loader
Dstv Habarileo  Mobile
Watumishi wa umma wavae sare

Watumishi wa umma wavae sare

HATUA ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ya kuziagiza taasisi za uhifadhi kuhakikisha watumishi wanavaa sare za kazi zenye nembo yenye majina haina budi kuigwa na taasisi nyingineza umma hapa nchini.

Tunasema ni vema na taasisi nyingine za serikali zikachukua hatua hiyo kwa kuwa mbali na kuwatambulisha watumishi wanapokuwa kazini, lakini pia inaondoa wasiwasi wa watu wasiokuwa na maadili mema kutumia nafasi zao vibaya.

Naibu Waziri Kanyasu alitoa agizo hilo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji 15 vinavyozunguka Pori la Akiba la Swagaswaga na Mkungunero mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa Kanyasu, watumishi wa taasisi za uhifadhi kwa sasa watalazimika kuvaa sare zenye nembo za majina ili kusaidia mwananchi kutambua kuwa amehudumiwa na nani, jambo litakalosaidia kuwabaini wale wanaofanya mambo ya hovyo.

Ni kutokana na mtazamo huo, tunaamini zipo taasisi nyingi za umma ambazo baadhi ya watumishi wake wamekuwa wakifanya mambo ya hovyo, lakini kwa kuwa wanakuwa hawana sare wala nembo zenye majina, inakuwa ni vigumu kwa wananchi kuweza kuwaripoti kwa ufasaha kwa wahusika.

Mfano mzuri ni askari polisi ambao wanavaa sare.

Hao hawawezi kuharibu au kufanya mambo ya hovyo mitaani kwa kuwa sare zao zenye namba maalumu za utambulisho walizovaa, zikinukuliwa ni rahisi kuripotiwa kwa wahusika.

Tatizo kubwa liko kwa askari polisi ambao hawavai sare. Walio wengi wamekuwa wakifanya mambo ya hovyo mitaani, ikiwa ni pamoja na kukamata wahalifu lakini wakaishia kuomba rushwa na kuwaachia.

Hili limekuwa ni tatizo sugu kwa kuwa kuwatambua askari hawa ambao hawana sare ni vigumu.

Naibu Waziri Kanyasu anasema kuvaa nembo zenye majina itasaidia kuwatambua watumishi ambao wanatekeleza majukumu yao kwa maslahi ya taifa na sio kwa matakwa yao binafsi.

Pia itasaidia wananchi kuwatambua watumishi kwa sura na majina. Mambo ya hovyo aliyoyataja Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, ni kuwa baadhi ya watumishi wanatumia nafasi zao vibaya kwa kuomba rushwa, kunyanyasa na kuwatisha wananchi ambapo alisema matendo hayo hayakubaliki hata kidogo.

Tunaamini, mkakati huu usiishie kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii tu, bali uende mbali zaidi na kwa taasisi nyingine za umma, jambo ambalo liziwezesha taasisi hizo kuondoa kero kwa kuwa watumishi wenye sare na nembo zenye majina ni vigumu kufanya mambo ya hovyo kwa wananchi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4de7f35500e122613f987695ead6f7af.jpg

KWA mara ya kwanza leo dunia inaadhimisha ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi