loader
Picha

Wakati umefika kuchangamkia soko EAC

HAKUNA ubishi kwamba ili kuimarisha biashara yoyote ile duniani, zikiwemo kampuni na nchi mbalimbali, uhakika wa kuwa na soko la bidhaa husika, lina umuhimu wa pekee kwa uhai na maendeleo ya biashara husika.

Tunapenda kuunga mkono kwa dhati, mwito uliotolewa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro katika mahojiano na gazeti hili kwamba Watanzania hawana budi kuchangamkia fursa ya soko la bidhaa zake katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa mujibu wa Dk Ndumbaro, kwa kuanzia Watanzania wanaweza kuchangamkia masoko ya vyakula, bidhaa za mimea na usafirishaji bandarini pamoja na kuongeza uwezo wa huduma za kifedha kwa mabenki kwa kufungua matawi yake mjini Kigali nchini Rwanda.

Alieleza fursa nyingine ya Tanzania ya kuuza bidhaa zake mbalimbali kwamba ziko pia nchini Kenya, ambako matatizo yaliyokuwa vikwazo kwa Tanzania kuuza bidhaa zake nchini humo hapo awali, yamepatiwa ufumbuzi na kwamba kazi sasa iko kwa wananchi kuishi na changamoto ya kupeleka bidhaa zake katika soko hilo.

Nchi nyingine wanachama wa EAC ni Burundi, Uganda na Sudan Kusini, ambako katika uzoefu wanaoendelea kuupata Watanzania katika nchi hizo za awali za EAC inazofanya nao biashara, kuna kila sababu za kuingia katika soko zima la jumuiya hiyo.

Katika hili, tunapenda kutoa mwito maalumu kwa Watanzania, kuachana na suala la umimi ili kushirikiana na kujifunza miongoni mwao mbinu nzuri za kuwawezesha kushika masoko katika nchi hizo kwa njia binafsi au kwa kushirikiana baina ya kampuni na kampuni kujipatia soko la uhakika kwa bidhaa zao.

Hapa pia tunapenda kutoa changamoto kwa taasisi zetu za mafunzo ya masuala mbalimbali ya biashara hapa nchini, vikiwemo vyuo vikuu, navyo vitenge muda wa kuwapatia mafunzo mbalimbali kampuni zetu ili nazo ziingie katika masoko ya biashara ya kimataifa kwa uhakika bila kufanya ubahatishaji.

Historia ya nchi yetu yenye kulinda, kuenzi na kuheshimu utu wa binadamu kwa gharama yoyote na kuheshimu umoja na mshikamano wa kitaifa, iwe dira yetu katika kufanya biashara na mataifa wanachama wa EAC na hata baadaye nje ya ukanda huu.

Watanzania wote wenye uwezo na dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo, kwa wao binafsi na kwa taifa letu, wana kila sababu ya kutumia fursa hii ya biashara, kutufikisha kwenye maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa kushika soko la EAC. Hili linawezekana.

HIVI karibuni wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni, Waziri ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi