loader
Picha

Polisi Tanzania yarudisha heshima ya soka Kilimanjaro

UNAPOZUNGUMZIA soka ukanda wa Kaskazini, unajumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, ambayo kiujumla ilipoteza mwelekeo katika gurudumu la ushiriki wa soka katika ngazi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mkoa wa Kilimanjaro umetegua kitendawili hicho baada ya Polisi Tanzania kufanikiwa kuingia Ligi Kuu, mikoa ya Arusha na Manyara imekuwa ikiendelea kukosa timu katika daraja hilo la juu licha ya kuwa na timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, ambazo ni Arusha FC na Arusha United. Katika mapinduzi makubwa yaliyofanyika ni timu ya Polisi Tanzania yenye maskani yake mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ilipambana kuhakikisha inarudisha heshima ya mkoa iliyopotea kwa miaka 27 kwa kukosa timu inayoshiriki kucheza Ligi Kuu soka Tanzania Bara baada ya Ushirika kushuka na kupotea kabisa mwaka 1992.

KUTINGA LIGI KUU

Mei 4 mwaka huu, ilikuwa shangwe kubwa katika mji wa Moshi baada ya maafande wa Polisi Tanzania kufanikiwa azma yao ya kutinga kucheza Ligi Kuu msimu ujao wa mwaka 2019/2020 pale walipoichakaza Boma FC kwa mabao 2-1 mchezo uliopigwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Ushirika.

Mabao ya ushindi yaliwekwa nyavuni na mchezaji Patrick Madadi dakika 13 na 34 huku Boma ikifunga kupitia kwa Ramadhan Abdallah dakika ya 90. Ushindi huo uliiwezesha Polisi Tanzania kumaliza ligi hiyo ikiwa kileleni kwa kujikusanyia jumla ya pointi 47 nyuma ya wapinzani wao Pamba FC kwa pointi 42 sawa na Geita Gold, ambazo zitaenda kuchuana katika hatua ya mwisho ya nchujo kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu kuungana na Polisi.

POLISI TANZANIA

Ni baada ya agizo la Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lililoelekeza kila taasisi au kampuni kuwa na timu moja katika mchuano ya Ligi Kuu ndipo Jeshi la Polisi nchini likaamua kuja na timu moja ambayo italiwakilisha. Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Geofrey alisema katika kutekeleza hilo, Jeshi la Polisi lilivunja timu zake zote na kuziunganisha pamoja na kuita Polisi Tanzania, ikitekeleza agizo la kila taasisi kuwa na timu moja.

“Baada ya hapo tuliamua kuja Mkoa wa Kilimanjaro na hii ni kutokana na kuwa timu ni ya Makao Makuu, hivyo ikaelekezwa iletwe Moshi kama maskani yake na ikizingatiwa Moshi ndio chimbuko la askari wote, huduma zote tungezipata tukiwa hapa,” alisema Geofrey. Alisema baada ya mabadiliko hayo sasa kuwa Polisi Tanzania, timu hiyo haikufanya vizuri katika msimu wake wa kwanza wa mwaka 2017/2018 na ikajipanga tena kwa msimu wa mwaka 2018 /2019 na hii ni kutokana na kuimarisha uongozi na kufanikiwa kutimiza malengo yao.

MIKAKATI MIKUBWA

Naye Mtendaji Mkuu wa timu ya Polisi, Robert Munisi alisema mzunguko wa kwanza hawakufanya vizuri, hali iliyosababisha kubadilisha benchi zima la ufundi, ambalo liliongozwa na kocha Mbwana Makata pamoja na uongozi mzima uliosababusha kupanda daraja. “Mikakati ni kuwa mipango yetu ni kuhakikisha mwaka wa kwanza lazima tunapambana kubaki Ligi Kuu mwaka wa pili kubaki na mwaka wa tatu kuwania ubingwa wa ligi,” alisema Munisi.

Naye Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata alisema azma yao ya kupanda Ligi Kuu ilitimia ikizingatiwa aliichukua timu ikiwa katika nafasi ya saba hivyo walipambana kwa ushirikiano wa pamoja na uongozi wa timu, mashabiki wote wa mkoa Kilimanjaro.

“Mkataba wangu umeshaisha baada ya kuipandisha timu vinginevyo tunaweza kukaa mezani na kuzungumza kuhusu mkataba mwingine, kama nikisaini tena mkataba tunaweza tena fanya usajili uliokuwa bora ili kuweza kuleta ushindani,”aliongeza Makata. “Nawashukuru wote kwani haikuwa kazi rahisi Ligi Daraja la Kwanza inahitaji mpira wa matokeo zaidi utumie nafasi na ucheze kwa majukumu zaidi na sisi kila mechi ilikuwa ni fainali zaidi,” alisema Makata.

CHAMA CHA SOKA KRFA

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), Goodluck Moshi alisema kupanda kwa timu hiyo ni mafanikio kwa wana Kilimanajro, kwani ni takribani miaka 27 mkoa ulikosa timu ya Ligi Kuu hivyo hivi sasa wapenzi wa soka waendelee kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika ligi hiyo.

“Hivi sasa tunajipanga kuhakikisha tunakutana na uongozi wa Chuo cha Ushirika ili kukaa na Mkuu wa Mkoa na Manispaa kwa pamoja kuangalia namna ya kuuboresha uwanja huo wa Majengo ili kuona namna gani uwanja utafanyiwa marekebisho ili uwe katika hadhi ya kuchezewa michezo ya Ligi Kuu.

Alieleza kuwa hivi sasa kama KRFA itaendelea kushirikiana na wananchi kwa ujumla kuhakikisha timu haishuki na kuongeza juhudi zaidi kupata timu itakayo cheza Ligi Daraja la Kwanza ili kuongeza msisimko wa Ligi Kuu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira aliipongeza timu hiyo ya Polisi Tanzania na kusema kama mkoa utaendelea kushirikiana nao kama ilivyokuwa katika michuano ya Daraja la Kwanza. “Tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha Uwanja wa Ushirika na viwanja vingine vinaboreshwa ili kusiwe na kukwama na tunawaomba wafanyabiashara mbalimbali mkoani Kilimanjaro kuiunga mkono timu kwa kila namna ili iendelee kufanya vizuri Ligi Kuu,” alisema Mghwira.

MASHABIKI WANENA

Mashabiki mbalimbali mkoani Kilimnajro waliipongeza timu hiyo na kusema kwa hatua hiyo kubwa ya kuingia Ligi Kuu huku wakiutaka uongozi wa timu hiyo uweke mikakati na mipango mipya . Mmoja wa mashabiki, Daudi Enyimba alieleza kuwa timu hiyo iungwe mkono ili iweze kufanya vizuri Ligi Kuu na kuweka mipango itakayowawezesha kuleta mapinduzi makubwa pia iweze kuangalia katika suala la usajili na mshikamano waliouonesha uendelee.

Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza ilipangwa katika makundi mawili A na B, ambapo Kundi A lilijumuisha timu za Namungo, Mlale, Mbeya Kwanza, Njombe Mji, Friends Rangers, Reha, Majimaji FC, Mufindi United, Ashanti United, Dar City na Kiluvya United. Kundi B lina timu za Polisi Tanzania, Pamba FC, Geita Gold, Boma FC, Mashujaa FC, Arusha United, Rhino Rangers, Dodoma, Green Warriors, Transit Camp, Arusha FC na Mgambo Shooting.

WADHAMINI SOKA

Klabu za soka zinahitaji fedha nyingi ili kujiendesha, na mkoa wa Kilimanjaro licha ya kuwa na wafanyabiashara wengi waliozagaa nchi nzima, lakini wamekuwa wagumu kusaidia timu zao na kusababisha kukabiliwa na ukata. Tuliona huko nyuma timu ya Ushirika ya Moshi ilishindwa kuendelea katika Ligi Kuu kutokana na kushindwa kudhaminiwa na kusababisha kupotea kabisa katika ligi hiyo. Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro wanatakiwa kubadilika sasa na kuisaidia timu yao ya Polisi Tanzania kama wanataka timu hiyo iendelee kuwepo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

NAHOD HA wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, ...

foto
Mwandishi: Yasinta Amos

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi