loader
Picha

JPM ameepusha athari za kutangaza ongezeko la mishahara hadharani

UCHUMI wa Tanzania unakadiriwa kukua kwa asilimia saba tangu Rais John Magufuli aingie madarakani na kuanza kuliongoza taifa hili lenye rasilimali nyingi katika vita ya uchumi.

Hii ni vita ambayo hata yeye mwenyewe Rais aliwahi kukiri kwamba ni vita ngumu. Hata mimi naamini vita ya uchumi inaweza kuwa ngumu kuliko hata vita ya kushikiana silaha! Mpaka sasa vita ya kuimarisha uchumi wa Taifa hili imeendelea kuwa imara na Tanzania kutajwa kuongoza katika nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni dhahiri shahiri kuwa kuimarika kwa uchumi wa Tanzania kunatokana na umoja, upendo, amani na mshikamano walionao Watanzania.

Watanzania wengi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 50 sasa, wamekuwa na kiu, ari na hamu kubwa ya kuona Taifa lao linapiga hatua zaidi chanya kimaendeleo (Positive and sustainable economic growth). Wanajiuliza kama Malaysia wameweza, sisi tunashindwa nini, kama Wachina wameweza kwani wao wana mapembe? Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu, wengi walitazamia kwamba Rais John Magufuli angetumia sherehe hizo kutangaza ongezeko la mishahara hadharani lakini Rais kwa bahati nzuri hakufanya hivyo.

Kwa nini ninasema ni bahati nzuri? Endelea kuwa nami. Baadhi ya wachumi nguli duniani wanaonya kwamba ni kosa kubwa kiuchumi kupandisha mishahara ya watumishi hadharani kama ambavyo imekuwa ikifanyika huko nyuma. Kwa lugha nyingine wanaona kwamba kama kuna haja ya kupandisha mishahara basi hilo lifanywe kimya kimya. Wanafafanua kwamba kupandisha mshahara hadharani athari zake ni kubwa kwa uchumi wa nchi kutokana na kushitua misuli ya virusi vya uchumi (economy virus muscles) kama vile kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, kusababisha mfumko wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha.

Mwanauchumi mmoja alipata kusema: “Taifa likiwa na mwenendo mzuri wa uchumi, viongozi wajiepushe kutangaza misharara mipya hadharani.” Katika falsafa ya uchumi, inaelezwa kwamba mfumuko wa bei (inflation) ukiwa mdogo huku pato la nchi nalo likiwa linaongezeka kistahimilivu (sustainably) ikiwa ni pamoja na kuruhusu ajira kuongezeka pamoja na upatikanaji mzuri wa huduma muhimu za kijamii, basi ongezeko lolote la mishahara kwa wakati huo litakuwa hatarishi kwa uchumi wa Taifa.

Wengi bila shaka wanakumbuka kwamba huko nyuma ongezeko la mishahara inayotangazwa hadharani limekuwa likiandamana na kupanda kwa kila kitu kama vile kodi za nyumba, bidhaa, mafuta na kadhalika. Watanzania ni mashahidi pia kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imekuwa ikiboresha huduma za kijamii nchi nzima, imekuwa ikitoa ajira kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati kama ujenzi wa barabara za juu, reli ya kisasa na katika sekta mbalimbali ikiwepo elimu, afya nk.

Hii ni ishara tosha kuwa kiongozi huyu wa nchi ambaye amekuwa kivutio kikubwa hata kwa watu wa nje ya nchi amedhamiria kwa dhati kulifanya Taifa la Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi imara na mkubwa duniani. Kwa mwendo huu kuna dalili kubwa ya kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda na hasa kama Watanzania tutaendelea kumuunga mkono.

Hivyo, katika ajenda ya kujenga na kuimarisha uchumi wa Taifa na wa wananchi walio wengi, kupandisha mishahara kwa ajili ya watumishi wa umma ambao hawafiki milioni mbili miongoni mwa Watanzania zaidi ya milioni 50 ni kuliingiza Taifa katika janga kubwa kiuchumi. Wananchi watajikuta wanateswa na bei kubwa za bidhaa, fedha yao itaendelea kukosa thamani na maisha kubadilika huku jamii ikikosa mahitaji muhimu ya kibinadamu.

Wachumi wanashauri kwamba cha msingi katika uchumi unaokuwa vizuri, siyo vyema kutangaza ongezeko la mshahara hadharani bali ni kuimarisha ufanisi katika sekta zinazokuza na kusisimua uchumi (economic appetizers).

Wanasema ni muhimu katika kuangalia pia maeneo nyeti yanayosaidia kudhibiti mfumuko wa bei, maeneo yanayoongeza ajira, kukuza pato la Taifa na kurahisisha wananchi kuzifikia huduma muhimu za kijamii kama afya, barabara, elimu, usalama wao na kadhalika. Hakuna ubishi kwamba serikali hii imejitahidi kuboresha sekta zote hizo muhimu kama vile kuongeza bajeti ya afya kutoka Sh bilioni mwaka 2015 hadi, inatoa elimu msingi bure, karibu kila mkoa wa Tanzania ujenzi wa miundombinu unaendelea, usalama wa watu unaimarishwa na kadhalika na kadhalika. Hakika hatuna budi kumpongeza Rais Magufuli kwa kufanikiwa kuruka kihunzi hatari kiuchumi.

Tunaweza kutumia nguvu nyingi na muda mwingi wa kujenga na kuimarisha uchumi wa taifa letu, lakini haichukui hata sekunde moja kubomoa uchumi huo tuliotumia muda mwingi kuujenga na kuuimarisha tusipokuwa makini. Nimpongeze sana Rais kwa kutoharibu misingi imara iliyokwishajionesha katika kila kiashiria tajwa hapo juu katika harakati ya kujenga na kukuza uchumi wa Taifa letu.

Sio mimi nasema bali wale watu wanaotumiwa na mabeberu wangesikia Rais ametangaza ongezeko la mishahara mipya wangekaa vyumbani na kugonga glasi za mvinyo na kushangilia huku wakisema; “wamejinyonga wenyewe. Baadhi yao wanaliombea mabaya Taifa letu hata kwa kujaribu kuwahadaa wananchi wetu ili ikiwezekana waendelee kutunyonya na kipora raslimali zetu kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa miaka mingi.

Ni katika muktadha huo sisi Watanzania tupige magoti na kumwombea kiongozi wetu, Dk Magufuli ili aendelee kuliongoza na kulivusha Taifa hili kwenye uchumi duni au mazingira ambayo ni wachache wanafaidi keki ya taifa hadi kuwa Taifa lenye asali na maziwa kwa wote. Mwandishi wa makala anajiita pia Mchapa kazi na mja anayemwogopa Mungu. Makala haya ambayo hapa imefanyiwa uhariri ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye Blogu ya CCM Mei 2, 2019.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Netho Ndilito

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi