loader
Picha

Athari za mifuko ya plastiki kwa binadamu, mazingira

HIVI karibuni serikali ilipiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usafi rishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko aina ya plastiki maarufu kama ‘rambo’ inayotumika kubebea bidhaa.

Katazo hilo lililotangazwa bungeni jijini Dodoma Aprili 9, 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tayari limeanza kutekelezwa na ifikapo Juni mosi, 2019 ni mwisho wa matumizi yote ya mifuko hiyo.

Katika kusimamia katazo hilo na kuhakikisha linatekelezwa kwa ufanisi, Ofisi ya Makamu wa Rais yenye dhamana ya kusimamia utunzaji wa mazingira imeunda kikosi kazi ambacho kinaundwa na taasisi mbalimbali za serikali.

Kuna msemo wa Kiswahili kuwa: ‘Heri kuzuia kuliko kuponya,’ hivyo Serikali imechukua hatua madhubuti za kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ili kuepusha athari mbalimbali za kiafya zinazoendelea kujitokeza. Ni dhahiri kuwa, wananchi wengi wamekuwa na mazoea ya kutumia mifuko ya plastiki kubebea bidhaa mbalimbali hususan za vyakula bila kujali athari za mifuko hiyo kwa afya za binadamu, wanyama na mazingira.

Mifuko hii baada ya matumizi imekuwa ikitupwa ovyo na hata ikitupwa kwenye mashimo ya taka huweza kupeperushwa kwa upepo na kusambaa hivyo husababisha uchafuzi wa mazingira. Hata ikichomwa moshi wake una athari kwa binadamu.

Pia mifuko ya plastiki haiwezi kuoza kwa haraka katika mazingira wanadamu walipo kwani inakadiriwa kuweza kudumu hadi zaidi ya miaka 500 na hivyo kuleta athari za muda mrefu na hata ikichomwa huleta madhara ya kiafya. Madhara mengine yanayoweza kutokea ni kusababisha mafuriko katika maeneo ambayo kuna mifereji kutokana na kuziba kwa miundombinu ya majitaka na mifereji ya mvua.

Kama ambavyo binadamu wanavyoweza kupata athari kutokana na matumizi ya mifuko hiyo hususan katika kubeba vyakula, pia wanyama nao huweza kuathirika. Je, wanyama wanawezaje kuathirika? Wanyama mbalimbali, ikiwemo mifugo kama ng’ombe, mbuzi au kondoo wanaweza kufa wanapoila na kuimeza mifuko hii.

Katazo hili linatolewa kauli na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba anayesema serikali itahakikisha linakuwa na nguvu kisheria. Anasema serikali itaandaa kanuni za katazo hilo zitakazotangazwa katika gazeti la serikali chini ya Sheria ya Mazingira na kutoa adhabu ya faini au kifungo kwa mtu atakayekiuka utaratibu uliowekwa.

Akizungumzia ushirikishwaji, Waziri Makamba anabainisha kuwa katazo hilo la mifuko ya plastiki limekuwa shirikishi na hatua iliyotangazwa na Waziri Mkuu si ya kushtukiza. Anasema kuwa, ofisi yake tayari ilisharatibu mikutano katika maeneo kadhaa nchini na kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu katazo hilo la mifuko ya plastiki. Waziri Makamba anasisitiza kuwa serikali itasimamia kikamilifu katazo hilo ifikapo tarehe hiyo ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakilalamika kipindi kilichotolewa ni kifupi.

Itakumbukwa kuwa, awali serikali ilitangaza kuzuia matumizi yote ya mifuko ya plastiki kuanzia Januari Mosi, 2017. Hata hivyo baada ya mashauriano na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na umma ilikubali kusogeza mbele hadi Desemba 31, 2017 ili kutoa muda kwa wajasiriamali, umma na CTI kujiandaa na utekelezaji wa katazo hilo. Kwa kutambua umuhimu na ukubwa wa jambo hilo, Serikali haikuanza kulitekeleza Januari mosi, 2018 ili kutoa muda wa ziada kwa wadau hao kujipanga zaidi.

Hivyo kutokana na hilo katazo lilisogezwa mbele hadi kufikia Juni mosi, 2019 kama ambavyo imetangazwa na kutoa muda wa kutosha wa matayarisho. Serikali imeunda kikosi kazi kitakachoratibu utekelezaji wa zoezi hilo ambacho kinajumuisha watendaji kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Mapato Tanzania na Idara ya Uhamiaji.

Taasisi nyingine ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Hata hivyo, Waziri Makamba anawaondoa hofu wananchi kwa kusema kuwa katazo hilo la mifuko ya plastiki halitahusu baadhi ya vifungashio vya bidhaa zikiwemo maziwa, mikate. Vifungashio vingine ni vya pembejeo za kilimo, ujenzi, dawa na baadhi ya vyakula kama korosho na vinywaji vikiwemo maziwa ambavyo ni lazima vikidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Habari katika Ofisi ya Makamu wa Rais.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Robert Hokororo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi