loader
Picha

Mafia; kisiwa chenye utulivu na ‘pepo’

UMEWAHI kusikia kuhusu uwepo wa samaki mkubwa kabisa duniani aina ya papa potwe (whale shark) mwenye urefu unaofi kia mita 18? Na kwamba, samaki huyu akiwa mdogo huwa na kimo cha basi dogo la abiria! Kwa mujibu wa watafiti wa bahari, samaki hawa hupatikana maeneo machache duniani, na ni miongoni mwa viumbe walio hatarini kutoweka.

Moja ya maeneo wanayopatikana ni kisiwani Mafia. Kisiwa cha Mafia kilichopo karibu na mlango wa Mto Rufiji, Kusini mwa Tanzania. Sehemu nyingine ni nchi za Mexico na Philippines. Hata hivyo, Mafia ni miongoni mwa maeneo yaliyo nyuma zaidi kimaendeleo nchini, japo kinaendelea kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kihistoria. Ingawa maeneo ya kuvutia ya mazingira ya bahari yametokea kujulikana zaidi, hasa baada ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Bahari (Mafia Island Marine Park – MIMP) na Maeneo Tengefu, habari nyingine kuhusu kisiwa hiki zimekuwa adimu kupatikana.

Unapotafuta habari za kisiwa hiki, hasa kwenye mitandao ya intaneti kuhusu utalii, utaishia kupata taarifa za vivutio vya utalii pekee ambavyo vinajenga sura ya kisiwa hiki kuwa ni pepo ya watalii, na hata watalii wenyewe hawatoi picha sahihi ya mambo yalivyo. Ndiyo maana baadhi ya mawakala wa utalii hujenga picha ya kisiwa hiki kuwa ni kisiwa cha utulivu na ‘pepo’ isiyojulikana iliyo nyuma miaka 30 kimaendeleo ukilinganisha na Zanzibar. Japo kisiwa hiki kinaonekana kuwa nyuma kimaendeleo, lakini inasemekana kuwa hakijachafuliwa wala kuathirika na maendeleo ya utandawazi duniani.

Hali hii inawafanya mawakala wa utalii ‘kukiuza’ kisiwa hiki kwa watalii wakilenga zaidi kwenye fukwe na vivutio vya baharini kama vile uzamiaji, aghalabu kuwepo kwa maelezo yahusuyo wenyeji ambao kwa kifupi huelezewa kuwa ni wacheshi, wavumilivu na wakarimu. Kwa mujibu wa tovuti ya www.mafiaisland. com/history/people1.htm, wamethubutu kutumia maelezo ya Kisiwa cha Mafia ya mwaka 1896 ya mwanajiografia wa Kijerumani kuelezea maisha yalivyo hivi sasa kisiwani hapo, kana kwamba hakuna mabadilko yoyote yaliyotokea hadi sasa.

Maelezo kama hayo hayaoneshi picha halisi ya kisiwa hiki ilivyo, japo kisiwa hiki hakikujitenga na mabadiliko ya kihistoria, kwani kimekuwa sehemu muhimu ya mabadiliko hayo kwa kiasi cha miaka elfu moja sasa. Kwa hali hii wakazi wengi wa kisiwa hiki wameendelea kuwa masikini wa kupindukia, huku bei ya zao kuu la nazi ikishuka kwenye masoko ya nje na ya ndani, kwa mujibu wa mtandao wa uchumi. Mtandao wa www.utalii. com/Mafia_Island/Mafia_Island. htm unasema mawakala wa utalii wamegundua kuhusu hila za upotoshaji huo na kuhakikisha kuwa watalii wanapata picha ya utulivu wa kisiwa hiki, huku wakibainisha kuwa, ingwa wakazi wa kisiwa hiki ni Waislamu lakini si wale “wenye msimamo mkali”.

Nao mtandao wa www. tourismconcern.org.uk, unasemwa katika miaka ya karibuni, mwamko wa utalii unaozingatia uhifadhi wa mazingira umeongezeka, na hivyo kujali maisha ya wenyeji na maeneo yanazunguka sehemu hiyo ya utalii. Kama nilivyoeleza awali, pamoja na changamoto nyingi zinazokikumba kisiwa hiki, bado haziondoi ukweli kuwa Kisiwa cha Mafia kina utajiri wa samaki wakubwa aina ya Papa Potwe. Kutokana na na umuhimu wao, wavuvi pamoja na wahifadhi wa bahari wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kuwalinda.

Ofisa Utalii katika Hifadhi ya Bahari Mafia, Humphrey Mahudi anasema wamekuwa wakishirikiana na wavuvi kuhakikisha wanawalinda samaki hawa adimu walio hatarini kutoweka. Wavuvi kwa upande wao, wametengeneza vikundi vya ulinzi shirikishi na jukumu la kwanza ni kuwalinda samaki hawa adimu. Hii inatokana pia na asili ya samaki hawa ya kutembea na makundi ya samaki wengi wadogo, hivyo kuwa fursa muhimu kwa baadhi ya wavuvi.

Baadhi ya wavuvi akiwemo mwenyekiti wa ulinzi shirikishi kwa rasilimali za bahari, Said Kombo, wanabainisha kuwa samaki hawa hawana msimu kwao, kwani huwaona kila siku. Katika maeneo ya ufukwe wa Mafia Mjini, inasemekana kuwa kuna wakati samaki hawa huonekana kwa uwazi hata unapokuwa ufukweni. Wavuvi hawa wanasema kuwa mara nyingi hukutana na samaki hawa na wakati mwingine hulazimika kuwaachia samaki waliowavua ili wamwache kwa kuwa hawataki kumdhuru.

Kwa mfano, akivuta nyavu za wavuvi na asiweze kujitoa basi wavuvi hulazimika kuwasamehe wale samaki wote waliowavua na kumwachia aende zake. Mbali na jitihada zinazofanyika, bado samaki hawa wanakumbwa na hatari kubwa kutokana na shughuli za uvuvi, na kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa, kizazi kinachokuja kitaishia kusoma historia kuwa kulikuwa na samaki wakubwa duniani. Hata hivyo, kitu cha kushangaza kwa samaki hawa ni kwamba, licha ya ukubwa wao, hujulikana pia kama ‘Papa wema’ kwa ukarimu wao, kwani huwa na tabia ya kuwafuata wavuvi na watalii wanapokuwa ndani ya maji na hucheza nao.

Kwa kipindi cha mwaka mmoja, samaki aina ya Papa Potwe huweza kusafiri umbali wa hadi kilomita 10,000. Watafiti wanasema kuwa Papa Potwe wanaopatikana katika Kisiwa cha Mafia hubaki eneo moja kwa muda mrefu. Maelezo haya yanabainishwa katika makala ya National Geographic na mtafiti mmoja kutoka nchini Marekani, Simon Pierce anayesema Papa Potwe wa Kisiwa cha Maafia huwa hawaendi mbali na inakuwa kama wanawatembelea rafiki zao wa zamani. 0685 666864 au bjhiluka@ yahoo.com

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi