loader
Picha

Kwaheri ya kuonana Mengi

Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk Reginald Mengi (77) anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwao Machame mkoani Kilimanjaro leo.

Tunaungana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyesema kuwa kifo cha Dk Mengi ni pigo kubwa taifa na kwa kampuni alizomiliki na kuziongoza.

Kabudi anasema serikali imeguswa mno na msiba huo mkubwa, kwa kuwa Mengi alifanya mambo mengi.

Kwa mfano kwenye sekta ya uchumi, alianzisha kampuni za IPP, sekta za gesi, madini na mafuta na alichangia sekta za kilimo, afya na kutoa ajira kwa mamia ya watu.

Kwa mujibu wa Kabudi, Dk Mengi alikuwa chachu ya kuhamasisha wawekezaji wazawa, kufanya uwekezaji na biashara mbalimbali nchini. Kwamba alishawishi mabadiliko ya sera ya uchumi na kutoa majawabu ya kuboresha sera hizo.

Dk Mengi alikuwa chachu ya sera ya viwanda kwa kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kati, kwa sababu alikuwa na mikakati mbalimbali ya kusaidia uchumi wetu, kwa kutaka kuwekeza kwenye uundaji wa magari kwa kushirikiana na Kampuni ya Young Sung iliyopo Korea na kuanzisha viwanda vya dawa za binadamu.

Kwa upande wa kijamii, Dk Mengi atakumbukwa kwa upendo wake, ukarimu na huruma kwa wanyonge, walemavu na wahitaji. Wote hao aliwagusa kwa maisha yao mbalimbali.

Hali kadhalika, Dk Mengi alikuwa mdau mkubwa wa mazingira na alihamasisha upandaji wa miti kwenye misitu inayozunguka mlima Kilimanjaro na yeye mwenyewe alipanda miti zaidi ya milioni 24 katika eneo hilo.

Dk Mengi alihakikisha kuwa sekta binafsi zinakuwa injini ya uchumi. Ni mtu aliyebarikiwa kuwa na utajiri, uzalendo na utaifa wa hali ya juu, kwa kusaidia watu na kuwa mshauri wa masuala ya kiuchumi na biashara na kuwa daraja kwa sekta binafsi na serikali.

Balozi Juma Mwapachu anatukumbusha kuwa Mengi alikataa umasikini uliopo nchini kutokana na raslimali nyingi zilizopo, hivyo alihakikisha kunakuwepo sera bora za uchumi, jamii na afya.

Kwa mujibu wa Mwapachu, Dk Mengi alikuwa na fikra pevu kwenye masuala ya ujasiriamali na alikuwa akikutana na wataalamu mbalimbali wa sayansi na teknolojia kwa ajili ya kugeuza fikra za vijana kutoka kuajiriwa hadi kujiajiri, jinsi ya kupata mitaji na kuhimiza mitaala ya elimu iinue ujasiriamali.

Kwa hakika, Mengi amegusa maisha ya Watanzania wengi na wa rika zote.

Ni mtu ambaye ameacha alama kubwa kwa Watanzania. Kwa heri Mengi. Kwa heri ya kuonana!

RAIS John Maguful amemaliza ziara yake mkoani Katavi kwa kuzindua ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi