loader
Picha

Minada ya mifugo kufanyika nje ya hifadhi

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameagiza minada ya mifugo baada ya serikali kushinda kesi ifanyike nje ya hifadhi ili kuondoa dhana ya kuwa wahifadhi wanajiuzia wenyewe.

Pia, amewaonya askari wanyamapori wenye tabia ya kuvizia mifugo ikiwa mpakani kati ya kijiji na hifadhi na kisha kuwasukumia ndani ya hifadhi ili waikamate na kusema si sawa. Kanyasu alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na viongozi wa vijiji 15 vilivyopo na vinavyozunguka Pori la Akiba la Mkungunero lililopo wilayani Kondoa mkoani hapa.

Alisema mifugo inayokamatwa katika hifadhi na kutakiwa kupigwa mdana, ipigwe mnada nje ya hifadhi ili kuondoa dhana ya kuwa wahifadhi wanajiuzia wenyewe. Kanyasu alisema kuwa kabla ya minada hiyo kufanyika ni lazima itangazwe katika vijiji ili kuwajulisha wananchi na kutoa fursa ya wao kushiriki katika minada hiyo. Pia, alisema hatua ya minada kufanyika nje ya hifadhi, kutaondoa tatizo la vibali vya kuingia kwenye hifadhi wakati wa minada kwani wananchi wanalazimika kuwa na vibali na kwa wale ambao huingia bila vibali hukamatwa kwa makosa ya kuingia hifadhini kinyume cha taratibu.

“ Minada hii ikifanyika nje ya hifadhi, hata tuhuma na malalamiko mengi yatapungua kama vile tuhuma za rushwa na malalamiko ya kuwa wahifadhi ndio wamekuwa wakishiriki kuwatafuta wanunuzi wa mifugo kwa makubaliano ya kulipwa mara baada ya mnada.” Aliongeza: “ Pia kumekuwapo na malalamiko ya wale ambao mifugo yao imetaifishwa kuwa hawajui siku inayofanyika minada hiyo na badala yake wanaopewa taarifa ni wafanyabiashara wakubwa pekee jambo ambalo linaibua chuku dhidi ya wahifadhi.”

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikengwe, Ismail Hamis alisema licha ya huo utaratibu mpya wa kufanyia minada nje ya hifadhi, anaiomba serikali iangalie upya sheria ya kutaifisha mifugo kwani imesababisha wafugaji wengi kuwa maskini. Alisema ni vyema mifugo ikikamatwa ndani ya hifadhi, waruhusiwe kulipa fidia kwa sababu mifugo hiyo ndio imekuwa tegemeo lao kwa kuwasaidia kusomesha watoto wao.

Kwa upande wake, Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi aliahidi kutekeleza agizo hilo na kusisitiza kuwa watafanya utaratibu wa kuwajulisha wananchi wa maeneo ambayo mifugo imekamatwa. Misungwi pia aliwataka watumishi hao kujiepusha na rushwa pindi wanapokamata mifugo kutoka kwa wafugaji.

MAKUBALIANO ya mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi