loader
Picha

Liverpool vs Tottenham Ni fainali ya mafahali wawili England

TIMU mbili zinazoshiriki Ligi Kuu ya England za Tottenham HotSpur na Liverpool ndizo zitakutana katika fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya itakayofanyika Juni mosi mwaka huu.

Liverpool na Tottenham zinakutana baada ya timu hizo kuziondosha Barcelona na Ajax katika mechi za marudiano za nusu fainali. Tottenham wenyewe waliifunga Ajax 3-2 na kusonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya kufungwa 1-0 nyumbani katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Tottenham na matokeo ya jumla kuwa 3-3.

Wakati Liverpool wenyewe ndio wanaonekana kufanya maajabu zaidi baada ya kupindua meza kibabe, licha ya kuwa nyuma kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza na kushinda 4-0 katika mchezo wa marudiano uliofanyika kwenye uwanja wao wa Anfield.

NI TIMU ZA ENGLAND

Fainali ya mwaka huu ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya inazikutanisha timu zinazojuana, ambazo zote zinashiriki katika Ligi Kuu ya England, huku Liverpool ikiwemo katika mbio za kuwania taji, huku Tottenham wenyewe wakifukuzia kumaliza katika nafasi ya tatu au nne. Liverpool wenyewe wana pointi 94, moja nyuma ya vinara na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Manchester City wakisubiri mchezo wa mwisho wa kufunga msimu wa Ligi Kuu, ambao ndio utakaoamua ubingwa.

Man City, wenyewe watamaliza Ligi Kuu wakiwa ugenini kwa kucheza dhidi ya Brighton & Hove Albion wakati Liverpool watamalizia ligi hiyo nyumbani kesho Jumapili kwa kukwaana na Wolverhampton Wanderers. Wengi walikuwa hawaamini Barcelona wenyewe kama Liverpool ingeweza kupindua meza na kubadili kabisa matokeo ya kufungwa 3-0 na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya mabingwa hao wa Hispania wakiwa na nyota wao akiwemo Leonel Messi. Mara nyingi Liverpool wamekuwa wazuri sana kwenye uwanja wao wa Anfield na hasa katika mechi za marudiano.

Kwa mujibu wa kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger anasema Liverpool huwa hatari kwenye Uwanja wa Anfield na aliwatahadharisha Barca kwenda kwa tahadhari kubwa katika mchezo huo wa marudiano, kwani lolote linaweza kuwatokea. Cha ajabu kingine, Liverpool pia walicheza mchezo wao huo wa marudiano bila ya kuwa na baadhi ya wachezaji wake nyota, akiwemo Mohamed Salah ambaye alikuwa majeruhi.

Baada ya kuidhalilisha Barcelona, sasa wengi wanaipa nafasi Liverpool ya kutwaa ubingwa huo, lakini haitakuwa kazi rahisi kwani zinakutana timu zinazojuana vizuri, ambazo zinashiriki ligi moja kwa muda mrefu sasa. Hii itakuwa ni mara ya 11 kwa timu za England kukutana katika fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, huku Liverpool ikiwa imelitwaa taji hilo mara tano na itakuwa ikilisaka kwa mara ya sita. Tottenham wenyewe wanasaka kulitwaa kwa mara ya kwanza taji hilo.

NYOTA TOTTENHAM

Tottenham katika mchezo huo wa nusu fainali ilicheza bila nyota wake Harry Kane, lakini sasa wana matumaini kuwa mshambuliaji huyo nyota atakuwepo katika fainali hiyo itakayofanyika Madrid, Juni Mosi. Kane, ambaye hajacheza tangu Aprili 9 alipoumia kifundo cha mguu, alishuhudia timu yake ikipambana kiume kutoka nyuma kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Ajax na kutoka sare ya 3-3 na kutinga fainali kwa faida ya mabao ya ugenini.

Ajax ilishinda mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika jijini London na kuonekana kama ingetinga fainali kirahisi baada ya Matthijs de Ligt na Hakim Ziyech kufunga mabao na kuifanya timu hiyo ya Uholanzi kuwa mbele kwa jumla ya mabao 3-0. Hata hivyo, mabao matatu au hat-trick ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Lucas Moura, likiwemo lile la ushindi la dakika 96, yaliipeleka Tottenham katika fainali yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Kane, ambaye aliumia katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya michuano hiyo walipocheza dhidi ya Manchester City, aliongeza kusema: “Nimefurahi na najua jinsi gani ilivyo muhimu kwa klabu yetu. “Ilikuwa inakatisha tamaa katika kipindi cha kwanza na tuliwaacha wacheze wao. Na nilienda katika chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko nikiwa (kiwango) hakikuwa kizuri. Tulisema tuna dakikia 45 tu za kufanya kila kitu.”

TIKETI ZA FAINALI

Klabu hizo mbili ambazo zitakutana katika fainali, kila moja imepewa tiketi 16,613 kwa ajili ya mashabiki wake siku hiyo jijini Madrid. Liverpool imetoa maelezo kwa mashabiki wake kuhusu tiketi hizo, ambapo shabiki atatakiwa kulipia kiasi cha pauni 60, ikiwa ni punguzo la asilimia 20. Huku asilimia zingine 54 za tiketi zitauzwa kwa kiasi cha pauni 154, asilimia 21 wakati kwa pauni 385 na asilimia 5 kwa pauni 513. Hata hivyo, Tottenham, ambao wametinga fainali baada ya kuwafunga Ajax, wenyewe hawajatoa maelezo kuhusu bei ya tiketi zao.

Tayari Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) limeshauza tiketi 4,000 kwa mashabiki duniani kote katika uwanja huo wenye kubeba watazamaji 68,000 unaojulikana kama Estadio Metropolitano. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Liverpool kucheza fainali hiyo, ambapo mwaka jana walitinga na kucheza dhidi ya Real Madrid na kufungwa 3-1 katika fainali iliyofanyika Kiev. Wakati huo tiketi ziliuzwa kuanzia pauni 61 hadi 394.

UONGOZI wa klabu ya Chelsea umempa ruhusa kiungo wake N’golo ...

foto
Mwandishi: LONDON, England

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi