loader
Dstv Habarileo  Mobile
Agizo la Magufuli usajili simu litekelezwe

Agizo la Magufuli usajili simu litekelezwe

HIVI karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitangaza kuwa usajili simu za mkononi kwa kutumia vitambulisho vya taifa, vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) utaanza Mei mosi mwaka huu.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye, alilieleza Bunge mjini Dodoma Aprili 25, mwaka huu kuwa ukomo wa kusajili laini kwa alama za vidole kwa kutumia vitambulisho vya NIDA ni Desemba 31, mwaka huu na baada ya hapo laini zisizosajiliwa, zitazimwa moja kwa moja.

Baada ya tangazo hilo la TCRA na wizara hiyo, makampuni ya simu yamekuwa yakiwapelekea ujumbe wateja wao kila siku mara kwa mara, unaowataka kuanzia tarehe 1 Mei mwaka huu kusajili upya laini zao za simu kwa mfumo wa alama za vidole; na kuwataka kutembelea maduka ya makampuni hayo wakiwa na vitambulisho vya Taifa au namba ya NIDA.

Hivyo, tunamshukuru mno Rais John Magufuli kwa ufafanuzi aliotoa juzi kuhusu suala hilo, wakati akihutubia wananchi katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya, kwenye ziara yake ya siku nane mkoani humo.

Katika hotuba hiyo, rais anaagiza kuwa kazi ya usajili wa simu, iliyotangazwa mapema mwezi ujao kwa kutumia vitambulisho vya taifa, iende sambamba na uandikishaji wa vitambulisho, kwani kwa sasa watu wengi hawana vitambulisho hivyo. Kwamba tarehe hiyo iliyotangazwa na TCRA haitawezekana, kwa sababu watu ambao hawajasajiliwa na NIDA ni zaidi ya nusu ya watanzania.

Kwa mujibu wa Rais, katika ‘lojiki’ ya kawaida watanzania ni milioni 55, lakini vitambulisho vya taifa vilivyotolewa ni milioni 13 au milioni 14 tu, hivyo unaposema watu wasajili kwa vitambulisho vya taifa wakati NIDA hawajamaliza, maana yake unataka watanzania milioni 20 wasiwe na simu. Rais anasisitiza kuwa hatuwezi kwenda kwa utaratibu huo.

Anaagiza kuwa kama vitambulisho vya taifa havijatolewa kwa watanzania wote, kauli ya watu lazima kusajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya taifa, haitawezekana.

Anasema kazi ya kutoa vitambulisho vya taifa, iende sambamba na kazi ya kusajili simu Lakini, Rais anasisitiza kuwa hajasema watu wasisajili simu zao, bali usajili wa simu usiwahukumu watu ambao hawajapata vitambulisho vya taifa. Vitambulisho visipotolewa kwa watanzania wote, hakuna kuwahukumu, kwasababu hawajasajiliwa.

Kwamba suala hilo la usajili wa laini za simu ni zuri, lakini wizara husika ianze kwa watu walio na vitambulisho. Kwamba wengine ambao hawajapata vitambulisho hivyo, wapewe muda.

Tuna imani suala hili la kusajili laini za simu, linalotekelezwa na TCRA na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ni zuri, kwani kila nchi duniani zinafanya hivyo ili kupunguza uahlifu na ugaidi.

Lakini, kama alivyosema rais, usajili huo wa simu ni vizuri uanze na wale wenye vitambulisho waliopo ambao ni milioni 14 tu. Wengine wapewe muda hadi Desemba au zaidi ya hapo.

Ni wazi kuwa kama agizo la sasa la TCRA na wizara litatekelezwa, mamilioni ya Watanzania wataachwa bila mawasiliano yoyote ya simu, pale laini zao za simu zisizosajiliwa kwa utaratibu mpya zitakapozimwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/993ab3e680000777f1ca2444fa7a42eb.jpg

KWA mara ya kwanza leo dunia inaadhimisha ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi