loader
Picha

Waseme wanaosema JPM mkombozi wetu

SIKU chache baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, mtangazaji mmoja alimuuliza mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Patrick Lumumba wa Kenya kama Rais John Magufuli alikuwa ni ‘real deal’ kwa aliyoanza kuyafanya na siyo nguvu ya soda ili kuwaridhisha wapigakura.

Profesa Lumumba alijibu kwamba ‘Magufuli ni real deal’ akimaanisha Watanzania wamelamba dume na akasema ingawa yeye si mtabiri, dunia itashangaa sana kwa jinsi mwanamume huyo atakavyochapa kazi na kusimamia vyema rasilimali za nchi yake kwa faida ya jamii nzima.

Alisema kweli kwani Rais Magufuli ameendelea kuonesha kwamba yuko pale Ikulu, siyo kwa ajili ya kuangalia mustakabali wake na familia yake bali kupigania maslahi ya taifa kwa manufaa ya Watanzania wote. Ingawa kila siku anazidi kuthibitisha hilo, bado kuna Watanzania ambao hawajamwelewa na bado wameshindwa kubadilika na kutambua kwamba hizi ni zama zingine.

Pamoja na Tanzania kumpata rais aliyeingia madarakani akijua hali ilivyokuwa na ni nini anakwenda kufanya, bado unaweza kusikia watu wakimpiga vita na kumkejeli wakati mwingine wakibeba ajenda za mabeberu ili kuonesha kwamba utawala wake ni mbaya au unaodidimiza uchumi. Katika mikutano yake ya hadhara ya hivi karibuni katika mkoa wa Mtwara, Njombe na Mbeya tumeshuhudia namna Rais alivyoendelea kuweka hadharani kwamba yuko makini katika kusimamia rasilimali za nchi na kuhakikisha sekta ya umma unawajibika vilivyo kwa Watanzania.

Ukiweka mbali ziara hizo, bila shaka bado Watanzania wanakumbuka namna Rais Magufuli alivyofanikiwa kuokoa Sh milioni 200 ambazo zilikuwa zitumike kwa kupaka ndege rangi tu.

Hii ni kazi ambayo baadae ilifanyika kwa gharama ya shilingi milioni tano pekee kutokana na jitihada za Rais kukwamisha ulaji huo wa mchana kweupe. Kutokana na kufurahishwa na kazi ile, Rais aliwaongeza wahusika fedha nyingine na kwa hatua hiyo kazi hiyo ikafanyika kwa shilingi milioni kumi tu! Kwa jinsi wahusika walivyokuwa wakijiandaa ‘kupiga’ hizo pesa, unaweza sasa kujua kwa nini mashirika mengi ya umma yalikufa.

Mpaka mimi ninajiuliza hivi Watanzania tumelogwa na nani ambaye hataki kuachilia fahamu zetu tukazama kwenye uzalendo kwa mustakabali wa taifa letu? Ni jambo la ajabu kuona kuwa baadhi ya Watanzania wenzetu bado wameamua kushupaza shingo zao kwa kukataa kubadilika pamoja na juhudi kubwa za Rais wetu anazofanya katika kutokomeza tabia za kifisadi. Hizi ni tabia ambazo zilizoeleka kufanywa bila woga katika awamu zilizopita huku wengi wao wakiachwa bila kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.

Hii ndio ilisababisha baadhi ya watu wakati huo kukatishwa tamaa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakidhani rais yeyote atakayetokana na chama hicho atawalinda mafisadi kwa mtindo uliozoeleka wa ‘huyu ni mwenzetu’ Ni dhahiri kuwa nyakati hizo zimepita na hazipo tena katika awamu hii ya tano, ndio maana Rais Magufuli anachukua hatua kali katika kuokoa rasilimali za nchi zisiende kwenye mikono nyang’au wachache. Haya yote, Rais Magufuli anayafanya kutokana na mapenzi yake mema aliyonayo kwa taifa hili na kwa faida ya Watanzania wote.

Tumeshasikia mara nyingi kauli za Rais akisisitiza kwamba yupo tayari kufa kwa ajili ya maslahi ya Taifa na Watanzania wote huku akiapa kuendelea kupambana na mafisadi wanaokwamisha maendeleo ya taifa letu kama kieleweke. Nakumbuka wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015, nilipokuwa nafanya kampeni, kiongozi mmoja ambae wakati huo alikuwa bado katika utumishi wa umma alisisitiza kuwa kamwe asingeweza kumpigia kura mgombea anayetoka CCM.

Aliamini kwamba kutokana na uozo uliokuwa umekita mizizi kila mahala kiongozi kutoka chama hicho asingeweza kuleta mabadiliko makubwa ambayo wananchi waliyataka. Hata mimi binafsi, ingawa nilikuwa ninamjua fika Magufuli kwamba ‘real deal’, mchapakazi na mwadilifu, lakini sikuwa na uhakika wa asilimia 100 kwamba angeweza kusafisha uoza ndani ya serikali na ndani ya CCM.

Miaka miwili baadae nilipokutana na kiongozi huyo, alinieleza kuwa anajutia kwa nini hakumpigia kura Dk Magufuli huku akisisitiza kuwa kwa sasa anamuunga mkono kwa asilimia 100. Akasema hatua zote anazoendelea kuchukua dhidi ya uozo uliokuwa umeighubika nchi kiasi cha kukatisha tamaa ni za kuungwa mkono na kila mwananchi anayejitambua.

Kiongozi huyo akaendelea kunidokeza juu ya kisa kimoja kilichomkuta. Kwamba siku moja alikuwa kwenye baa moja akijichangamsha akiwa na wenzake kadhaa ambao huko nyuma walimjua kwamba analalamikia ufisadi na ndani ya serikali ya CCM. Akaanza kusifu jitihada za Rais katika kupambana na ufisadi na maendeleo anayoyaleta kwa manufaa ya Watanzania.

Anasema licha ya kueleza kwa mifano mazuri anayofanya Rais, baadhi ya watu aliokuwa akinywa nao pombe walimbadilikia ghafla wakionekana kana kwamba wanaunga mkono ufisadi kuendelea nchini mwetu sambamba na uwajibikaji duni. Anasema waliibuka na madai ya ajabu kwamba sasa hivi hawana pesa wakimaanisha zile walizokuwa wanapata kwa njia isiyo halali, kwa maana ya kwamba wanachotaka ni wao kuneemeka hata kama idadi kubwa ya Watanzania wanataabika! Akaniambia kwamba hilo linaonesha namna baadhi ya watu wachache wasivyotaka mabadiliko katika nchi hii.

Ndugu zangu, Waswahili wanasema katika msafara wa mamba, kenge hawakosekani, kwa hiyo hao ‘kenge’ wachache ni wa kuupuzwa. Kutokana na jitihada anazofanya Rais Magufuli za kusimamia vyema na kwa uaminifu rasilimali za taifa, tumeanza kushuhudia kuboreka kwa sekta karibu zote.

Tunaona miradi mingi ya kimkakati ikifanyika kwa kasi na mara nyingi kwa kutumia pesa za ndani ambazo zamani zilikuwa zikiishia kwenye mifuko ya wachache kama zile Sh milioni 200 za kupaka rangi ndege zilivyodhamiriwa kuliwa na wachache.

Ingawa bado wapo wachache wanaoendelea kukwapua rasilimali za Taifa kutokana na tabia waliyojijengea kwa kipindi kirefu ya uchoyo na ulafi, lakini ninaamini madhali Magufuli anaendelea kuchapa kazi wataaendelea kupungua. Matumaini ni kwamba Magufuli ataendelea kutuongoza katika kipindi kingine cha miaka mitano baada ya 2020, muda ambao bila shaka mafisadi waliobaki watatoweka na kuzoea mabadiliko ya sasa ambayo yanawanufaisha Watanzania wengi na siyo kundi la wachache. Wengi tuna imani kwamba ile tabia ya njia ya mkato, tabia ya mtu kufanya kazi kwa muda mfupi na kuibuka tajiri kinyume na mshahara wake itakoma tu siku moja.

Kwamba sasa kila mmoja atavuna alichopanda, na siyo kuwaibia Watanzania hawa masikini. Shime Watanzania wenzetu mliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali zetu kama hamtaki kubadilika kwa kumsikiliza Rais anachotaka basi mumrudie Mungu wenu ili akate kiu ya tamaa iliyojaa mioyoni mwenu. Nanyi viongozi mlioteuliwa kumsaidia Rais katika maeneo na ngazi mbalimbali msaidieni kwa moyo na dhamira ya kweli na siyo vinginevyo.

Ni kweli wapo viongozi ambao wanachapa kazi kweli kweli bila kuchoka, na wala sioni haya hata kidogo kutoa mfano wa waziri wa nchi, ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo. Kwa kweli, licha ya kuwa waziri kijana lakini anapiga mzigo kwelikweli na kuwa uadilifu. Ni Waziri aliyejipambanua katika uwajibikaji uliotukuka. Waziri huyu hata kwetu sisi wanahabari amekuwa akitupa changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu yetu, kwa vile amekuwa akifanya ziara ambazo kwa siku moja anaweza kutembelea mikoa miwili au mitatu.

Hivyo ukijidanganya kwa kulaza stori yake basi ujue imekula kwako kwani itakuwa imepitwa na wakati. Kutokana na kasi hii ya utendaji wa kazi, Waziri Jafo ameshapata ajali mara kadhaa, lakini Mungu ni mwema, amekuwa akimnusuru kila mara, na Inshallah ataendelea kumnusuru siku zote maadam anayoyafanya ni kwa ajili ya Watanzania.

Nimalizie makala yangu kwa kuwaachia swali ambalo nimekuwa nikijiuliza kwamba hivi Rais Magufuli akimaliza muda wake wa miaka 10 ni nani atakayetosha kuvaa viatu vyake? Sawa, wapo viongozi wengi ndani ya chama tawala na hata ambao bado hawajajifunza na CCM wanaoweza kushika nafasi hiyo ya juu kabisa katika nchi yetu.

Lakini kushika nafasi hiyo ni jambo moja na kuvaa viatu vya Dk Magufuli na vikawaenea ni jambo lingine! Niendelee tu kuwahimiza Watanzania wenzangu kuendelea kumuunga mkono Rais wetu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo amejitoa mhanga kwa ajili yetu kuifanya, na tuendelee kumwombea Mwenyezi Mungu azidi kumwongoza vizuri na pia tuiombee nchi yetu kwa ujumla. Mwandishi wa makala ni mwakilishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) anayeripoti kutokea Morogoro.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Praxeda Mtani

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi