loader
Picha

Awamu ya Tano imeng’ara ripoti za CAG

TATHMINI hii imesheheni ripoti mbalimbali za Ofi si ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/2014 ili kuweza kutoa mwangaza halisi kwa mambo ambayo wananchi wengi wameshindwa kuyaona au kuyafahamu.

Hali hii imesababisha watu wachache kuishia kuelezea upande mmoja bila kuonesha au kueleza kiwango cha mafanikio yaliyofikiwa kwa kulinganisha tulikotoka, tulipo na tunapokwenda. Halikadhalika, inaonesha kiwango cha utekelezaji wa mapendekezo mbalimbali ya Ofisi ya CAG kwa muda wa miaka mitatu ya fedha, kuanzia 2015/2016, 2016/2017 hadi 2017/2018.

Nitoe angalizo ya kuwa ripoti ya jumla ya CAG iliyosomwa mwaka huu imejumuisha pia ukaguzi maalumu wa miradi ya muda mrefu kabla ya uwepo wa Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo ni vyema wananchi wakawa makini ili wasipotoshwe na watu wenye maslahi yao binafsi dhidi ya serikali.

Tathmini hii inabeba taswira halisi ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuchambua ripoti za CAG kuanzia mwaka 2013/2014 kabla ya uwepo wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Dk John Magufuli. Uchambuzi huu utajikita katika maeneo makubwa manane kama ifuatavyo: Hati za ukaguzi kwa miaka mitatu Katika mwaka wa fedha 2015/2016, jumla ya hati za ukaguzi 505 zilitolewa huku hati zilizoridhisha zikiwa 436 sawa na asilimia 86.34, hati zenye mashaka zilikuwa 60 sawa na asilimia 11.88, hati zisizoridhisha zilikuwa nne sawa na asilimia 0.79 na hati mbaya zilikuwa tano sawa na asilimia 0.99.

Katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya hati 561 zilitolewa huku hati zilizoridhisha zilikuwa 502 sawa na asilimia 90, hati zenye mashaka zilikuwa 45 sawa na asilimia 8, hati zisizoridhisha zilikuwa 7 sawa na asilimia 1 na hati mbaya pia zilikuwa 7 sawa na asilimia 1.

Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya hati za ukaguzi 548 zilitolewa huku Hati zilizoridhisha zilikuwa 531 sawa na asilimia 97, hati zenye mashaka zilikuwa 15 sawa na asilimia 2.6, hati zisizoridhisha ilikuwa 1 sawa na asilimia 0.2 na hati mbaya pia ilikuwa 1 sawa na asilimia 0.2. Kwa mantiki hiyo kumekuwa na ongezeko la hati safi mwaka hadi mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli na ongezeko hili linaonesha uwepo na uimarikaji wa ufanisi katika usimamizi wa rasilimali fedha.

Hali hii kwa sehemu kubwa ni matunda ya ongezeko la nidhamu kazini na utendaji uliojikita katika kusimamia fedha za umma kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuweka msisitizo kwenye matokeo (result driven). Ukaguzi wa miradi ya maendeleo Katika muda wa miaka mitatu ya fedha, yaani kutoka 2015/2016 hadi 2017/2018 jumla ya miradi ya maendeleo 2,008 imekaguliwa na Ofisi ya CAG.

Katika mwaka 2015/2016 jumla ya miradi ya maendeleo 797 ilikaguliwa huku katika miradi hiyo jumla ya miradi 725 sawa na asilimia 91 ikipata hati safi, miradi 71 sawa na asilimia 8.9 ilipata hati yenye mashaka na mradi mmoja tu ndio ulipata hati mbaya ambao ni sawa na asilimia moja. Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 jumla ya miradi ya Maendeleo 742 ilikaguliwa huku miradi 697 sawa na asilimia 94 ikipata hati safi; miradi 44 sawa na asilimia 5.9 ilipata hati yenye mashaka na mradi mmoja sawa na asilimia 0.1 ulipata hati mbaya.

Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya miradi ya maendeleo 469 ilikaguliwa na kati ya miradi hiyo miradi 455 sawa na asilimia 97 ilipata hati safi, huku miradi 14 sawa na asilimia 3 ikipata hati yenye mashaka na hakukua na mradi wowote uliopata hati mbaya. Aidha, uimarikaji wa usimamizi na kupungua kwa sehemu kubwa ya matumizi mabaya ya fedha za umma kumeondoa nafasi ya uwepo wa hati mbaya katika miradi na hivyo kuongeza nguvu ya mataifa rafiki kuweza kuwekeza zaidi katika miradi mbalimbali nchini.

Kwa kipindi kirefu sasa ni mwaka 2018 tu ndio ambao hakuna mradi hata mmoja wa maendeleo uliopata hati mbaya. Ufanisi kwenye serikali za mitaa Katika kipindi cha miaka mitatu yaani kutoka mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2017/2018, mamlaka ya serikali za mitaa imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka, hii ni kwa ongezeko la utekelezaji wa mapendekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Ofisi ya CAG.

Ongezeko hili linaendana na kupungua kwa idadi ya makosa mbalimbali ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakionwa na Ofisi ya CAG Kwenye ukaguzi uliofanywa na CAG mwaka 2015/2016, jumla ya mapendekezo 79 yalitolewa katika ripoti ya CAG huku mapendekezo yaliyofanyiwa kazi mpaka mwisho wa mwaka huo wa fedha yakiwa ni asilimia nne na yale yaliyokuwa yakiendelea na utekelezaji yalikuwa ni asilimia 44.

Lakini katika mwaka 2016/2017 kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na serikali kwenye kusimamia halmashauri nyingi, mapendekezo yalipungua hadi kufikia 68 na yaliyofanyiwa kazi yaliongezeka hadi kufikai asilimia 4.4 huku yaliyokuwa yakiendelea kufanyiwa kazi yakifika asilimia 50 ya mapendekezo yote.

Katika mwaka 2017/2018 tulishuhudia ufanisi ukiongezeka maradufu na mapendekezo ya mapungufu na ufanisi yalipungua kwa zaidi ya asilimia 21 na kufikia 62 kulinganisha na mapendekezo yaliyoonekana katika ripoti ya mwaka 2015/2016 huku utekelezaji wa mapendekezo hayo ukiongezeka kwa zaidi ya asilimia 2.2 kulinganisha na muda kama huo kwa mwaka 2015/2016.

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imekuwa na ongezeko kubwa la utekelezaji wa mapendekezo ya Ofisi ya CAG na kuongeza uimara katika usimamizi wa fedha za umma hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo nchini. Ongezeko la mapato ya kodi Mpaka kufikia Juni 30 mwaka 2016, makusanyo yatokanayo na kodi yalipita malengo kwa asilimia moja.

Fedha iliyokusanywa ilikuwa ni shilingi trilioni 12.363. Uvukaji wa malengo ulichangiwa na ongezeko la usimamizi mzuri na ufatiliaji wa malipo ya kodi yaliyotokana na uboreshaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Aidha tarehe 30 Juni 2018 makusanyo yatokanayo na kodi yalifikia Jumla ya shilingi za kitanzania trilioni 15.38, hilo ni ongezeko la ukusanyaji wa kodi kwa zaidi ya Sh trilioni 3.02 kulinganisha na makusanyo kama hayo yaliyofanyika Juni 2016.

Makusanyo halisi yakijumuisha misamaha ya vocha katika mwaka 2018 yalifika hadi shilingi trilioni 15.40 na ongezeko likiwa ni shilingi trilioni 3.04 Usimamizi wa Deni La Taifa Deni la Serikali au maarufu kama Deni la Taifa ni fedha ambazo serikali imekuwa ikikopa kutoka ndani au nje ya nchi kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Nchi zote duniani hukopa ili kufanikisha miradi au utekelezaji wa mambo ya kitaifa. Kwa muda wa miaka mitatu kumekuwa na kushuka kwa kiwango cha ongezeko la ukuaji wa deni la Taifa, kinyume kabisa na taarifa zinazosambazwa na watu wengi.Tarehe 30 Juni 2013, deni la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 25 huku likiongezeka kutoka trilioni 16.98 mwaka 2011/2012 hadi kufikia trilioni 21.20 mwaka 2012/2013. Ongezeko hili ndio lilikuwa ongezeko kubwa kwa kipindi kirefu.

Mwaka 2014/2015 lilikua kwa asilimia 22 kutoka shilingi trilioni 33.54 hadi shilingi trilioni 41.04 mwaka 2015/2016. Mwaka 2016/2017 ongezeko hili lilishuka kwa asilimia 10 kutoka asilimia 22 mpaka asilimia 12 katika mwaka wa fedha ulioshia Juni 2017. Ongezeko la ukuaji lilishuka tena hadi kufikia asilimia 10.5 mwisho wa mwaka wa fedha wa 2017/2018 yaani tarehe 30 Juni 2018.

Hii inamaanisha ya kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Magufuli utegemezi wa mikopo kutoka ndani na nje ya nchi umepungua kwa asilimia 58 na hii inadhihirishwa na kiwango cha ukuaji wa Deni la Taifa kutoka asilimia 25 mwaka 2013 hadi kufikia kiwango cha asilimia 10.5 mwaka 2018. Kupungua huku kunatokana na kuimarisha mifumo ya usimamiaji na ukusanyaji mapato nchini.

Mishahara kwa watumishi hewa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la mishahara iliyokuwa ikipotea kupitia ulipaji wa watumishi waliokufa, waliostaafu na wale waliosimamishwa kazi. Mwaka 2013/2014 jumla ya shilingi bilioni 1.62 zilitumika kulipa mishahara hewa huku wizi kupitia malipo ya mishahara hewa ukiwa zaidi ya asilimia 77 na katika mwaka 2015/2016 na kufikisha jumla ya shilingi bilioni 7.3 ambayo yote ilitokea kabla ya serikali ya awamu hii.

Lakini hadi kufikia tarehe 30 Juni 2018 ni shilingi milioni 207.37 ndio fedha zimepotea kama malipo ya mishahara hewa, hivyo Rais Magufuli kwa kiwango kikubwa kupitia kampeni yake aliyoifanya ya kudhibiti malipo ya mishahara hewa kuanzia mwaka 2016 nchi nzima iliyoenda pamoja na kuwachukulia hatua watendaji wote waliokuwa wakihusika katika kufanya udanganyifu huu imekuwa na matokeo chanya. Kampeni hiyo imesaidia kuokoa zaidi ya Sh bilioni 7 kwa kulinganisha na fedha zilizotumika kulipa wafanyakazi hewa katika mwaka wa fedha 2015/2016.

Haya ni mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi kwani tatizo hili liliora mizizi kwa muda mrefu. Ujenzi mji wa Serikali Dodoma Maamuzi ya Rais Magufuli kuhamia Dodoma na kuhakikisha wizara na taasisi mbalimbali za serikali zinahamia kwenye majengo yaliyojengwa na serikali kumekuwa ni nafuu kubwa na kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikipotea kwa muda mrefu huko nyuma. Mathalani, kwa ukaguzi maalumu uliofanywa na Ofisi ya CAG katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 ulibaini kwamba serikali ilikuwa ikitumia jumla ya shilingi bilioni 7.9 kama kodi kwa ajili ya kulipia pango kwenye ofisi 14 tu za serikali.

Hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imeokoa fedha hizi kupitia ujenzi wa Ofisi za serikali na mwisho kuondoa matumizi yasiyo ya kilazima kama ilivyopendekezwa na CAG mstaafu, Ludovick Utouh katika ripoti yake ya mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni 2013.

Japokuwa zimekuwepo changamoto nyingi katika usimamiaji wa miradi ya maendeleo nchini kwa muda mrefu bado serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli inabaki kama moja ya serikali za mfano nchini na barani Afrika kwa kuweza kupunguza na kuondoa sehemu kubwa ya matumizi ya fedha ambazo zilikuwa zikipotea kwa uzembe na udanganyifu.

Halikadhalika, tofauti na huko nyuma, fedha ambazo zimekuwa zikichukuliwa kama mikopo zimekuwa zikitumika vizuri na thamani yake kuonekana katika ujenzi wa miradi mikubwa ya nchi inayotupeleka kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.

Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kama Mchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe. Alichapisha makala haya kwenye Mtandao wa Jamii Forum Aprili 22, 2019.

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi