loader
Picha

Wawili jela miaka 15 kwa wizi wa betri za Bombardier

WAKAZI wawili wa Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, Patrick Chirwa maarufu kwa jina la Boy (42), mkazi wa Lizaboni na Ramadhani Nivya (41), mkazi wa Ruhuwiko wamehukumiwa kwenda jela miaka 15 wote wawili katika kesi ya uhujumu uchumi baada ya kupatikana na betri mbili zinazotumika kuchaji betri zinazotumika kwenye ndege aina ya Bombardier zote zikiwa na thamani zaidi ya Sh milioni 36, mali ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Songea, mkoani hapa, Clofasi Waane ambapo kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 26/2017 ilifunguliwa mahakamani hapo Oktoba, 26, 2017 na washtakiwa wote wawili wakiwa wanakabiliwa na makosa matatu na waliposomewa mashtaka yao walikana makosa yote.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Hamimu Nkoleye uliiambia Mahakama kuwa mnamo Oktoba, 12, 2017 ndani ya uwanja wa ndege uliopo Ruhuwiko washtakiwa wote wawili waliingia kwenye huo uwanja na kuiba betri mbili zinazotumika kuchaji betri zinazotumika kwenye ndege aina ya Bombardier.

Ilielezwa kuwa kitaalamu betri hizo zinatumika kwenye Ami ground power unit (Ami – 2400-55) zenye namba 245203 na zina thamani ya Sh 36, 963,168, ikiwa ni mali ya Shirika la Ndege la Tanzania. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa shitaka la pili kwa washitakiwa wote lilikuwa ni la kuvunja na kuiba.

Mwanasheria Nkoleye pia aliiambia Mahakama kuwa shitaka la tatu lilikuwa likimkabili mshitakiwa wa kwanza, Chirwa ambapo alidai mnamo wa Oktoba 13, 2017 katika njia ya kuelekea Lupapila alikutwa akiwa na betri hizo mbili za kuchajia ndege ikiwa mali ya ATCL.

Hata hivyo washitakiwa wote wawili walikana makosa yote matatu, kabla ya kutiwa hatiani na kupewa adhabu hiyo ya kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 15 jela wote wawili.

Kabla ya Hakimu Waane kusoma hukumu hiyo aliwataka washtakiwa waiombe Mahakama iwapunguzie adhabu ambapo mshitakiwa wa kwanza Chirwa aliyekuwa akitetewa na Mwanasheria wa kujitegemea, Benard Mapunda aliiambia Mahakama kuwa mteja wake ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na pia amekaa mahabusu kwa muda mrefu, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na Mahakama hiyo. Mshitakiwa wa pili, Nivya akiiomba Mahakama impunguzie adhabu akidai anasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu (BP).

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Songea

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi