loader
Picha

Ubinafsi, ujuaji umeiangamiza Serengeti Boys

NDOTO za Watanzania kuishuhudia timu yao ya taifa ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, ikishiriki kwa mara ya kwanza fainali za kombe la dunia Brazil zimepotea, baada ya kupoteza michezo yote mitatu ya fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo.

Tanzania ikiwa mwenyeji, wawakilishi wake Serengeti Boys walianza kwa kipigo cha mabao 5-4 kutoka kwa Nigeria, katika mchezo wa pili wakafungwa mabao 3-0 na Uganda kabla ya kukamilisha safari yao ambapo walifungishwa virago na kuwa watazamaji kwa kipigo cha mabao 4-2, kutoka kwa Angola.

Vijana hao wa kocha Oscar Mirambo, tofauti na wanavyojulikana, hawakuwa na jipya lolote kwenye michuano hiyo zaidi ya kila mchezaji kuonekana kutumia kipaji chake na siyo mbinu za kocha kama ilivyokuwa kwa timu nyingine za wageni.

Serengeti Boys imemaliza na kutolewa kwa aibu kwani haikupata hata pointi moja huku ikiruhusu mabao 12 katika mechi tatu ilizocheza kwenye kundi hilo la A yenyewe ikifunga mabao sita.

Haya ni matokeo mabaya na ya aibu kuwahi kutokea kwa timu zetu za taifa hasa tukiwa ndiyo waandaaji na maandalizi ambayo imepatiwa timu hiyo.

Kocha Mirambo ambaye ndiye mtuhumiwa namba moja, amekiri matokeo waliyoyapata siyo rafiki kwake, benchi la ufundi na watanzania wote na kuomba radhi kwa kilichotokea kwani hata wao hawakukitarajia.

Mirambo anasema analazimika kubeba lawama ingawa sababu iliyosababisha timu hiyo kufanya vibaya ni kukosa maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kufanya vizuri mashindano hayo.

“Kwa niaba ya benchi la ufundi la Serengeti Boys naomba radhi kwa Watanzania wote, nakiri matokeo siyo mazuri kwetu na yamewaumiza wengi lakini haikuwa matarajio ingawa tumejifunza kitu kutoka kwa wenzetu,” anasema Mirambo.

Kauli ya kocha Mirambo inashangaza wengi kwani kama kuna timu ambayo imekaa kambini kwa kipindi kirefu nchini basi ni Serengeti Boys na ilipangiwa muda maalumu na kocha huyo.

Mbali na kukaa kambini muda mrefu, Serikali chini ya Rais John Magufuli ilitoa kitita cha Sh bilioni moja kwa maandalizi, hiyo ni kwa mara ya kwanza serikali kutoa fedha nyingi kiasi hicho kwa timu za taifa.

Serengeti ndiyo timu inayoongoza kwa kupanda ndege zaidi ya ilivyokuwa viongozi wa serikali kwenda nje ya nchi na kushiriki mashindano mbalimbali hiyo yote, ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo.

Hapo ifahamike kwamba harakati za kuiandaa timu hiyo zikianza miaka mitatu nyuma chini ya kocha huyo ambaye alipewa nafasi hiyo baada ya kuondolewa Bakari Shime aliyekuwa chini ya Kim Poulsen.

Kocha huyo hodari katika kutumia lugha ya kigeni anapokuwa kwenye mikutano na vyombo vya habari na hata anapofundisha wachezaji wake wakati mwingine, anasema ameitumia michuano hiyo kujifunza vitu vingi ikiwemo namna ya maandalizi kuelekea michuano mikubwa kama hiyo ya Afcon.

Kauli za Mirambo zinatia shaka kwani inaonesha maandalizi yote waliyofanya kwa zaidi ya miaka miwili akiwa na timu hiyo ilikuwa ni sawa na bure?.

Leo anatuambiaje hakupata maandalizi ya kutosha, alitakaje, akae na wachezaji miaka mitano?

Anajiandaa na nini? Mirambo akiwa na kikosi cha Serengeti ameshinda mataji mbalimbali ikiwemo COSAFA tena wakiwa waalikwa lakini pia alishinda taji la Afrika Mashariki kule Burundi CECAFA na hivi karibuni alifanya hivyo nchini Rwanda katika mashindano maalumu.

Kwa mafanikio hayo ukitoa ile michuano maalumu iliyofanyika kule Uturuki ambapo Serengeti haikufanya vizuri, watu wengi waliamini mwaka huu ni zamu yetu kuondoa machungu ya kushindwa katika mchezo huo kumbe tunakuja kujitia aibu.

Mirambo aliwajaza watanzania imani na kujitapa kuwa hakuna timu wanayoihofia na jeshi lake lipo tayari kwa ajili ya fainali hizo na jambo la kushinda mechi mbili na kwenda Brazil halitokuwa gumu kutokana na uenyeji wao.

Leo mambo yamegeuka kila mmoja anamtaja Mirambo kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha timu hiyo kutofanya vizuri na hiyo inatokana na aina ya uchezaji wa timu katika mechi zote tatu.

Ukilinganisha na timu nyingine Serengeti ndio walioonekana kuwa wepesi zaidi kufungika na hata haikujulikana walikuwa wanatumia mfumo gani wanapokuwa uwanjani, fikiria muda wote wachezaji wamekaa kambini mpaka wakati mashindano kocha haijulikani anatumia mtindo gani, hana kikosi cha kwanza, mechi zote tatu kabadili sehemu kubwa ya wachezaji, ajabu.

Yapo mambo mengi yanayomhusu kocha yanaongelewa na utawala wake kwenye timu hiyo ambapo inadaiwa kocha huyo hakuwa na uwezo sahihi kuiongoza timu katika michuano mikubwa kama hiyo kwani uwezo wake bado ni wakufundisha mashindano ya ndani.

Taarifa kutoka ndani ya TFF, zinaeleza kwamba kocha Mirambo alikuwa mbinafsi na alikuwa akiifundisha timu hiyo kwa minajili ya kupata sifa yeye kama yeye bila kushirikiana na wenzake.

Ndiyo maana yeye kama kocha mkuu lakini kazi zote za timu ambazo zingeweza kufanywa hata na msaidizi wake alikuwa akizifanya yeye jambo ambalo ni nadra sana.

Kama siyo mfuatiliaji sana wa timu hiyo huwezi kumjua msaidizi wa Mirambo lakini msaidizi yupo ni Maalim Salehe ‘Romario’ lakini yupo kwenye benchi kama ushahidi, lakini kazi zote ikiwemo upangaji wa koni kwenye mazoezi anafanya mwenyewe. Lakini pia wakati mashindano yanaanza, Romario hakuwepo kabisa nchini, badala yake alikwenda Misri na timu nyingine ya vijana, kufanya nini?

Kama Romario alipewa timu nyingine basi angeteuliwa kocha mwingine wa kusaidiana na Mirambo, hili ni kosa ambalo TFF haiwezi kukwepa pia.

Katika mechi ya mwisho Romario, muda mwingi alionekana akiwa sawa na wachezaji wa akiba pasipo kufanya kazi yoyote na muda wote Mirambo na kocha wa makipa Peter Manyika ndiyo waliokuwa wakisimama kutoa maelekezo kwa wachezaji.

Lakini baadhi ya watendaji waliopo ndani ya Shirikisho la Soka nchini, TFF, wanamtupia lawama Mirambo wakidai kwamba yeye ndio mhusika namba moja kutokana na namna alivyokua akijiamulia mambo yake mwenyewe. Inaelezwa kwamba Mirambo, mara kadhaa aligoma kupewa makocha wa kumuongezea nguvu na kumshauri katika kukiandaa kikosi hicho na ndiyo hata wakati maji yanamzidi watu walijiweka pembeni na kumuangalia akizama.

Kocha huyo anadaiwa kuwanyima uhuru wachezaji wake na muda mwingi kuwafungia ndani jambo ambalo inadaiwa kukosa muda wa kuwaza mambo mengine ili kuzirifresh akili zao jambo ambali limetafsiriwa kama kuwabebesha mzigo mkubwa hasa baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Nigeria.

Katika mabenchi ya timu za wenzetu tumeona yalivyokamilika wakiwemo makocha wasaidizi wachua misuli wataalamu wa mazoezi ya viungo na wengineo lakini kwetu ilikuwa tofauti.

Tangu juzi baada ya kipigo cha Angola wadau wa soka walionesha kumkumbuka aliyekuwa kocha wa timu hiyo siku za nyuma Mchawi Mweusi Bakari Shime ambaye aliipeleka Serengeti Boys fainali za Afcon za Gabon, ambapo pamoja na kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia lakini alivuna pointi nne kwa kushinda mechi moja kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Lakini siyo yeye tu mwingine anayekumbukwa hapa ni Mdenmark Kim Poulsen, ambaye kwa muda aliokuwa nchini alijenga timu imara ya vijana wenye umri huo na kuwa ya kuogopewa Afrika Mashariki na kati lakini alikuwa akishirikiana na Shime.

Baada ya kutolewa TFF, inapaswa kufanya maamuzi magumu kwa manufaa ya soka letu lakini pia inapaswa kuanza mapemamkakati wa kuiandaa timu mpya ambayo itafuzu fainali zijazo ambazo zitafanyika Cameroon 2021.

Na katika maandalizi hayo, TFF isirudie kosa ililolifanya kwa Mirambo, itafute makocha wanaostahili na kuweka mikakati thabiti, michuano ya mwaka huu ilijulikana miaka zaidi ya mitatu iliyopita, lakini timu yetu imeshiriki kama ilikurupushwa kutoka usingizini.

Tumeyataka wenyewe.

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi