loader
Picha

Vyakula vya kula, kutokula mfungo wa Ramadhani

WIKI iliyopita Waislamu nchini walianza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili kutekeleza moja ya nguzo muhimu za dini hiyo.

Katika kipindi hiki cha toba, Waislamu walio katika mfungo wanajinyima na kujizuia katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kula na kunywa hadi kuzama kwa jua.

Pamoja na hayo, wanaanza safari na juhudi mpya zaidi za kuacha mambo machafu na yale yanayokatazwa katika dini hiyo ili mfungo wao uwe na umuhimu kwa kila muumini husika.

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hutumika kufanya ibada kwa unyenyekevu zaidi na kujisafisha kiroho dhidi ya matendo mabaya aliyowahi kuyafanya au ambayo muumini huyo amekuwa akiyafanya. Kimsingi, huu ni mwezi wa toba.

“Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.” (2:183). Hapa Waislamu wote wanalazimishwa kufunga isipokuwa wale wenye udhuru kama wagonjwa na wanawake walio kwenye hedhi. Swahaba mmoja Al-Miqdam ibn Ma’diykarib kasimulia:

“Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi- Mungu akisema, ‘Hajawahi mwanadamu kujaza vibaya chombo chochote kama anavyolijaza tumbo lake. Yanamtosha mwanadamu matonge kadhaa ya kunyoosha mgongo wake. Lakini ikibidi, basi theluthi moja (ya tumbo) iwe kwa ajili ya chakula, theluthi moja iwe kwa ajili ya maji na theluthi moja iwe kwa ajili ya pumzi.”

(Ahmad na Tirmidhi).Kwa mujibu wa uchunguzi, katika mwezi huu, Watanzania wengi waliofunga huitumia nafasi hii kupika mapochopocho au aina nyingi za vyakula wakati wa kufuturu pale jua linapozama, bila kuangalia athari zake kiafya au kuzingatia mafundisho ya dini yenyewe.

Kwa mfano, unakuta mtu amepika mihogo kwa nazi, chapati, vitumbua, magimbi na uji. Kimsingi ukiviangalia vyakula vyote hivi, unagundua ni vyakula vya wanga na humuoni mtu huyu akiwa na mpango wowote wa kula mboga za majani wala matunda. Mara nyingi hali hii huwafanya wengine kesho yake kujawa na gesi tumboni hali inayozorotesha utendaji kazi wake.

Mtu wa aina hiyo mara nyingine katika kipindi hiki cha Mwezi wa Ramadhani, mtu huyo pia hujikuta anaongezeka uzito kupita kiasi; na hata anavimbiwa kiasi cha kushindwa kufanya ibada ambayo ndiyo lengo kuu la Mwezi Mtukufu.

Katika kuwaongoza waumini wa dini ya Kiislamu kwenye vyakula vinavyofaa kufuturu, Kiongozi wa dini hiyo, Mtume Muhammad (S.A.W) anasema: “Fungueni swaumu zenu kwa tende, au vinginevyo, basi fungueni kwa maji, kwani ni twahara.”

Tende hii inaandamana na sunna ya Mtume Muhammad (S.A.W). Waislamu wameelekezwa waanze kula tunda hili wanapofungua kwa sababu lina sukari inayomsaidia mfungaji kupata nguvu kwani siku nzima kutokana na kukaa na njaa, kiwango chake cha sukari bila shaka kinakuwa kimepungua.

Sukari hii inakwenda kwenye ubongo na kumsaidia mfungaji kuondokana na ulegevu wa siku nzima na pia, hufanya glukosi ya mwili kujisawazisha na kumfanya mtu apate nguvu na nuru zaidi ya macho.nguvu na nuru ya macho anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufanya ibada.

Tende pia ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi ambazo huwezesha umeng’enyaji mwilini kuendelea, huzuia tatizo la kushindikana kwa michakato hiyo ya uyeyushaji wa chakula mwilini.

Vilevile, tende ni chanzo kizuri cha potasiamu, madini ambayo ni muhimu kwa usawazishaji wa maji mwilini. Mtume (S.A.W) alikuwa na kawaida ya kula tende kwa idadi ya witiri yaani moja, tatu, tano au saba na kuendelea.

Hivyo, wale ambao hawapendelei ladha ya tende wanaweza kupata manufaa ya chakula hiki kwa kula angalau tende moja, na wale wanaopendelea tende, basi wanaweza kula tatu, tano na kuendelea. Kitu kingine kinachohitajika mwilini kwa mfungaji pindi anapofungua ni maji.

Inafahamika maji ndiyo yanayojenga mwili na mtu anaweza kuishi kwa zaidi ya siku kumi kwa kunywa maji tu, hivyo ni kitu muhimu sana mwilini.

Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wakiwamo wa kisayansi na kiroho, maji yanamfanya mtu apate nguvu ili aweze kufanya ibada na kufanya kazi vizuri. Maji hulainisha koo kutokana na kiu ya siku nzima, lakini pia huondoa uchafu na sumu kutoka mwilini.

Hata hivyo licha ya umuhimu huo wa maji, unapokunywa maji mengi yanaweza kukufanya uvimbiwe ushindwe kula na kufanya ibada, hivyo inashauriwa wakati wa kufuturu kunywa maji glasi moja na baadaye, unaweza kunywa zaidi.

Vilevile, wakati wa kufungua, inashauriwa kunywa chai, kahawa au uji ili tumbo na ubongo vipate kitu cha moto kuweza kushitua baada ya siku nzima kudorora. Pia huzuia maumivu ya kichwa.

Hata hivyo, inatakiwa kuepuka unywaji mwingi wa vinywaji hivi kwani husababisha mtu kwenda sana haja ndogo, hivyo maji kupungua kwa kiwango kikubwa mwilini.

Kinywaji kingine muhimu ni maziwa kwani kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kitaalamu, kinywaji hiki ni chanzo kizuri cha laktosi, madini ya kalsiamu, potasiamu na fosiforasi. Unaweza kutengeneza juisi ya maziwa ukachaganya na tende na hata kuongeza tunda lingine kama parachichi au ndizi.

Matunda nayo hayatakiwi kukosekana kwa kila mfungaji. Hiki ndicho chanzo cha vitamini na madini kama vile vitamin C, potasiamu, folati, majimaji, sukari na nyuzinyuzi.

Wataalamu wa lishe pia wanashauri vyakula vya jamii ya njugu viliwe kwani ni vyanzo vizuri vya kalori nyingi za protini, chuma, vitamin E na mafuta.

Vyakula hivyo ni kama korosho, njugu mawe, karanga na lozi. Unaweza kujiuliza vyakula hivyo vinaliwaje kwani si vyakula vikuu kama mihogo au viazi.

Kwa wanawake, wanaweza kupika njugumawe kwa nazi, vyakula vya sukari wakaweka na lozi, karanga ikatumika mbadala wa nazi kwenye kuunga chakula, biskuti za karanga, juisi ya maziwa na tende ikachanganywa na korosho au karanga.

Baada ya kufuturu, familia ikiwa imekaa inaangalia televisheni inaweza kupata korosho, karanga na lozi na kushushia kwa juisi au chai.

Hata hivyo, inatakiwa kuwa makini na kutokula kwa kiwango kiikubwa vyakula hivi jamii ya njugu kwani kutokana na mafuta yake, husababisha kuongezeka mwili.

Kwa sababu Watanzania wengi wamezoea sana vyakula vya wanga, kipindi hiki ni cha kuwa waangalifu kwani wanga hukaa sana mwilini na kwa sababu wengi wakishafuturu hawafanyi sana kazi ngumu, ni vema kutokula kiwango kikubwa cha wanga.

Wanga husababisha maradhi mengi hasa yasiyoambukiza kama kisukari na unene, hivyo si vyakula vya kupendelea sana.

Katika kila mlo wakati wa kufuturu, ni vizuri kula mboga za majani kwani zina faida sana mwilini na hii inashauriwa na wataalamu wa lishe ifuatwe ama iwe ni katika kipindi cha katika Mfungo wa Ramadhani, au katika siku zisizo za mfungo.

Kwa jumla, muumini aliyefunga anapaswa kula vyenye faida mwilini vya makundi yote na kuhakikisha hali chakula kupita kiasi kwani chochote kinachozidi huwa na madhara.

Ikumbukwe kuwa, Ramadhani si mwezi wa kula na kufanya maonesho ya kula, ujuzi wa mapishi wala kula sana, bali mwezi unaopaswa kutumika kwa ibada kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi