loader
Picha

Wahifadhi waagizwa kuvaa sare, nembo za majina

KATIKA kukabiliana na vitendo visivyofaa, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameziagiza taasisi za uhifadhi kuhakikisha watumishi wanavaa sare za kazi zenye nembo yenye majina.

Akizungumza na wananchi wa vijiji 15 vilivyomo na kuzunguka Pori la Akiba la Swagaswaga na Mkungunero mkoani Dodoma, Kanyasu alisema kwa mtumishi wa taasisi za uhifadhi kuvaa sare yenye majina kutasaidia mwananchi kutambua kuwa amehudumiwa na nani jambo litakalosaidia kuwabaini wale wanaofanya mambo ya hovyo.

“Naziagiza taasisi zote za uhifadhi, sare za watumishi ziwe na nembo yenye jina la mtumishi, lengo letu ni kusaidia kuwabaini wale wachache wanaotenda matendo yasiyofaa kwa Wananchi na hivyo kuharibu sifa ya mafunzo ya Jeshi Usu.

Aliongeza: “ Pia nembo yenye majina itasaidia kuwatambua wahifadhi ambao wanatekeleza majukumu yao kwa maslahi ya taifa na sio kwa matakwa yao binafsi. Pia itasaidia wananchi kuwatambua wahifadhi kwa sura na majina,” Akizungumzia kuhusu matendo yasiyofaa ambayo baadhi ya wananchi wamekuwa wakiyalalamikia kutoka kwa baadhi ya Wahifadhi hao, Kanyasu alikemea tabia ya baadhi ya watumishi kuwaomba rushwa, kuwanyanyasa na kuwatisha wananchi na kuwa matendo hayo hayakubaliki hata kidogo.

“Siwezi kukubali kuona Wahifadhi wote wanaonekana ni wala rushwa, watu makatili katika jamii ilhali kuna wachache wanaochafua sifa ya jeshi letu.” Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia Wahifadhi kuwa vitendo hivyo ni hatari na vina madhara makubwa pande zote. Hata hivyo, aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kulinda na kuhifadhi maeneo ya hifadhi kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote na kuwataka nao wafuate sheria.

Naye, Juma Ismail kutoka kijiji cha Ikengwe alisema kuna baadhi ya Wahifadhi wamekuwa na utu katika jamii kwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria ila kuna baadhi wamekuwa ni vinara wa rushwa. Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, (TAWA) Mabula Misungwi aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vile hifadhi hizo wanazilinda kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye. Pia aliwahimiza wananchi kufuata sheria za mhifadhi ili kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na Wananchi.

MAKUBALIANO ya mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi