loader
Picha

Majaliwa apokea watalii wengine 330

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewapokea watalii 330 wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka jimbo la Zhejiang, China ambao waliwasili juzi usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 ambao wanatarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu, chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.

Akizungumza na watalii hao kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa kwenye Hoteli ya Mount Meru juzi usiku, Waziri Mkuu Majaliwa alimshukuru Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad Group, Liehui He kwa kuwaunganisha Watanzania na Wachina kupitia mpango wake wa kukuza utalii.

“Mbali na kutuunganisha Watanzania na Wachina, tunakushukuru pia kwa kuamua kuitangaza Tanzania kuwa nchi yenye fursa nyingi za kitalii duniani,” alisema.

Waziri Mkuu alitaja vivutio vingine vilivyopo ambavyo watalii hao wanaweza kuvifurahia kuwa ni mbuga za Ngorongoro, Serengeti, Manyara, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Katavi na akawataka waende visiwa vya Zanzibar kuona fukwe zenye mchanga mweupe na kupata marashi ya karafuu.

Aliwapongeza watendaji wa Bodi ya Utalii na makampuni ya utalii kwa maandalizi na mapokezi mazuri kwa watalii hao.

Pia alimpongeza Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kushirikiana na TouchRoad na kuifanya Tanzania ipokee watalii wengi.

Akielezea ujio wa kundi la kwanza la watalii, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini, Devotha Mdachi alisema watalii hao wametokea Djibouti ambako walikaa kwa siku moja, na hapa nchini watakaa kwa siku nne na kisha wataelekea Bulawayo, Zimbabwe ambako watakaa kwa siku mbili na kurejea China.

Mapema, akizungumza katika mkutanohuo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema ujio wa watalii hao ni sehemu ya mpango mkubwa wa nchi wa kuongeza watalii kutoka China unaofahamika kama Tour Africa - The New Horizon.

Aliwataka Watanzania wachangamkie fursa ya ujio wa wageni ili waweze kunufaika kiuchumi.

“Naomba niwasihi Watanzania, hii ni fursa hatuna budi kuichangamkia ili wao wafurahie utalii nchini lakini nasi tunufaike na uwepo wao.”

ILI kukabiliana na ugonjwa wa Covid- 19 unaosababishwa na virusi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi