasema. Katarina anaongeza: “Nilikaa kijijini maisha yakawa magumu sana; mama mzazi naye akawa mbogo. Nikaambiwa ni mimi malaya; sina adabu. Ikabidi niende kwa shangazi anayeishi Ng’ambi Mpwapwa…”

“Basi; nikajifungua mtoto wa kiume kwa operesheni, niliambiwa mtoto ni mkubwa na nyonga hazitanuki kutokana na umri wangu kuwa mdogo.”

Anasema licha ya juhudi zake kumjulisha mwanaume huyo kuwa amejifungua, mtu huyo hakuwahi kwenda kumuona mtoto wala kumpigia simu.

“Siku moja mwaka jana (2018) wakati namsindikiza mamamdogo kwenda stendi, bwana huyo akamuona mtoto na kuanza kujisemeshasemesha kuwa mtoto anafanana naye.”

“Hata hivyo, ingawa alimuona mtoto na kumkubali, lakini hajawahi kumtolea huduma yoyote; hata senti moja,” anasema.

Anasema amekuwa akimtegemea shangazi yake kwa kila kitu na binamu zake wamekuwa wakimsaidia. Kwamba, baada ya kutelekezwa, ameamua kupambana na hali hali yake kikamilifu.

“Nataka niwe fundi mkubwa, niwe na ofisi yangu nijitegemee,” anasema Katarina akiwa miongoni mwa mabinti 30 waliojifungua katika umri mdogo wanaopatiwa mafunzo na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) mintarafu afya ya uzazi, stadi za maisha, uongozi na ujasiriamali kwa ufadhili wa Shirika la FORWARD-UK, Ubalozi wa Uholanzi na Ubalozi wa Uswidi nchini Tanzania.

Ofisa Miradi wa CDFDodoma, Clara Wisiko, anasema CDF inalenga kuwezesha wasichana walio ndani na nje ya shule, kuwezesha ulinzi wa mtoto na ushiriki wa wanaume na vijana katika kulinda haki za mtoto.

Anasema mambo mengi sasa yanawezekana kutokana na waathirika kuanza kuwa wazi kuhusu ukatili dhidi yao.

Mratibu Mkuu wa Miradi ya CDF, Evance Rwamuhuru, anasema umaskini na elimu duni ya afya ya uzazi ni changamoto na kichocheo kikubwa cha mimba za utotoni.

Wilayani Mpwapwa walipoanza huduma Machi 2017 kwa tathimini ya hali ya ukatili wa watoto, mimba za utotoni na umama katika ujana, matokeo yanaonesha haja ya huduma yao kurekebisha maisha ya waathirika na kuzuia wengi kuingia katika mkumbo huo.

Anasema tatizo la mimba za utotoni ni kubwa wilayani Mpwapwa hali inayoashiria kuwapo ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto sambamba na ukatili wa kijinsia kwa watoto hasa mimba za utotoni, ndoa za utotoni, masuala ya ukeketaji, na ukatili dhidi ya watoto kingono, kimwili na kijinsia.

Rwamuhuru anasema ili kupambana na hali hiyo, kuna mikakati inayofanyika kuwezesha wasichana kwa kuundaji vikundi na kuwatibu kisaikolojia waathirika wa mimba za utotoni ili kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida na kumudukazi zao.

Anasema CDF imewaweka pamoja wasichana 60 katika kata nne ambapo kila kata ina kikundi kimoja chenye watu 15.

“Tumeanza na kata nne, halmashauri imeomba tufike angalau kata 14. Wilaya ya Mpwapwa ina kata 33. Hata hivyo, ombi hilo tumelipokea na tutafanya hivyo ili tuzifike kata hizo,” anasema.

Anaongeza: “Tumetengeneza klabu za wasichana kila klabu wasichana 30. Kupitia klabu hizo zilizoundwa mwaka 2017/2018, tunawafundisha wasichana masuala mbalimbali kuhusu haki za watoto na mifumo ya ulinzi ili wajue ukatili sio hali yao, hivyo wasikae kimya wanapofanyiwa ukatili.”

“Hii itawasaidia kujua aina mbalimbali za ukatili, wahusika na namna ya kuuepuka, kuthubutu kukabiliana nazo au kuzikomesha.”

Miongoni mwa manufaa ya kuwapo makundi haya ni pamoja na vijana wengi na watoto kuanza kuthubutu kuzungumza matatizo yaliyopo.

“Tulikaa na wasichana wa shule za msingi tukagundua watoto wengi walikuwa wakifanyiwa ukatili wa kingono wakati wanarudi nyumbani; tulipowafundisha wakaanza kusema wanaporudi kutoka shuleni wanafunzi wa kiume au watu wazima wanawavizia,” anabainisha.

Katika shule moja ya msingi (jina tunalihifadhi), ilielezwa kuwa mlinzi wa shule hiyo alikuwa na tabia ya kulawiti watoto, lakini siku moja alipokuwa amejipanga kufanya unyama huo, aligundua kuwa tabia yake imejulikana hivyo, akatoroka na tangu mwaka jana hajaonekana.

“Hapo utaona kumbe watoto wanasema na wanaongea juu ya ukatili wanaopitia na pia tunapowafundisha, tunataka nao waende kufundisha wenzao kutambua haki za watoto na kuepukana na mimba za utotoni,” anasema.

Mratibu huyo anasema katika elimu ya afya wanasaidiana na walimu wanaangalia kipindi hatari cha kuingia ujana yaani balehe kwani wasichana wengi wamebainika kuwa, hawajui kujisimamia hivyo, kuwapa elimu hiyo.

“Wanafundishwa pia usafi maana shule nyingine kama Sekondari za Ilolo, Mount Igovu, Berege, Kibakwe na Pwaga zimetenga chumba kwa ajili ya wasichana kujisitiri huku shule za msingi zenye huduma hizo zikiwa ni Chazugwa na Mtejeta,” anasema.

Kingine wanachokifanya ni kujenga uwezo wa walimu na wakuu wa shule na bodi za shule kuhusu namna ya kuepusha ukatili katika muktadha wa shule, kuweka mikakati ya kukabiliana na ukatili katika shule zao na kuangalia namna ya kushughulika na watoto watukutu bila kuathiri haki zao.

“Tunasaidia walimu waone namna ya kusaidia watoto hapo tunagusia walimu wasitangulize wala kuruhusu hasira na tunawafundisha walimu kutofautisha kujengea mtoto nidhamu na kuadhibu mtoto maana kazi ya mwalimu ni kumjengea nidhamu mwanafunzi siyo kumwadhibu na pia, tunajadiliana na walimu kuhusu njia tunayotakiwa kutumiwa kwa watoto,” anasema.

Anatoa mfano: “Tulipata kesi katika Shule ya Msingi Ilolo ambapo mtoto alitaka kujinyonga kwa sababu aliiba Sh 1,000 nyumbani kwao akatumia Sh 300, lakini Sh 700 zilizobaki akapoteza… mama akasema asirudi nyumbani ndipo mtoto huyo akachukua kamba ili akajinyonge, ingawa bahati nzuri hakutimiza lengo hilo maana watu waliwahi kumwokoa.”

Anasema ushiriki wa wazazi katika elimu ya watoto wao ni mdogo na hata wakiitwa shuleni hawatoi ushirikiano wa kuitikia mwito.

“Kibakwe kuna mzazi aliitwa mara tatu, lakini hakufika shuleni kujua anaitiwa nini… changamoto kubwa kwa wazazi ni kutotaka kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni…. Tunataka tuweke kanuni ndogo kwa wazazi wasiojishughulisha na elimu ya watoto wao.”

Changamoto nyingine kubwa ni baadhi ya watoto kupanga nyumba (vyumba) vijijini ili waishi karibu na shule.

“Hali hii inawafanya wengine kujikuta wanaishi kinyumba na wanaume,” anasema na kuongeza: “Tuliwahi kupata kesi ya binti wa kidato cha pili, alikuwa amepanga mtaani. Kijana mmoja akaenda kuvunja mlango usiku akaingia ndani na kutaka kumbaka binti akapiga kelele wale vijana wa shuleni wakasikia wakaenda kutoa taarifa kwa mwalimu na kwa mtendaji, yule kijana alikamatwa tayari akiwa amevua nguo akapelekwa kituo cha polisi.”

Alifahamisha, walikutana na kesi nyingine ambapo ofisa mtendaji wa Kijiji cha Barege alikuwa anasuluhisha kesi ya binti wa miaka 14 kumkimbia kijana aliyetaka kumwoa aliyemshitaki kaka wa binti akidai amrudishie mke au mahari aliyotoa.

“Tulimhoji kwanini kuna usuluhishi kwenye kesi ya jinai, kesi ya jinai kama hiyo lazima iende polisi,” anasema.

Aidha ilibainika kuwa, baada ya walimu kufundihswa mintarafu ulinzi wa mtoto, walimu hao walirudi kuwasikiliza watoto na miongoni mwa malalamiko waliyoytoa wanafunzi hao ni kuwa, walimu wanawasema na kuwapa matusi yanayowafedhehesha. Rwamuhuru anasema kila mwaka kutakuwa na Siku ya Mtoto wa Ilolo.

BANDARI za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinginezo ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi