loader
Picha

Mshahara na maadili

Mwanazuoni, Joseph Zimmerman katika makala yake ya mwaka 1982 kuhusu maadili ya utumishi wa umma, alisema mshahara wa kutosha ni moja kati ya mambo muhimu, yanayoweza kukuza maadili katika utumishi wa umma.

Ni ukweli usiopingika kwamba, watumishi wa umma wanapokuwa na mishahara ya kutosha, inakuwa rahisi zaidi kwao kujiepusha na utafutaji wa vipato vya ziada kinyume na maadili.

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa mshahara wa kutosha peke yake hauwezi kumfanya mtumishi wa umma awe mwadilifu. Wako watumishi waadilifu wenye mishahara midogo na watumishi wasio waadilifu wenye mishahara mikubwa.

Alichosisitiza Zimmerman wakati huo ni kwamba, mshahara wa kutosha unaweza kuhamasisha watu wengi wenye sifa kutafuta ajira kwenye utumishi wa umma na hivyo, kutoa nafasi kwa serikali kuchagua watumishi wenye maadili.

Kwa bahati nzuri, watu wanaotamani kuajiriwa katika utumishi wa umma nchini kwetu ni wengi sana na kwa maana hiyo, upo uwezekano mkubwa wa kufanya mchujo mkubwa, ili kubaki na watumishi waadilifu zaidi.

Ili kuwa na uhakika wa kupata watu waadilifu ni lazima juhudi za serikali katika kujenga kizazi chenye kuheshimu maadili shuleni, ofisini na katika jamii zetu kwa jumla ziendelee kuungwa mkono.

Kimsingi, zipo juhudi nyingi za serikali, zinatotakiwa kuungwa mkono.

Kwa mfano, Rais John Magufuli, alipata kumuelekeza Katibu Mkuu Kiongozi kumuandikia barua Meneja wa TRA katika Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Lameck Mbibo kutokana na kitendo chake cha kukataa hongo wakati akitekeleza majukumu yake.

Machi 31, 2019 yaani muda mfupi baada ya agizo hilo, Rais alimteua Mbibo kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA. Vilevile, mshahara wa kutosha unaweza kusaidia sana kujenga uadilifu kwa watumishi wa umma.

Hata hivyo, kuwa na mshahara wa kutosha siyo lazima uwe mkubwa kwa sababu, mshahara unaweza kuwa mdogo na ukatosha na pia unaweza kuwa mkubwa lakini usitoshe. Ili mshahara wa mtumishi wa umma uweze kutosha, lazima kuwe na mikakati ya kutosha kwa upande wa serikali (mwajiri) na mtumishi (mwajiriwa).

Kwa upande wa serikali, kumekuwa na jitihada kubwa kuboresha mishahara ya watumishi wa umma kwa kuzingatia matarajio ya watumishi wenyewe kulingana na hali halisi ya maisha, ulinganifu baina ya taasisi na taasisi kulingana na kazi zinazofanywa na watumishi wenye taaluma na shughuli zinazofanana na pia, uwezo wa serikali kulipa mishahara hiyo.

Aidha, serikali imeweza kupunguza mzigo mkubwa wa matibabu ya watumishi wa umma kwa kuanzisha mfuko wa bima ya afya ambao umekuwa na mafanikio makubwa hadi sasa.

Hatua hii inaenda sambamba na kuondoa malipo ya ada kwenye shule za msingi za serikali ikiwa ni pamoja na kutoa wito kwa shule za binafsi kuangalia ukubwa wa ada zake.

Kwa upande mwingine, watumishi wa umma wanaweza kuweka mikakati mizuri ili mishahara wanayopata itoshe. Moja ya mikakati hiyo ni kwa watumishi vijana kuchukua muda wa kutosha kupanga ukubwa wa familia zao.

Mipango mingi ya serikali kwa watumishi wa umma inaangalia zaidi mwenza mmoja wa mtumishi, watoto wanne na wazazi.

Kwa mfano, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unahudumia mtumishi na mwenza wake na wategemezi wanne. Kwa tamaduni zetu, ukubwa wa familia vilevile unaweza kuongezeka kutokana na nia ya kusaidia ndugu na jamaa.

Pamoja na kwamba hili ni jambo zuri na wengi wamefaidika kwa kupitia utamaduni huu, bado mtumishi wa umma anatakiwa kutambua hali yake halisi ya kipato na kubainisha kipi anaweza kufanya na kipi hawezi ili aweze kuweka mambo yake sawa.

Vilevile, ni vizuri mtumishi wa umma akajenga utamaduni wa kutengeneza bajeti nzuri ili kuhakikisha kuwa, kuna uhusiano mzuri kati ya mapato yake na matumizi yake.

Matumizi yake lazima yajikite kwenye mambo ya msingi zaidi na kuepuka matumizi yasiyo na ulazima na matumizi yanayoweza kusababisha matumizi mengine makubwa zaidi.

Mfano mzuri hapa ni hamu ya kununua gari badala ya kutumia usafiri wa umma kama kipato ni kidogo au hata kama kipato ni kikubwa, kununua gari lenye matumizi makubwa ya mafuta, gharama kubwa za vipuli na matengenezo na uimara mdogo.

Kitu kingine kinachoweza kuleta usumbufu ni kwa mtumishi wa umma kuelemewa na madeni.

Mshahara wa mtumishi wa umma hauwezi kutosha hata kidogo kama sehemu kubwa itakuwa inatumika kila mwezi kulipia madeni.

Kwa kutambua hilo, serikali iliweka kiwango cha chini kinachotakiwa kubaki baada ya marejesho ya mikopo mbalimbali na kanuni za maadili ya utumishi wa umma zimewaasa watumishi wake wote kujiepush na madeni yasiyo ya lazima.

Pamoja na yote hayo, watumishi wa umma hawakatazwi kutunza sehemu za mapato yao na kuwekeza katika maeneo yanayoweza kuwaletea faida na hivyo, kuwaongezea vipato.

Pamoja na kutokatazwa, bado watumishi wa umma wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanafanya uwekezaji wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ili pamoja na mambo mengine waweze kuepuka migongano ya maslahi.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Dk Alfred Nchimbi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi