loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Marufuku mifuko ya plastiki itaongeza ulinzi wa mazingira

MEI 3, mwaka huu, Tanzania itaandika historia mpya ya mabadiliko katika matumizi ya mifuko mbadala ikiachana na mifuko ya plastiki. Kwa kipindi kirefu mifuko hii imekuwa ikitajwa na kulalamikiwa kuwa moja ya vyanzo vikuu vya uharibifu wa mazingira nchini na duniani kwa jumla.

Ni historia mpya kwani licha ya uamuzi wa kuachana na mifuko hiyo kutangazwa mara kadhaa katika siku za nyuma, utekelezaji wake haukuwahi kufanywa hadi ulipotangazwa upya bungeni hivi karibuni. Katika tangazo lake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisisitiza kuwa, mwisho rasmi wa matumizi wa mifuko hiyo nchini ni Mei 31 huku Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) likiwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

Katika kuhakikisha suala hilo linatekelezeka baada ya kutangazwa kwake, serikali iliitisha mkutano wa wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji wa mifuko mbadala na wazalishaji wa malighafi kwa ajili ya utengenezaji wa mifuko hiyo. Mkutano huo ulilenga kupata mawazo yao na kujadili fursa mpya za ujio wa mifuko mbadala ili kuzitumia kujiinua kiuchumi.

Ulitumika pia kuwakumbusha wazalishaji hao wa mifuko ya plastiki mintarafu mipango inayosisitizwa na serikali kama mikakati endelevu ya kukabiliana na kasi ya uharibifu wa mazingira sambamba na kulinda viumbe hai wa majini. Kwa mujibu wa tafiti za kimataifa, ifikapo mwaka 2050, kutakuwa na mifuko mingi ya plastiki baharini kuliko samaki.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Januari Makamba anasema hatua ya kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo pamoja na mambo mengine, itasaidia kuokoa mazingira nchini hasa ikizingatiwa kuwa, baadhi ya nchi za Afrika ya Mashariki zikiwemo Kenya na Uganda tayari zimeachana na matumizi ya mifuko hiyo. Ukiacha mataifa hayo, Zanzibar pia ilishaachana na matumizi ya mifuko hiyo na hivyo kufanya mkakati huo uliochukuliwa na Tanzania Bara sasa, kuwa kama hatua yake muhimu katika kutekeleza kwa vitendo sualoa hili.

Makamba anawataka wazalishaji wa malighafi karatasi zinazotumika katika utengenezaji wa mifuko hiyo na bidhaa nyingine, kutumia fursa ya mabadiliko hayo kuzingatia hatua mbalimbali zitakazofanikisha azma hiyo, ikiwa ni pamoja na uzalishaji malighafi sahihi za utengenezaji wa mifuko hiyo zitakazoendana na viwango vinavyotakiwa ili kuepusha soko la mifuko isiyo na ubora.

Hadi sasa, mzalishaji wa kuaminika wa malighafi za karatasi zinazotarajiwa kuzalisha mifuko hiyo ni kiwanda cha ‘Mufindi Paper Mills’ (MPM) maarufu Mgololo kilichopo Mafinga mkoani Iringa. Meneja Msaidizi wa Mgololo, Gregory Chogo anasema kiwanda hicho kimejiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa malighafi ya karatasi kwa wazalishaji wa mifuko mbadala wanaozihitaji.

Chogo anasema kiwanda hicho kinao uwezo mkubwa wa kuzalisha karatasi za kutosha kwa ajili ya kutengenezea mifuko hiyo na kukidhi mahitaji ya soko la hapa nchini huku akitolea mfano kuwa katika idadi yote ya karatasi wanazozizalisha ni asilimia 25 pekee ya karatasi zinatumika nchini huku kiasi kinachobakia kikisafirishwa kwenda nchi za nje kutokana na kukosa soko la uhakika nchini.

Kwa msingi huo anasema watengenezaji wapya wa mifuko hiyo na walio katika mikakati ya uzalishaji wa mifuko hiyo, waunge mkono azma hiyo ya serikali mintarafu ujio wa matumizi mifuko mbadala. Anasema hili litafanikiwa kwa kuzalisha mifuko yenye ubora ambayo kimsingi, itatokana na matumizi ya karatasi zenye viwango zikiwemo zinazozalishwa na kiwanda hicho.

Meneja msaidizi huyo wa kiwanda anasema wakati mifuko mbadala inatarajiwa kuanza kutumika hususani baada ya kusimamishwa kwa mifuko ya plastiki, zipo kila dalili za soko kujaa mifuko ya aina tofauti ikiwemo iliyozalishwa kwa kutumia karatasi zisizo na ubora na hivyo, kutia dosari mkakati huo wa serikali wa matumizi ya mifuko mbadala (karatasi).

“Kuna kila dalili soko la mifuko hiyo kuvamiwa na mifuko iliyotokana na malighafi kutoka katika madampo na hata mifuko iliyotokana na ubebaji wa saruji, kitu ambacho ni hatari kiafya.” “Kikubwa, tunapoenda kutekeleza hatua hii muhimu ni jukumu la kila Mtanzania kuzingatia usalama na matumizi ya karatasi sahihi,” anasema Chogo. Anasema hakuna sababu ya wazalishaji wa mifuko hiyo kutumia karatasi zisizo na ubora kwani kuna uzalishaji wa kutosha wa karatasi hizo.

Kwa mujibu wa Chogo, uwezo wa kiwanda hicho kuzalisha karatasi ni tani 4,500 kwa mwezi na kwamba, kiwango hicho kinaweza kuongezeka kwa kadri ya mahitaji. “Hatupendi kusafirisha karatasi hizi kwenda nje ya nchi, isipokuwa tunafanya hivyo kutokana na kutokuwepo kwa soko la uhakika nchini… Tunaamini kupigwa marufuku kwa mifuko hiyo kutaongeza soko la karatasi zetu,” anasema.

Aidha katika mkutano huo, Makamba aliwakumbusha wadau hao kuwa kwa sasa Taifa linajielekeza katika kupokea mawazo ya wajasiriamali mbalimbali wa uzalishaji wa mifuko mbadala, kama utekelezaji wa agizo hilo ambalo awali lilikuwa lifanyike Mwaka 2016, kabla ya kutolewa kwa ombi na wamiliki wa viwanda kuomba kusogezwa muda. Anasema ombi la wazalishaji hao liliishia Desemba 31 mwaka 2017 ingawa utekelezaji wake ulichelewa kutekelezwa hadi wakati huu ambapo serikali imeamua kuzuia rasmi mifuko hiyo ikiwa ni miezi 19 tangu ombi hilo lilipotolewa.

Inaelezwa kuwa, muda huo ulitosha kwa wazalishaji na wauzaji wa mifuko ya plastiki kujipanga kwa uzalishaji na biashara mbadala. Anafafanua kuwa, mifuko iliyopigwa marufuku kupitia agizo hilo ambalo utekelezaji wake unaanza Juni Mosi, mwaka huu ni inayotumika kubebea bidhaa na siyo inayotumika kwa vifungashio vya bidhaa kama korosho, maziwa na nyingine za kilimo na viwandani zikiwamo dawa. Kwa mujibu wa Waziri Makamba, tayari zimeweka kanuni mbalimbali za kisheria zitakazosaidia kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo zilizoandaliwa na wanasheria wa Wizara na NEMC.

Kanuni hizi kimsingi, zitaanza kutumika Juni mosi dhidi ya wazalishaji, wafanyabiashara pamoja na wananchi watakaokutwa na mifuko hiyo. “Kimsingi adhabu zitakazowahusu wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa mifuko na watumiaji zitahusisha faini, vifungo vya jela au vyote kwa pamoja kulingana na ilivyoelezwa na kwa kuzingatia matakwa ya kanuni hizo,” anasisitiza.

Katika utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa mifuko hiyo, serikali imejipanga kushirikiana na vyombo vyote ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na viwanja vya ndege ili kupambana na uingizaji na usafishaji wa mifuko hiyo ndani ya nchi na katika mipaka yake yote ili kudhibiti udanganyifu.

Anawataka Watanzania kuanza kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki na kujiandaa na mifuko mbadala ili kulilinda Taifa dhidi ya uharibifu wa mazingira na hivyo kuungana na mataifa mengine duniani sambamba na kutekeleza mpango wa kimataifa wa kudhibiti mifuko hiyo.

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi